The House of Favourite Newspapers

Kigoma All Stars Gari Limeishiwa Mafuta au Dereva Amesinzia?

0
Staa wa Bongo Fleva, Ommy Dimpoz.

BRIGHTON MASALU | RISASI MCHANGANYIKO | MAKALA

ALHAMISI mchana. Wingi wa watu hususan vijana wakiwa kimya kabisa, unanipa hamasa ya kutaka kujua nini kinaendelea. Lengo la kwenda kwenye saluni hiyo, ni kunyoa lakini nakutana na picha ya tofauti, watu wanafuatilia jambo moja. Ni Julai 9, 2012 saa 12: 57, moja kwa moja nalazimika kuingia ndani kusikiliza kilichoteka akili za vijana, ilikuwa kijijini kwetu, Buligi mkoani Geita.

Ni siku ambayo wimbo mpya ulioimbwa na wasanii wenye uwezo wa hali ya juu kabisa, wenye asili ya Mkoa wa Kigoma, uliopewa jina la Leka Dutigite unasikika kwa mara ya kwanza. Wimbo wa Leka Dutigite uligeuka wa taifa.

Staa wa bongo Fleva Chege.

Maudhui yake yalivutia kwa mazingira matatu makubwa. Kwanza, ujumbe ulioimbwa wa kusifia Mkoa wa Kigoma, kwani ni wazi kuwa watu wengi wamekuwa wakiubeza na kuudharau sana mkoa huo. Lakini sifa ambazo ziliimbwa kwenye wimbo huo ulibadili fikra za Watanzania wengi waliokuwa na mabezo kuhusu mkoa huo ambao kwa uhalisia una rasilimali nyingi za kimaendeleo.

Pili, kama nilivyosema hapo juu, muungano wa wasanii wengi wenye uwezo mkubwa, mchanganyiko wa sauti zao na ufundi waliouonesha kuhakikisha kila mmoja anang’ara kupita wenzake, ulileta chachu mpya kwenye ubongo wa wadau wa burudani ya muziki.

Mtifuano ulisisimua na binafsi sijawahi kuona wimbo kwa hapa nyumbani, ulioimbwa na wasanii wengi wenye uwezo kiasi hicho, ukiondoa ule wa Uhuru wa miaka kadhaa iliyopita, zaidi ya robo tatu ya wasanii wote bila kujali mikoa wanayotoka waliungana na kuimba pamoja.

Staa wa muziki wa Bongo Fleva, Linex Sunday.

Wasanii hawa wa Kigoma, waliunda kundi na kulipa jina la Kigoma All Star, likijumlisha vichwa vya kazi kama Chegge, Abdu Kiba, Banana zorro, Mwasiti, Baba Levo, Peter Msechu, Rachel, Muba, Muki, Linex, Ommy Dimpoz na wengine wengi! Nataka tusemezane kidogo nyie wasanii mliounda kundi hili.

Ujio wenu, ulishtua wengi ndiyo maana hata mikoa kama Mwanza na Morogoro nao wakaingia kwenye mkumbo wa kuunda makundi na kuimba nyimbo za pamoja, ingawa nao hawakudumu, lengo la kuzungumza na nyinyi, sababu kubwa ni mbili tu. Kama waasisi na ukubwa wa majina yenu.

Mlitoa nyimbo mbili, wa kwanza ukiwa wa Leka Dutigite na pili mliimba mkiupigia chapuo Mfuko wa Hifadhi wa Jamii, National Social Security Fund (NSSF). Sisi tuliendelea kuwa na matarajio makubwa kwamba, zipo ngoma zingine nyingi ambazo zitafuatana kama mvua za vuli. Lakini tofauti na matarajio, tulianza kuona ukimya na kila mmoja akifanya mambo kivyake.

Msanii wa Bongo Fleva, Mwasiti Alimasi.

Leo imepita miaka mingi (mitano), bado mko kimya na habari zisizokuwa na chembe ya shaka hamko pamoja kwa maana ya kwamba kundi halipo tena! Visa vikitajwa kwa wingi wa porojo, lakini kubwa ni kujiweka pembeni kwa Zitto Kabwe pamoja na migogoro ya ninyi kwa ninyi, dharau za kujiona bora kuliko wengine na mambo mengi yenye mfanano huo.

