The House of Favourite Newspapers

Kigogo Chuo Kikuu Aliyekaa Mahabusu Miaka 7, Ahukumiwa

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu, Marietha Milinga kulipa fidia ya Sh12.9 milioni na kifungo cha nje cha miezi sita baada ya kukutwa na hatia ya kukisababishia hasara Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).

 

Milinga, amehukumiwa baada ya kukiri kosa. Alifanikiwa kulipa kiasi hicho cha fedha na atatumikia kifungo hicho cha nje. Alikiri shtaka la kusababishia hasara katika makubaliano na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).

 

Akisoma hukumu hiyo Hakimu Mkazi mwandamizi, Agustine Rwezile amesema mshtakiwa ametiwa hatiani, anatakiwa kuilipa Serikali Sh 12.9 milioni.

“Mbali na kulipa fidia hiyo, pia mshtakiwa atatumikia kifungo cha nje cha miezi sita,” amesema Hakimu Rwezile.

 

Amebainisha kuwa ametoa hukumu hiyo kwa kuzingatia maombi ya mshtakiwa kuwa ana mtoto mgonjwa na ni kosa lake la kwanza. Awali, mshtakiwa huyo aliyekuwa akikabiliwa na mashtaka 69 yakiwemo ya utakatishaji fedha baada ya kufanya makubaliano na DPP alisomewa shtaka moja la kukisababishia hasara chuo hicho.

 

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, wakili wa Serikali, Jackline Nyantori ameiomba mahakama kutoa adhabu kwa mshtakiwa na kuzingatia makubaliano waliyoingia na DPP.

 

“Naomba mahakama itoe adhabu kali dhidi ya mshtakiwa huyu ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hii pamoja na kulipa fidia ya hasara aliyoisababishia Serikali,” amesema wakili Nyantori.

 

Katika utetezi wake, mshtakiwa huyo aliyekaa mahabusu miaka saba, aliiomba mahakama isimpe adhabu kubwa kutokana na kukaa mahabusu muda mrefu na ana mtoto mdogo mwenye maradhi ya saratani.

 

Katika kesi hiyo, Marietha na wenzake wanadaiwa kati ya Julai 2009 hadi Aprili 2011 walikisababishia hasara chuo hicho zaidi ya Sh. 500 milioni.

Comments are closed.