The House of Favourite Newspapers

Kiongozi Ahama Kijiji kwa SMS za Kifo!

kiongozi-wa-kijijiRichard Bukos na Issa Mnally, Gazeti la Uwazi, Toleo la Desemba 27, 2016.

PWANI: Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Kijiji cha Nyambunda kilichopo Mkuranga mkoani hapa, Shaban Shija hivi karibuni alikutwa na Uwazi akiwa amejificha ugenini kwenye kijiji ambacho jina linahifadhiwa na kuacha mali zake ikiwemo nyumba, mifugo na mashamba kwa hofu ya kuuawa na watu wanaomtishia maisha kila kukicha, Uwazi lilizungumza naye.

Akizungumza na Uwazi akiwa mafichoni, mjumbe huyo alisema amefikia hatua ya kukihama kijiji hicho yeye na familia yake baada ya Afisa Mtendaji, Ally Omar na Mwenyekiti wa Kitongoji, Mohammed Thabit kuuawa hivi karibuni kwa kupigwa risasi kwa nyakati tofauti na watu wanaodhaniwa ni magaidi.

Shija alisema amekuwa akitishiwa uhai wake na watu hao ambao wamekuwa wakimtumia ujumbe mfupi wa simu (SMS) na kabla ya kukihama kijiji hicho, kuna watu walikwenda kumgongea dirishani nyumbani kwake na kumweleza dhamira yao ya kukatisha uhai wake.

Mpaka muda huo kiongozi huyo alikuwa hajaripoti tukio hilo polisi na kusema kuwa, alichoona cha muhimu ni kukimbia kijijini hapo ili kusalimisha uhai wake.

“Bado sijaenda kuripoti polisi kwa kuwa nahofia hata njiani wanaweza kunivizia wakati nakwenda huko polisi, yaani inanitia hofu sana. Chamsingi nilichokiona ni kutoroka kimyakimya na si kwenda kutoa ripoti polisi halafu urudi kuishi palepale kijijini. Utakuwa umejipalia makaa zaidi,” alisema Shija.

Kuuawa kwa Amir na Mohammed hivi karibuni kuliandikwa na gazeti hili katika toleo lake la Desemba 18, mwaka huu ambalo lilifuatilia kwa kina habari hiyo ikiwa na kichwa cha habari; BADO ROHO TISA.

Ilikuwa bado roho tisa, baada ya kundi hilo tangu mwanzoni mwa mwaka huu, kuahidi kuua viongozi kumi na nane wa vijiji mbalimbali vya Wilaya ya Mkuranga kwa madai kuwa, waliwachoma kwa polisi na kukamatwa kwa madai ya uhalifu na mauaji ya Askari wa Kituo cha Polisi cha Kimanzichana, Joseph Ngonyani, Juni 2014.

Tangu kundi hilo kutangaza nia yao hiyo, walianza kuua viongozi mmoja mmoja kila wakati mpaka kufikia tisa na kubaki tisa. Staili yao ya kuua ni kutumia bunduki huku wauaji hao wakiwa kwenye bodaboda na wamevaa kininja.

DIAMOND PLATINUM ALIVYOWASILI KWA BOTI KWENYE SHOW YA WASAFI BEACH PART

Comments are closed.