The House of Favourite Newspapers

Kiiiza hafai hata kidogo

0

Mohammed Mdose, Dar es Salaam
KATIKA kuonyesha kuwa yupo kikazi zaidi, mshambuliaji wa Simba, Hamisi Kiiza, amezidi kuonyesha mavitu yake kwenye mechi za Ligi Kuu Bara na kuweka bonge la rekodi.

Kiiza ambaye kwa sasa ndiye anaongoza kwenye chati ya wafungaji kwenye ligi kuu akiwa na mabao 19, ameweka rekodi mbili mara baada ya bao lake alilolifunga juzi Jumamosi kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Rekodi ya kwanza ni ile ya kuwa mchezaji aliyezifunga timu zote zinazotokea Tanga ambazo ni Mgambo JKT, Coastal Union pamoja na African Sports. Amefanya hivyo katika mechi zote mbili za mzunguko wa kwanza na wa pili.
Rekodi ya pili ni kuiwezesha timu yake kushinda mara zote tatu aliposhuka kucheza kwenye Uwanja wa Mkwakwani ambao mastraika wengi wameshindwa kufunga kwa kuulalamikia kuwa ni mbovu.

Kiiza alianza kufungua ukurasa wa rekodi hizo kwenye Uwanja wa Mkwakwani waliposhinda 1-0 mbele ya African Sports, kisha kwenye ushindi wa 2-0 dhidi ya Mgambo alipiga bao moja, na juzi Jumamosi akapiga bao kwenye ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Coastal.

Pia Simba ilipopata ushindi wa bao 1-0 mbele ya Coastal kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, Kiiza ndiye aliyepiga bao hilo, kisha akapiga mawili kwenye ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya African Sports na akafanya tena kwenye ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Mgambo ambapo alipiga mawili. Kwa jumla Kiiza amezifunga timu hizo mabao nane.

Leave A Reply