The House of Favourite Newspapers

Kifo Mikononi Mwangu (Sehemu ya 8)

ILIPOISHIA IJUMAA…

NIKAKATA simu na kusimama.

“Yule mtu tunayemtafuta ameshafika pale baa. Acha twende tukamkamate,” nikamwambia mke wangu.

SASA ENDELEA…

MKE wangu hakushangaa. Alikuwa akizijua kazi zetu za kijeshi kwa vile yeye mwenyewe alikuwa polisi. Polisi unaweza kuamshwa saa nane usiku, ukaambiwa unatakiwa kituoni. Hapo unamuacha mkeo au mumeo bila kujali mlikuwa mnafanya nini na kuitikia wito.

Kwa vile sikuwa katika zamu ya kazi, nilikwenda vilevile na nguo zangu za kiraia. Koti jeusi la mtumba, shati jekundu na suruali ya kijivu.

Nilipofika kituoni nilimfahamisha aliyekuwa akisimamia kituo usiku ule kwamba nimepigiwa simu na msichana mhudumu wa Baa ya Nane Nane kwamba Mdachi ambaye alikuwa mtuhumiwa tunayemtafuta, ameshafika hapo baa. Nilipewa gari na polisi wanne nifuatane nao wakiwa na bunduki mikononi.

Tulipofika nilishuka peke yangu nikaingia baa. Nilikwenda moja kwa moja kaunta ambapo nilimkuta yule msichana aliyenipigia simu.

“Yuko wapi?” Nikamuuliza kwa pupa.

“Mmechelewa, ameshaondoka.”

Nikamkunjia uso na kumuuliza.

“Unasemaje?”

“Ameondoka sasa hivi hata bia yake hakuimaliza.”

“Mmemshtua?”

“Kuna msichana alimwambia kuwa Matilida ameuawa jana usiku akataharuki.”

“Nilisema msimueleze kitu.”

“Ulinieleza mimi, lakini hapa tuko wengi. Kuna msichana alimwambia. Nafikiri alikuwa hajui kama Matilida amekufa, asingetaharuki vile.”

“Sasa amekwenda wapi?”

“Inaelekea hakuamini kama Matilida amekufa, ameondoka kwenda nyumbani kwake kuhakikisha kama amekufa kweli!”

“Naona kama alikuwa anazuga tu, yeye ndiye tunayemtuhumu halafu anajifanya kuwa hajui, hajui nini?”

Msichana huyo alinyamaza kimya.

“Aliondoka sasa hivi?” Nikamuuliza.

“Ni sasa hivi tu. Huko nyumbani kwa marehemu pia atakuwa hajafika.”

“Ana usafiri gani?”

“Wakati mwingine anakuja kwa pikipiki, wakati mwingine anatumia miguu, sijui leo alikuja kwa usafiri gani.”

Nikatoka bila kumuaga msichana huyo. Nilipotoka nje niliwaambia wenzangu.

“Huyu jamaa ameshaondoka, nimeambiwa amekwenda nyumbani kwa marehemu, tumfuate hukohuko.”

Nilifungua mlango wa gari nikajipakia. Gari la polisi likaondoka.

“Ni wapi?” Polisi aliyekuwa akiendesha gari hilo akaniuliza.

“Twende Kwaminchi.”

Hapo Gofu na Kwaminchi ni kama pua na mdomo. Palikuwa karibu sana. Dereva alikata kushoto. Baada ya mwendo mfupi tu tuliingia eneo la Kwaminchi. Nilimuelekeza mtaa aliokuwa akiishi marehemu. Tulipofika katika nyumba ya marehemu tuliona msichana aliyekuwa amesimama barazani.

Tulisimamisha gari nikashuka na kumsalimia msichana huyo.

“Hujambo?”

“Sijambo. Shikamoo.”

Katika mazingira ya kawaida hakupaswa kuniamkia kwa vile kama tulipishana ilikuwa ni kidogo tu. Lakini nilifahamu aliniamkia kutokana na uoga wa kuona polisi.

“Marahaba. Wewe nani, mbona uko hapa?” Nikamuuliza.

“Mimi ni rafiki yake Matilida. Nilikuja kumsalimia, lakini naona nyumba imefungwa.”

“Unaishi wapi?”

“Naishi Chumbageni.”

“Hujakutana na Matilida tangu lini?”

“Tangu juzi.”

Nilinyamaza kimya nikawaza kidogo kisha nikamwambia.

“Matilida ameuawa usiku wa jana. Kwa hiyo hutaweza kuonana naye tena.”

“Kuna mtu alikuja hapa nyumbani sasa hivi, akaniambia amekwenda kazini kwake Matilida na kuambiwa Matilida ameuawa, lakini hakuamini, akaja hapa nyumbani kwake kuthibitisha. Mimi nikamwambia sijui.”

“Huyo mtu yuko wapi?”

“Baada ya kuona nyumba imefungwa ameondoka.”

“Ni muda gani aliokuja?”

“Ni sasa hivi tu. Hata mimi nilikuwa naondoka.”

Nikahisi huyo mtu alikuwa ni Mdachi.

“Alikuwa na usafiri gani?”

“Alikuwa akiendesha pikipiki.”

