The House of Favourite Newspapers

Kibarua Cha Kaze Yanga Hiki Hapa

0

HABARIya mjini kwa sasa ndani ya Yanga ni ujio wa kocha mpya wa timu hiyo Cedric Kaze, ambaye anatarajia kutua nchini kesho Alhamisi akitokea nchini Canada.

Kaze ambaye ana historia nzuri na soka la Ulaya kufuatia kuwahi kufundisha Akademi ya FC Barcelona, anatarajia kutua nchini kukisimamia kikosi cha Yanga kuweza kutimiza ndoto yake ya kutwaa ubingwa msimu huu baada ya kuukosa kwa misimu mitatu mfululizo.

 

Championi Jumatano linakuchambulia mambo kadhaa ambayo Kaze anatakiwa kuyatimiza ndani ya timu yake hiyo mpya ili kuweza kuendelea kudumu katika kikosi hicho.

KUIFUNGA SIMBA

Mtihani wa kwanza kwa Kaze utakuwa Novemba 7 katika mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga itakayochezwa katika Uwanja wa Mkapa jijini Dar.

Mara nyingi mechi kama hii ya watani wa jadi huwa na mihemko kutoka pande zote mbili kwa Simba na Yanga ambapo wote wanahitaji ushindi.

Mechi hii huwa inachukuliwa uzito wa hali ya juu kwenye ligi kuliko mechi zozote wanazocheza watani hao, hivyo kocha yeyote atakayefanikiwa kumfunga mpinzani wake ndiye anaonekana kuwa bora na wakati mwingine hufikia hadi baadhi ya makocha wanafungashiwa virago vyao, hivyo mchezo huo utakuwa kipimo cha kwanza kwake katika timu yake hiyo mpya.

Mechi ya Novemba 7 itakuwa ni ya nne kwa watani hao kukutana katika mwaka huu wa 2020 ambapo mchezo wa kwanza uliochezwa Januari 4, timu hizo zilivyokutana kwenye ligi na matokeo yalikuwa 2-2, mchezo wa marudiano uliochezwa Machi 8, Yanga waliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Bernard Morrison na mchezo wa mwisho waliokutana kwenye FA Simba ilishinda mabao 4-1.

UBINGWA Yanga haijatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa misimu mitatu mfululizo, 2017/18, 2018/19 na 2019/20 ambapo misimu yote hiyo ubingwa umeenda kwa watani zao Simba.

 

Hivyo basi moja ya kazi iliyokuwa mbele ya Kaze, ni kuhakikisha anafanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi msimu huu wa 2020/21 ambapo ndipo kutamjengea mazingira mazuri ya kuweza kuendelea kubaki katika kikosi hicho na iwapo atashindwa, basi kuna uwezekano mkubwa asiweze kuendelea kubaki kwa kuwa Wanayanga kiu yao ni moja tu, ubingwa wa ligi.

 

Yanga inahitaji kutwaa kombe la FA msimu huu kwani msimu uliopita kombe hilo lilikwenda kwa watani wao Simba ambao waliwatoa katika hatua ya nusu fainali kwa mabao 4-1, hivyo moja ya matumaini ya Wanayanga ni kuona Kaze anafanikiwa kutwaa kombe hilo la FA hasa kutokana na rekodi yake.

 

POINTI TATU KATIKA KILA MECHI

Yanga ilishindwa kufanya vizuri msimu uliopita wa 2019/20 na kujikuta ikimaliza katika nafasi ya pili ya msimamo wa ligi ikiwa na pointi 72 huku Simba walitwaa ubingwa wakimaliza na pointi 88 ikiwa ni tofauti ya pointi 16.

 

Yanga ilishinda michezo 19 kati ya 38 iliyocheza huku ikijikuta ikitoa sare michezo 15 na kupoteza michezo minne, hivyo Kaze anatakiwa kuonyesha uwezo wake katika kukiimarisha kikosi chake ili kiweze kuendana na kasi ya ligi na kufanikiwa kupata pointi tatu katika kila mchezo ili kuepukana na matokeo ya msimu uliopita.

 

KUREJESHA HESHIMA YA YANGA

Yanga ya sasa sio ile ya misimu mitatu nyuma iliyopita ambapo ilikuwa ikiitwa Yanga ya kimataifa chini ya aliyekuwa mwenyekiti wake, Yusuph Manji ambapo Yanga ilikuwa moto.

 

Kwa sasa uongozi wa Yanga umejitaidi kufanya usajili wenye kiwango cha hali ya juu kwa kuleta nyota wenye viwango wakiwemo kina Mukoko Tonombe na Tuisila Kisinda ili kuboresha kikosi hicho, hivyo uwepo Kaze unaleta matumaini makubwa ya kubadili kikosi hicho hasa ukizingatia asilimia kubwa ya nyota waliotua kikosini hapo amewaleta yeye.

 

 

KUIMARISHA NIDHAMU

Kocha atakuwa na kazi ya ziada kuhakikisha anaimarisha nidhamu ndani ya kikosi ikiwa ni pamoja na kuwaunganisha wachezaji ili wafanye vizuri kwenye kila mechi, kwani iwapo hakutakuwa na nidhamu ndani ya timu basi hawataweza kufanya vizuri.

 

MATOKEO YA YANGA KWENYE LIGI

Hadi sasa Yanga ambayo ipo nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 13 sawa na Simba wakipishana kwa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa, huku Azam ikiongoza msimamo kwa kuwa na pointi 15, Yanga imeshinda michezo minne, imetoa sare mchezo mmoja, imefunga mabao saba na kufungwa bao moja.Mechi ambazo imecheza hadi sasa ni dhidi ya Tanzania Prisons 1-1, Mbeya City 1-0, Mtibwa Sugar 1-0, Kagera Sugar 1-0 na Coastal Union 3-0.

STORI: KHADIJA MNGWAI | CHAMPIONI

Leave A Reply