The House of Favourite Newspapers

Kifafa chamharibu Kijana Pua, Macho

0

OMARY MBALALE AKIWA NA MWANDISHI WA HABARI HII
Kijana Omar Said Mbalale akiwa ameharibiwa pua baada ya kuugua ugonjwa wa kifafa.

Stephano Mango, Amani

RUVUMA: Kweli hujafa hujaumbika, ndivyo unavyoweza kusema ukikutana na Omar Said Mbalale (30), mkazi wa Kijiji cha Libango wilayani Namtumbo ambaye anateseka baada ya macho na pua kuharibika kufuatia ugonjwa wa kifafa.
Akizungumza na gazeti hili juzi, Omar alisema ugonjwa huo ulimuanza mwaka 2009 ambapo alipata matibabu bila mafanikio kutokana na kukosa pesa za kutosha kiwango cha dawa.

Umeendelea kumtesa mpaka sasa bila kupatiwa matibabu ya uhakika na kwamba Juni 3, mwaka 2015 ndipo alipokumbana na balaa kubwa.
“Siku hiyo familia ilikwenda shamba, mimi nikabaki nyumbani. Niliachiwa chakula jikoni. Niliposikia njaa, niliamua kuingia jikoni ili nipakue chakula.

“Ghafla niliangukia kwenye jivu la moto jikoni na kupoteza fahamu kwa muda mrefu mpaka ndugu zangu waliporudi na kuniokoa. Walinipa huduma ya kwanza kabla sijapelekwa kwenye Kituo cha Afya cha Wilaya ya Namtumbo kwa matibabu, baadaye nikahamishiwa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Ruvuma,” alisema Omar.

DSC_0492Omar alisema kuwa, alilazwa katika hospitali hiyo kwa muda mrefu mpaka majeraha yaliyotokana na jivu la moto yalipopona na kuruhusiwa kurudi nyumbani kwa ajili ya kujipanga kuelekea Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi ya kifafa na kufanyiwa marekebisho ya uso.
Alisema kutokana na hali hiyo, alikwenda wilayani Namtumbo na Songea mjini ili aweze kupata msaada kutoka kwa wasamaria wema na taasisi mbalimbali za binafsi na serikali kwa lengo la kupata fedha  ili aweze kufanikisha matibabu ya maradhi yanayomsumbua. 
“Januari 29, mwaka huu nilifika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Songea na kupata kibali cha kuomba michango kutoka kwa wasamaria wema na taasisi. Kibali chenye kumbukumbu Na. AB 308/398/01/176.

“Nateseka sana, nimekuwa nikipata fedha kidogo ambazo nakula nyingine nanunulia dawa kutokana na maradhi niliyoyapata ya kulala nje na vumbi linaloniingia puani na machoni,” alisema Omar.
Akasema yeyote atakayeguswa na matatizo yake, anaweza kumchangia kupitia simu namba 0755-335051 na 0715-335051.
Omar alimaliza elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Libango wilayani Namtumbo mwaka 1999 akiwa ni mtoto wa pili kati ya watoto 6 wa mzee Said Mbalale Kulasa.

Leave A Reply