The House of Favourite Newspapers

KILICHOTOKEA MAHAFALI MTOTO WA MASOGANGE

Marehemu Agnes Gerald Waya ‘Masogange’.

INASIKITISHA sana! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya hivi karibuni simanzi kubwa kutawala katika mahafali ya mtoto wa aliyekuwa video queen maarufu Bongo, marehemu Agnes Gerald Waya ‘Masogange’ anayejulikana kwa jina la Sania Sabri, Risasi Mchanganyiko linakupa habari kamili.

 

Mahafali ya mtoto huyo yalifanyika wikiendi iliyopita katika Shule ya Msingi ya Kisutu jijini Dar ambapo Sania alihitimu darasa la saba, lakini badala ya sherehe hiyo kutawaliwa na furaha iligeuka kuwa ya majonzi makubwa.

 

Akizungumza na gazeti hili, mmoja wa wageni waalikwa ambaye hakutaka jina lake kutajwa alieleza kwamba, licha ya baba wa Sania aitwaye Sabri kujitahidi kumnunulia keki, vinywaji na zawadi mbalimbali, lakini muda mwingi alikuwa akilia na kusababisha hata baba yake naye kuangua kilio.

“Unajua mtoto wa Masogange amehitimu darasa la saba na sherehe ya mahafali ilifanyika Jumamosi iliyopita, yaani mtoto alilia sana baada ya kumkumbuka mama yake (Masogange) na kusababisha baadhi ya watu waliokuwa wakimpongeza kujikuta wakiangua vilio,” alisema mwalikwa huyo.

 

BABA AELEZA KWA UCHUNGU

Akizungumza na Risasi Mchanganyiko, baba wa Sania, Sabri alisema kuwa, yeye kama mzazi alimfanyia mwanaye mahafali na kumnunulia zawadi mbalimbali anazozipenda ikiwemo keki, lakini mwanaye huyo alishindwa kuvumilia baada ya kumkumbuka mama yake na kuanza kuangua kilio.

“Mwanangu alilia sana kwenye mahafali na kusababisha kila mtu kulia mpaka mimi mwenyewe nilishindwa kujizuia nikajikuta nalia, ukweli sherehe ilibadilika na kuwa kama msiba maana vilio vilitawala,” alisema Sabri.

 

KWA NINI?

Aliendelea kueleza kuwa, siri ya mwanaye kulia kiasi hicho ni kwamba enzi za uhai wa mama yake, Masogange, licha ya kwamba alikuwa akimlea yeye, lakini mtoto huyo alikuwa akienda kwa Masogange na kukaa wakati wa likizo au siku za mwisho wa wiki.

“Unajua ni kipindi kifupi sana kimepita tangu mama yake afariki dunia hivyo bado hajamtoka machoni maana Sania alimzoea na kumpenda sana mama yake kwani licha ya kwamba alikuwa haishi naye, alikuwa anamchukua anampa zawadi mbalimbali kama mama na mengine mengi.

“Sasa alipomkumbuka tu, palepale alianza kulia, nikawa na kazi nzito ya kumtuliza ambapo nami niliishia kulia, ninamshukuru Mungu tulifanikiwa kumaliza salama japo kwa majonzi,” alisema Sabri.

 

TUJIKUMBUSHE

Masogange aliyekuwa akitikisa kwenye mitandao ya kijamii kutokana na umbo lake matata alifariki dunia Aprili 20, mwaka huu katika Hospitali ya Mama Ngoma, Mwenge jijini Dar alikolazwa kwa siku nne akisumbuliwa na ugonjwa wa Pneumonia (Nimonia).

Mwili wake ulipumzishwa kijijini kwao Utengule jijini Mbeya baada ya kuagwa katika Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni jijini Dar. Mrembo huyo aliyeonekana kwenye video za wasanii wa Bongo Fleva kama Masogange ya Belle 9, Msambinungwa ya Tundaman na nyinginezo ameacha mtoto huyo mmoja pekee.

STORI: Gladness Mallya, Risasi Mchanganyiko

Comments are closed.