The House of Favourite Newspapers

Kifo cha Kanali Mamadou Ndala Chamuibua Hayati Magufuli Kongo

0

Ni miaka nane sasa imepita tangu kifo cha Kanali Mamadou Mustafa Ndala, kiongozi wa kijeshi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), aliyeongoza mapambano ya kuwang’oa waasi wa M23 na makundi mengine yaliyokuwa tishio kubwa nchini humo.

Mamadou Ndala aliuawa Januari 2, 2014 baada ya kushambuliwa na waasi wa Kundi la ADF NALU la nchini Uganda kilometa 10 kutoka Mji wa Beni, Kivu Kaskazini baada ya msafara wake kuvamiwa ghafla na waasi waliofyatua risasi na mabomu na kusababisha kifo chake, walinzi wake wawili na maafisa wengine wa jeshi la DRC.

Ni kawaida kwa Wakongomani kuadhimisha kifo cha mwanajeshi huyo shupavu aliyekuwa kipenzi cha wengi, kila ifikapo Januari 2 ya kila mwaka ambapo tofauti na miaka mingine yote, maadhimisho ya mwaka huu, yamemuibua Hayati Dokta John Pombe Magufuli.

Wananchi wa DRC waliozungumza na mwandishi wetu, Jistee Kabumba kutoka Mji wa Goma, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wamemuelezea Hayati Magufuli kama mtu ambaye alikuwa na moyo wa kijasiri kama Kanali Mustafa Ndala, mzalendo wa kweli na mwenye uchungu na nchi yake.

Kanali Mamadou Ndala aliyezaliwa Desemba 8, 1978 katika Mji wa Ibambi, Jimbo la Wamba, alizikwa Januari 6, 2014 jijini Kinshasa na miaka kadhaa baada ya kifo chake, alipandishwa cheo na kutangazwa kuwa Brigedia Jenerali, kama heshima kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kupambana na waasi nchini humo.

Leave A Reply