Kila mtu anauelewa wake, usiige wenzako

uelewaNa Richard Manyota
Kuna wakati fulani mwanafunzi hujikuta akiingia katika mkumbo wa kuishi kama wanafunzi wenzake, ikiwemo kufuata hata ratiba ya kujisomea kwao huku akiamini kuwa kwa kufanya hivyo na yeye anaweza akafaulu kwa viwango sawa na wale anaowaiga.
Hali hii hutokea sana kwa wanafunzi ambao huwa na ufaulu mdogo darasani, hasa baada ya kujaribu mbinu kadhaa za kuwawezesha kufaulu na kujikuta wakishindwa kufanya hivyo na kuona kuwa njia pekee ni kuiga usomaji wa wale wanaoamini wana akili darasani.
Bahati huwadondokea wale ambao huwaiga wanafunzi wanaojisomea kwa bidii ambapo kwa kuwaiga hawa hujikuta na wao wakifaulu lakini kwa upande mwingine wanafunzi wengi hujikuta wakifeli kwa kuwaiga wanafunzi ambao hawajisomei mara kwa mara lakini hufaulu vizuri aidha sawa au kumzidi yule anayejisomea kila mara.
Kisayansi kila mmoja ana njia zake za kupokea mambo na kuelewa, wapo wengine ambao huelewa mara moja pindi wanapofundishwa darasani au kusoma kitu kwa mara ya kwanza huku kumbukumbu zao zikiwa vyema bila kuhitaji kujikumbusha kwa kujisomea mara kwa mara.
Wakati huohuo, kuna kundi la wanafunzi wengine ambao uelewa wao huwa ni wa wastani kwa kuingiza mambo kiasi huku kwa kujisomea mara kwa mara kumbukumbu zao huwa thabiti na kuweza kufaulu vizuri.
Kundi la mwisho ni wale wanaoelewa taratibu ambao hawa hupaswa kujifunza mara kwa mara kwa walimu tofauti huku wakijisomea kwa bidii ili kufaulu masomo yao.
Hivyo basi kabla ya kuiga namna mwanafunzi mwenzako anavyojisomea ni vyema kujitambua upo kundi gani kati ya hayo niliyoyaandika hapo juu.
Kwa kupitia makundi hayo, utagundua fika kuwa kwa namna yoyote ile kama mwanafunzi ataiga usomaji wa mwanafunzi mwingine basi atajikuta akishindwa kufaulu vizuri masomo yake kwa kuwa mbali na uelewa tofauti wa makundi hayo pia kila mmoja ana usomaji wake na malengo yake katika maisha anayojichagulia.
Kwa maana hiyo mwanafunzi makini ambaye anataka kufaulu anatakiwa ajifunze kwa bidii bila kujali uwezo wake darasani upoje kwa kuwa mara nyingi hata wale waliokuwa wakifaulu hufeli mitihani yao kwa sababu mbalimbali ikiwemo presha ya mtihani ambayo humfanya asahau kila kitu alichokisoma hapo kabla.


Loading...

Toa comment