Maswali yamekuwa mengi Hivi karibuni, nilimsikiliza Baba Levo kwenye moja ya mahojiano na redio moja, akidai kuwa sababu zilizoua kundi ni mtafaruku wa wasanii wawili waliomo kweye kundi hilo, wenye majina makubwa sana hapa nchini, hali iliyowavunja moyo wengine, sababu ambayo baada ya kuichuja kwa mapana na marefu, haina mashiko hata kidogo.

Staa wa muziki wa Bongo Fleva anayeupiga kwa njia ya bendi, Banana Zahir Zorro.

Swali la kwanza ni, je, muungano wa Kigoma All Star ulikuwa wa masilahi ya muda? Ilikuwa nguvu ya soda au mpango mahususi uliokuwa umesukwa kwa lengo maalum? Kama lengo lilikuwa moja kuwakilisha mkoa katika anga la muziki, mbona imekuwa kidogo sana tofauti na matarajio? Nani kiongozi mkuu wa kundi hili?

Kama ni Mbunge Kabwe kama inavyotajwa, ni nini kimempata na kuacha kusimamia kundi hili lenye wasanii bora? Halafu, kama Kabwe ndiye kiongozi, inakuwaje akosekane miongoni mwenu kuwa kiongozi na kumuacha aendelee kutumikia wito wake wa siasa? Mbona gari lenu liliwaka kwa mbwembwe na kuanza safari kwa kasi ya kufurahisha na matumaini makubwa ya kufika mwisho wa safari? Nini kimempata dereva wa gari lenu? Au tatizo liko kwenye gari kwamba limeishiwa mafuta?

ONDOKENI NA OFA HII

Akili yenu ibebe mimba na izae ukweli huu vichwani mwenu; ninyi ni watu muhimu mno katika anga hili la muziki wa kikwetu. Umoja wenu una utofauti mkubwa kwani umebeba vichwa vyenye vipaji kushinda wengine Tanzania nzima. Kama Kabwe alikuwa mwanzilishi wa wazo la kuunda kundi, hata kama amekaa pembeni, achaneni naye. Itaneni muanze upya, tazameni mlianguka wapi na nini kilisababisha kupotea kwenu kama kundi na kuanzia hapo mjiwekee mipango na kanuni madhubuti zitakazowasimamisha kwenyeramani na kuleta mapinduzi yakinifu, kuliko yale ya mwanzo. Chukueni hii; Kabwe ameitiwa siasa, ninyi mmeitwa kuimba.

Kila mmoja aheshimu wito wake na asimame sawasawa na mapenzi ya aliyempa kipaji. Mimi sina asili ya Mkoa wa Kigoma, lakini hadi leo nikiusikia Wimbo wa Leka Dutigite, mara nyingi hulazimika kuacha kazi ninayoifanya na kuanza kuusikiliza tena. Hauishi utamu.

Nini kiliwapata Kigoma All Star? Linex yupo, Chegge yupo, Banana Zorro kajaa tele. Abdu Kiba kila siku anashinda mitaa ya Kariakoo, Mwasiti hakauki mitaa ya Kinondoni, Baba Levo ndiyo kabisaaa, yeye hata makazi yake yapo Kigoma mjini, maana ni mwakilishi wa wananchi katika Kata ya Mwanga. Binafsi nataka niwaambieni kwa Kabila la Kiha: “Mwansizye nkaakazebha omchali katagilka nyina” (mmeniacha kama kifaranga kwenye kiota kisichokuwa na mama).

Kama tatizo ni dereva wa gari lenu, muamsheni atoke usingizini na kama ishu ni gari, lipelekeni gereji na safari iendelee. Natafuta nafasi nzuri, niwatafute ana kwa ana, tuzungumze kwa kirefu maana wengi wenu tuna uhusiano hata nje ya kazi. Ndimi Mjenzi wa Taifa kupitia Kalamu (MTK), 0673 42 38 45.

Leave A Reply