The House of Favourite Newspapers

Kikundi cha Taarifa na Maarifa cha TGNP Kivule Kilivyoendesha Bunge la Jamii Mtaani

0
Mwenyekiti wa Kikundi cha Taarifa na Maarifa Kata ya Kivule, Zahra Omary akifungua bunge hilo kabla ya kuwapata viongozi.

 

 

 

Kikundi cha Taarifa na Maarifa cha Kata ya Kivule Wilaya ya Ilala jijini Dar, kilichoundwa na Mtandao wa Jinsia wa TGNP sambamba na vikundi vingine kama hivyo nchi nzima kimeendesha bunge la jamii ambalo limefanyika Desemba 31 mwaka 2021, kwenye Viwanja vya Stendi ya Mbondole.

Sehemu ya washiriki waliohudhuria bunge hilo.

 

 

 

MCHAKATO WA KUMPATA SPIKA WA BUNGE

Katika bunge hilo lililohudhuriwa na wakazi wa eneo hilo kama ilivyokawaida ya mabunge mengine lilianza na mchakato wa kumchagua spika wa kuliongoza bunge hilo ambapo mkazi wa eneo hilo, Bahati Mwaseba ndiye aliyeibuka na bahati hiyo.

Spika wa Bunge hilo, Bahati Mwaseba akiendelea na majukumu yake baada ya kuchaguliwa kuliongoza bunge hilo.

 

 

 

MAWAZIRI WALIVYOPATIKANA

Baada ya kupatikana spika wa bunge hilo, Spika Bahati kwa kushirikiana na wabunge jamii waliojitokeza kushiriki kwenye bunge hilo walianza mchakato wa kuwatafuta mawaziri ambao baada ya kupatikana walikuwa na jukumu la kujibu hoja za wabunge kwa kushirikiana na viongozi wa serikali ya mtaa ambao nao walialikwa kama wajibu hoja wakuu kwenye maswali yaliyoibuliwa na wabunge jamii.

Mawaziri katika bunge hilo wakibadilishana mawazo kabla ya kuanza kujibu hoja za wabunge wa jamii.

 

 

 

BUNGE LILIVYOANZA KAZI RASMI

Baada ya kupatikana viongozi hao bunge lilianza ambapo kama kawaida wabunge wa jamii walianza kuuliza maswali mbalimbali yaliyoibua changamoto kwenye bunge hilo ambapo mwisho wa yote yalipokelewa na viongozi wa serikali za mitaa katika kata hiyo ambapo waliahidi kuyapeleka serikali kuu kwa ajili ya utatuzi.

Mbunge wa jamii akiuliza maswali mbalimbali kwenye bunge hilo na kuitaka serikali kueleza kuwa ina mpango gani na kata ya Kivule kukosa High school? Kushoto ni viongozi wa serikali za mitaa wakimsikiliza.

 

 

 

UKOSEFU WA HIGH SCHOOL KIVULE

Mmoja wa washiriki wa bunge hilo aliibua changamoto ya ukosefu wa high school kwenye kata hiyo jambo linalosababisha wanafunzi wa kata hiyo wanapofaulu elimu ya sekondari kupelekwa shule za mbali jambo linawasababishia gharama kubwa ya kwenda na kurudi huku wakitumia muda mwingi njiani jambo linalosababisha kupunguzia ufanisi wao.

Chamoto hiyo ilianza kujibiwa na Waziri wa Elimu katika Bunge hilo, Prisca Dominic lakini pia lilipokelewa na viongozi wa mitaa ya kata hiyo ambapo waliahidi kumpelekea diwani wa kata hiyo kwa ajili ya kulipeleka kwenye halmashauri.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kerezange Kata ya Kivule, Ismail Ibrahim (kulia) akijibu maswali yaliyoulizwa na wabunge wa jamii.

 

 

 

UJENZI WA KITUO CHA POLISI KUTELEKEZWA

Bunge hilo likiendelea kunoga mmoja wa wabunge aliibua suala ya kituo kidogo cha polisi eneo hilo kilichotelekezwa wakati kilishaanza kujengwa na kudai ni kazi ngumu kupambana na ukatili wa kijinsia eneo hilo bila nguvu ya polisi.

Hilo lilijibiwa na Waziri wa Wizara Mtambuka, Salma Selemani ambaye alianza na kuwaasa wananchi kuanza kujilinda wenyewe.

Waziri Salma aliwaonya na kuwatolea mfano wa wazazi wanaowavalisha watoto zao mavazi yanayoweza kuwatamanisha wabakaji na kutoa ushauri jamii kujiepusha na mazingira ya kutamanisha wahalifu.

Hata hivyo hilo lilichukuliwa na viongozi wa serikali ya mtaa ambapo walisema kituo hicho kilikuwa kikijengwa kwa nguvu ya wananchi hivyo baada ya bunge hilo kuliibua suala hilo wanaanza kuhamasisha tena ujenzi huo ili wakimalizie kabisa na kianze kutumika.

Waziri wa kilimo kwenye bunge hilo, Jesca Athanas, akijibu maswali ya wabunge.

 

 

 

SHULE KUKOSA VYUMBA VYA KUBADILISHIA TAULO ZA KIKE

Mmoja wa wabunge wa jamii aliibua changamoto ya shule kwenye kata hiyo kukosa vyumba vya kubadilishia taulo za kike pamoja na kuzihifadhi lakini hilo lilijibiwa Waziri wa Elimu wa Bunge hilo, Prisca Domonic aliyeanza kuweka wazi bajeti ya serikali iliyopagwa kwa ajili ya elimu ambapo Mwenyekiti wa Mtaa wa Kerezange, Ismail Ibrahimu alifafanua zaidi kuwa si shule zote kwenye kata hiyo zenye ukosefu wa vyumba hivyo na kusema baadhi ya shule tayari zina vyumba hivyo.

 

WANANCHI KUTEGEMEA MAJI YA VISIMA VYA WATU BINAFSI

Kero nyingine iliyoibuliwa kama changamoto kwenye kata hiyo pale mmoja wa wabunge alipoibua kero ya wanavyoishi kuishi miaka yote kwa kutegemea maji ya visima vinavyochimbwa na watu binafsi ambavyo vingi si salama na wananchi wanatozwa bei kubwa ambayo wanashindwa kuimudu.

Hoja hiyo ilijibiwa na Waziri wa Maji kwenye bunge hilo, Mariam Ng’ariba ambaye aliwachambulia wabunge hao bajeti ya miradi ya maji inavyoonesha kuelekea kutatua changamoto ya maji kwenye eneo hilo.

Hoja hiyo ilishibishwa na Mwenyekiti wa Mtaa wa Kerezange, Ismail Ibrahim ambaye alisema mpaka sasa tayari karibu maeneo yote ya kata hiyo yameshatandazwa mabomba na kuna pampu ya kuvuta maji nayo imeshawekwa na kilichokuwa kikiendelea wakati huo ni majaribio ya pampu hiyo.

Pamoja na hayo katika bunge hilo mambo mbalimbali yaliibuliwa na viongozi wa mitaa waliyapokea na kuahidi kuyafanyika kazi.

 

SHUKRANI KWA TGNP

Baada ya bunge hilo kuahirishwa mmoja wa wananchi aliyeshiriki bunge hilo alisema anaishukuru sana TGNP kwa kuunda vikundi hivyo ambapo amesema anaamini vitasaidia sana kuleta maendeleo na kuwaamsha vingozi waliolala kwenye mitaa yao.                                                                       HABARI/PICHA NA RICHARD BUKOS /GPL   

Leave A Reply