The House of Favourite Newspapers

Kimewaka! Ufisadi Bil. 300 Wamkumba Mchumba Ben Pol

HABARI kubwa nchini Kenya ni juu ya familia ya wakwe wa staa wa Muziki wa RnB Bongo, Benard Paul ‘Ben Pol’ kukumbwa na ufisadi mzito ambapo sasa kimewaka ile mbaya, Risasi Mchanganyiko limedokezwa.

 

Ben Pol amemchumbia binti mwenye ukwasi mkubwa nchini Kenya, Anerlisa Muigai Keroche ambaye wiki iliyopita, wazazi wake, Joseph Karanja na Tabitha Karanja walikamatwa kisha kufikishwa mahakamani kabla ya kuachiwa kwa dhamana.

 

UKWEPAJI KODI BIL. 300

Wazazi wa Anerlisa (pichani) wanakabiliwa na tuhuma nzito ya ukwepaji wa kodi kiasi cha shilingi bilioni 14.4 za Kenya (zaidi ya shilingi bilioni 300 za Tanzania.)

 

MAKOSA 10

Sakata hilo lilianza baada ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali ya Kenya (DPP), Noordin Haji kuamuru wakurugenzi wa Kiwanda cha Bia cha Keroche Breweries Ltd kukamatwa na kufunguliwa mashtaka hayo ya ufisadi. Wakurugenzi wa kiwanda hicho ni Tabitha na mumewe Joseph. Katika taarifa yake ya Agosti 21, mwaka huu, DPP Noordin Haji alisema uchunguzi ulibaini kuwa wawili hao wamejihusisha na makosa 10 ya udanganyifu wa kodi.

 

UCHUNGUZI NA UKAGUZI

Noordin Haji alisema kuwa, Agosti 18, mwaka huu, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato ya Kenya (KRA), aliwasilisha kwake faili la uchunguzi na ukaguzi uliofanywa na KRA ambao ulijiridhisha kwamba Kampuni ya Keroche Breweries imekwepa malipo ya ushuru wa jumla ya shilingi 14,451,836,375 za Kenya.

 

Famili hiyo inatuhumiwa kutolipa malipo ya mihuri VAT ya shilingi bilioni 12.34 za Kenya, kutolipa kodi ya moja ya vinywaji vyao cha Crescent Vodka shilingi milioni 135.4 za Kenya pamoja na bidhaa zingine.

KUKWEPA USHURU BIL. 2

Kampuni hiyo pia inatuhumiwa kukwepa malipo ya ushuru wa forodha wa jumla ya shilingi bilioni 2 za Kenya kwa vitu hivyohivyo.

 

DPP alisema kuwa ameridhika kwamba kuna ushahidi wa kutosha kushtaki watuhumiwa hao kwa makosa 10 ya udanganyifu wa kodi kinyume na Sheria ya Taratibu za Kodi ya Mwaka 2015. Kufuatia kujiridhisha huko, DPP aliamuru wakurugenzi hao kufikishwa mahakamani jambo ambalo linaelezwa kumtesa mno Anerlisa.

 

ANERLISA AMWANGUKIA KENYATTA

Baada ya kesi hiyo kufikishwa mahakamani mwishoni mwa wiki iliyopita, Anerlisa alimwangukia Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta akimuomba kuingilia kati sakata hilo. Katika maelezo yake, Anerlisa ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Maji ya Nero, alimsihi Uhuru kuwalinda wafanyabiashara wa ndani ya nchi. “Ninaandika waraka huu kufikisha kilio cha wajasiriamali wetu wa hapa nchini.

“Ninakuomba, kwa unyenyekevu mkubwa kuingilia kati, kutusaidia na kutulinda sisi sote katika biashara. Tulikuchagua wewe kama Rais wetu,” alisema Anerlisa ambaye alichumbiwa na Ben Pol mwezi Aprili, mwaka huu. “Kila siku wajasiriamali wetu wa ndani wanadhulumiwa. Tunatumai na kuamini kwamba utafanya jambo fulani. Asante. Nunua Kenya, Uijenge Kenya.”

 

WALIVYOKAMATWA

Wazazi hao wa Anerlisa walikamatwa Alhamisi ya wiki iliyopita katika kiwanda chao huko Naivasha, Nairobi. Maofisa wa KRA na wapelelezi wa Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jina (DCI) walikuwa wamepiga kambi katika majengo hayo kwa muda kufuatia agizo la kukamatwa kwao.

 

WAACHIWA KWA DHAMANA

Baada ya kukamatwa, wawili hao walielekezwa kwenda makao makuu ya DCI kwenye Barabara ya Kiambu kisha siku iliyofuata walifikishwa mahakamani na kuachiwa kwa dhamana ambapo kesi hiyo iliahirishwa hadi Septemba 2, mwaka huu itakapoanza kusikilizwa rasmi.

BEN POL NA ANERLISA

Mwaka jana, Anerlisa aliandaa shoo ya kuwapongeza watu wanaosapoti biashara yake ya maji ambapo mtumbuizaji alikuwa ni Ben Pol. Ilisemekana kuwa, baada ya shoo alimuomba Ben Pol wakatoe misaada kwenye kituo cha watoto yatima. Baada ya hapo ndipo mrembo huyo akatangaza kwa rafiki zake kuwa ni mchumba rasmi wa Ben Pol.

 

Katika Sherehe za Krismasi zilizopita, wawili hao walikwenda kujiachia kwenye mgahawa maarufu wa bei mbaya huko Dubai, Falme za Kiarabu. Mwezi Aprili, mwaka huu, Ben Pol alimvisha Anerlisa pete ya uchumba tayari kwa ndoa.

 

Jumamosi ya Juni 22, mwaka huu, wawili hao walianza kwa kufunga ndoa ya kimila ambayo sasa itafuatiwa na ndoa nyingine kubwa ya kukata na shoka. Ndoa hiyo ya kimila ilifungwa eneo maarufu linalotembelewa na watu wenye pesa zao la Runda Estate lililopo jijini Nairobi, Kenya.

Comments are closed.