The House of Favourite Newspapers

Kila kitu cha Samatta ni rekodi

0

IMG_3803Mshambuliaji Mbwana Samata.

Na Mwadishi Wetu
MBWANA Samatta ni Mtanzania wa kwanza kutwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika kwa wale wanaocheza soka ndani ya bara hili.

Samatta ambaye anakitumikia kikosi cha TP Mazembe, lakini akiwa njiani kujiunga na Genk ya nchini Ubelgiji ameweka historia ambayo haiwezi kusahaulika hapa nchini.

Mshambuliaji huyo alianza kufahamika wakati akiwa na timu ya Mbagala Market ambayo iliuzwa na kuitwa African Lyon.

Aliondoka kwenye timu hiyo na kujiunga na Simba huku akiwindwa na timu nyingi ikiwemo Yanga, akiwa Simba mshambuliaji huyo alifanya kazi yake ipasavyo.

Mafanikio yake makubwa aliyapata kwenye mchezo wa Klabu Bingwa Afrika baada ya Simba kukutana na TP Mazembe, ambapo Simba waliondolewa lakini kijana huyo akaonyesha kiwango cha hali ya juu ambacho kiliwavutia Wacongo hao na kuhitaji huduma yake.

Samatta-Waziri-Mkuu-15Championi: Ilikuwaje siku ya kwanza ulipopata taarifa kwamba TP Mazembe wanakuhitaji?

Samatta: Nakumbuka siku hiyo nilikuwa nyumbani, ilikuwa baada ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, sisi tulikuwa tumetolewa na hao TP Mazembe.

Championi: Taarifa ilikufikiaje?
Samatta: Alinipigia simu Rage (Ismail Aden, Mwenyekiti wa Simba wakati huo). Nilipopokea akaniambia kwamba TP Mazembe walikuwa wananitaka, alitaka kujua kama niko tayari.

Championi: Vipi ulimjibuje, ujifikirie kwanza?
Samatta: Hapana, kwanza nilijiamini hadi nikashangaa, nilimwambia wao wamalizane nao halafu baadaye wataniambia, akasema sawa atanipa taarifa.

Championi: Kutoka Simba kwenda TP Mazembe hakiwezi kuwa kitu kidogo. Hukuingiwa hofu hata kidogo?
Samatta: Nilianza kuona kama mbele kuna kiza, niliona ni jambo jipya, nikaanza kujiuliza maswali kadhaa. Usiku kidogo usingizi ulikata lakini nilijipa moyo ninaweza.
Hayo yalikuwa mahojiano ya Championi na Samatta akielezea safari yake ilivyoanza.

Kuanzia hapo Samatta akiwa na Mtanzania mwenzake, Thomas Ulimwengu, wamekuwa na mafanikio makubwa, moja ya mafanikio hayo ni kitendo chao cha kutwaa ubingwa wa Klabu Bingwa Afrika, huku yeye akiibuka mfungaji bora kwenye michuano hiyo.

Lakini kali kuliko zote ni kutwaa tuzo hiyo mbele ya Robert Kidiaba na Baghdad Bounedjah, kila kitu kwake ni historia hapa nchini, kutwaa ubingwa wa Klabu Bingwa, kutwaa tuzo hii na hata mapokezi yake.

Championi limekuletea toleo maalum la mwanasoka huyo mzaliwa wa Mbagala, kuna mengi ingia ndani ujisomee.

Leave A Reply