The House of Favourite Newspapers

Kilichojificha Kwenye Mgogoro wa Zanzibar

1

Na Elvan Stambuli

Baada ya kueleza kwa urefu jinsi Mwalimu Julius Nyerere alivyokosana na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi, wasomaji wengi wameniomba niwaandikie historia fupi juu ya mgogoro wa kisiasa Zanzibar nikianzia na Mapinduzi ya Zanzibar, kwa faida ya wengi nimejitahidi kuandika nikiamini wengi watapata elimu.

Sasa ifuatayo ni makala kwa ufupi nikianzia na kipindi cha Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964 yaliyoipindua serikali ya ubia ya chama cha Zanzibar Nationalist (ZNP) (maarufu Hizbu) na kile cha Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP), naamini wengi wa kizazi hiki hili hawalijui.
Ngoja tuangazie nini hasa kilitokea usiku wa Jumamosi Januari 11, 1964 yaliyojiri siku ya pili yake na mwezi mzima wa Januari, mwaka huo.

Nimekusanya simulizi hizi baada ya kuzungumza na walioshuhudia Mapinduzi hayo akiwemo aliyekuwa rafiki yangu, Sheikh Yahya Hussein ambaye siku hiyo ya Mapinduzi alikuwa Zanzibar.
Serikali iliyopinduliwa ilikuwa ni ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Sheikh Muhammed Shamte Hamadi tofauti na inavyoelezwa sasa kuwa alikuwa Mwaarabu mwenye ‘nywele za kuteleza.’ (angalia picha yake juu).

Usiku wa manane wa Januari 11, 1964 makada wapatao 200 wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Afro-Shirazi (Afro-Shirazi Party Youth League) walielekea kwenye Kituo cha Polisi cha Ziwani, nje kidogo ya mji kisiwani Unguja, wakiongozwa na Yusuf Himid, wanamapinduzi hao hawakukabiliwa na upinzani walipofika kituoni hapo.
Isipokuwa walikuta ghala la silaha likiwa wazi na wakazinyakua silaha na kukimbia nazo hadi kwenye uwanja ulio nje ya jengo la Raha Leo.

Hapo ndipo palipokuwa makao makuu ya Mapinduzi kwa siku chache na ndipo wanamapinduzi walikokuwa wakipewa silaha.
Studio za Redio ya Serikali pia zilikuwa hapo.
Moja ya sababu zilizoyafanya Mapinduzi yafanikiwe haraka ni uamuzi wa viongozi wa Serikali iliyopinduliwa wakiongozwa na Sheikh Muhammed Shamte kuwataka wafuasi wake wasitumie nguvu kuyapinga kwa kuhofiwa umwagaji mkubwa wa damu.
Hivyo, mbali na mapigano yaliyozuka saa za asubuhi ya Jumapili Januari 12, 1964 mbele ya Kituo cha Polisi Malindi, hapakuzuka mapigano Unguja baada ya hapo kati ya waliopindua na waliopinduliwa.

Pemba nako pia hakukuwa na upinzani ijapokuwa kisiwa hicho kilikuwa ngome ya vyama vya ZNP na ZPPP vilivyokuwa vikitawala.
Itaendelea wiki ijayo.

1 Comment
  1. aristides omary says

    mwandishi muongo mapinduzi ya Zanzibar yaliongozwa field Marshal okello wala si himmid

Leave A Reply