“Alipoondoka alielekea wapi?”

“Alielekea huo upande mliotokea ninyi.”

Nikamuacha yule msichana na kurudi kwenye gari.

“Huyu jamaa amefika hapa na ameshaondoka. Huenda amerudi tena kule kule baa. Turudi tena,” nikawaambia polisi wenzangu.

Tukageuza gari na kurudi tena kwenye ile baa. Kama kawaida nilishuka peke yangu. Nikaingia ndani. Nilimfuata yule mhudumu wa kaunta nikamuuliza.

“Yule mtu alirudi tena hapa baa?”

Msichana akatikisa kichwa.

“Hajarudi tena. Kwani hamkukutana naye?”

“Hatukukutana naye. Tuliambiwa alifika na kuondoka, tukadhani amerudi huku.”

“Huku hajafika bado.”

Baada ya kuzugazuga hapo baa, nikatoka na kujipakia kwenye gari.

“Naona bora turudi, safari yetu haikuwa na mafanikio.”

Tulipofika kituoni nilimfahamisha msimamizi wa kituo kwamba hatukufanikiwa kumpata Mdachi. Polisi wenzangu waliendelea na kazi, mimi nikarudi nyumbani kwangu.

Mke wangu alikuwa ameshalala. Nilibisha mlango, akaja kunifungulia. Niliingia ndani tukasimama sebuleni kidogo.

“Vipi mmemkamata?” Akaniuliza.

“Hatukumpata.”

“Kwa nini?”

“Kuna mtu alimwambia kuwa Matilida ameuawa, akaondoka pale baa na kwenda nyumbani kwake. Sisi tulipofika tukaambiwa ameondoka. Tulipofika nyumbani kwa marehemu tukaambiwa alifika na kuondoka.”

“Inaonesha wazi huyo jamaa siye aliyeua.”

“Kwa nini?”

“Kama ni yeye kwa nini alipoambiwa Matilida ameuawa aliondoka na kumfuata nyumbani kwake!”

“Binadamu wajanja. Inawezekana alikuwa anawazuga wale wasichana ili asifahamike kuwa amemuua yeye.”

“Haya, mbivu na mbichi zitafahamika mtakapompata.”

Mke wangu akaingia chumbani.

Kusema kweli usiku huo sikupata usingizi kwa mawazo. Wakati mwingine mtu anakupa ushauri unaukataa halafu baadaye unagundua alikupa ushauri wa maana.

Mke wangu aliniambia nisiende katika ile sherehe ya harusi kule Mkonge Hoteli, nikakataa. Baada ya kwenda nilichokutana nacho kinanifanya nijute kutosikiliza ushauri wake.

Kama ningemtii na kutokwenda, nisingekutana na mkasa ule. Na moyo wangu ungekuwa umetulia. Sasa nimefikwa na kizungumkuti kiasi kwamba sielewi muuaji halisi alikuwa nani. Mwanzo niliamni asilimia kwa mia kwamba muuaji alikuwa Mdachi kutokana na vigezo mbalimbali.

Lakini sasa zile asilimia za kumtuhumu Mdachi kuwa muuaji zimekuwa zikipungua kidogodogo. Kile kitendo cha Mdachi kuambiwa kuwa Matilida ameuawa na yeye akataharuki na kuamua kumfuata nyumbani kwake, kinaonesha alikuwa hajui kuwa Matilida ameuawa. Na kama alikuwa hajui kama Matilida ameuawa, maana yake ni kwamba si yeye aliyemuua.

Katika kuwazawaza kwangu, nikamkumbuka mtu mmoja muhimu sana.

Unajua nilimkumbuka nani?

Nilimkumbuka Azzali Mubarak, mfanyabiashara ya magendo ya meno ya tembo ambaye aliwahi kushitakiwa na kuachiwa na mahakama kwa kukosekana kwa ushahidi wa kutosha.

Nilimkumbuka kutokana na maneno aliyoniambia alipoachiwa na mahakama.

Alinikuta nimesimama nje ya mahakama, akaniambia.

“Ulinikamata kwa kunionea tu.”

“Unasemaje?” Nikamuuliza nikiwa nimemkunjia uso.

“Nimekwambia ulinikamata kwa kunionea tu.”

“Kumbe ulitaka tukuachie hata kama unashukiwa?”

“Kuwa na roho mbaya haitakusaidia.”

“Kama mahakama imekuachia, shukuru Mungu. Usinilaumu mimi. Mimi niko kazini.”

“Sawa. Tutaonana.”

Nikashtuka. “Tutaonana kwa heri au kwa shari?” Nikamuuliza.

Azzal Mabruki hakujibu kitu, akaelekea kwenye gari lake la kifahari lililokuwa likimsubiri hapo mahakamani. Akajipakia na kuondoka. Wakati gari linaondoka alinipungia mkono wa kuniaga. Nikampuuza.

Sasa nilianza kupata wasiwasi kutokana na yale maneno aliyoniambia. Nikajiambia isije kuwa ni yeye aliyesuka mpango huu wa kuuawa kwa Matilida ili anitie mimi katika balaa!

Je, nini kiliendelea? Usikose Jumatatu kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda.

Comments are closed.