The House of Favourite Newspapers

Kisa Joash Onyango… Ouattara Aomba Kuondoka Simba Katika Usajili wa Dirisha Dogo

0
Beki wa Simba raia wa Ivory Coast, Mohamed Ouattara.

 

IMEFAHAMIKA kuwa, beki wa Simba raia wa Ivory Coast, Mohamed Ouattara, ameushinikiza uongozi wa timu hiyo, uvunje mkataba wake ili aende akaanze maisha mapya sehemu nyingine, baada ya kukosa nafasi ya kucheza mbele ya Joash Onyango.

 

Nyota huyo ni kati ya wachezaji wapya waliosajiliwa na Simba msimu huu akitokea Al Hilal ya Sudan, akisaini mkataba wa miaka miwili.

 

Ouattara wakati Simba ikiwa chini ya Kocha Mserbia, Zoran Maki, alikuwa akipata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza, huku Joash Onyango akisotea benchi.

 

Lakini tangu Juma Mgunda apewe kikosi cha Simba, Onyango anacheza, huku Ouattara akiishia nje.

 

Mmoja wa mabosi kutoka ndani ya Simba, ameliambia Spoti Xtra kuwa, beki huyo ameomba mkataba wake uvunjwe ili katika usajili wa dirisha dogo aondoke.

 

Bosi huyo alisema sababu ya Ouattara kuomba kuondoka ni baada ya kukosa nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

 

Aliongeza kuwa, bado uongozi haujafikia muafaka wowote juu ya maombi hayo.

 

“Ouattara ni ngumu kuendelea kubaki Simba, kwani tayari amekata tamaa, hivyo upo uwezekano mkubwa wa kuondoka dirisha dogo.

 

“Tayari ameuomba uongozi avunje mkataba wake na kwenda kwingine kutafuta changamoto mpya baada ya kupoteza nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza.

 

“Kikubwa anataka kucheza kikosi cha kwanza, kwani akiendelea kukaa benchi kiwango chake kitapungua, hivyo hataki hiyo itokee,” alisema bosi huyo.

 

Alipotafutwa Meneja wa Habari wa Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, kuzungumzia hilo, simu yake iliita bila kupokelewa.

WILBERT MOLANDI NA MUSA MATEJA

NABI ALIA NA MUDA, BEKI AOMBA KUONDOKA SIMBA|SPORTS ZONE

Leave A Reply