The House of Favourite Newspapers

KISA MREMBO… AVUNJWA MKONO NA MWALIMU

LINDI: Mkazi mmoja wa Nyangao, Wilaya ya Lindi, Shawezi Mohamedi, amevunjwa mkono wake wa kulia na mwanaume mwenzake aitwaye Mwalimu Mboka Lwimiko Mwakyelwike katika kile kilichodaiwa kuwa sababu ni ugomvi wa kumgombea mrembo ambaye sasa ni mchumba wake.   

 

Mboka ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Chiwelele, iliyopo Kata ya Nyangao katika Halmashauri ya Wilaya ya Lindi. Imedaiwa kuwa mwanamke aliyekuwa anagombewa anaitwa Stella Anga naye ni mkazi na mkulima wa kata hiyo na ugomvi ulitokea Agosti 25, mwaka huu, saa 10:0 alasiri.

 

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Amani nyumbani kwake Nyangao, Shaweji alidai kuwa Stella ambaye kwa sasa ni mchumba wake, hapo awali alikuwa mpenzi wa Mboka na kufanikiwa kupata mtoto wa kike na baadaye kutengana baada ya kuoa mke mwingine wa kabila lake. ‘‘Kama ujuavyo mwanamke au mwanaume wanapotengana na mwenzake kila mmoja hupata mtu mwingine wa kuishi naye, ndivyo ilivyokuwa mimi na Stella,” alisema Shaweji.

 

Akisimulia mkasa huo, Shaweji alisema mwanzoni mwa mwaka 2016, alikutana na Stella, ambapo walitengeneza uhusiano na kuamua wawe mke na mume hivyo akajitokeza mbele ya wazazi wake na akalipa mahari, hivyo kujiandaa kwa ajili ya maandalizi ya kufunga naye ndoa.‘‘Hivi ninavyozungumza Stella Anga ni mchumba wangu, kwani tayari nimeshamtolea mahari kwa wazazi wake, tunasubiri kufunga ndoa tu,” alisema Shaweji.

 

Shaweji alidai kitendo cha yeye kuwa na uhusiano na Stella kinaonyesha kumkasirisha mgomvi wake na akaanzisha visa dhidi ya Stella ikiwemo kwenda sehemu anazofanyia biashara na kumharibia, kuvunja mlango nyumba wanayoishi, hali iliyosababisha kumfikisha Kituo Kidogo cha Polisi Nyangao kwa hatua zingine za kisheria.

 

Hata hivyo, Shaweji alidai Agosti 25, mwaka huu, Mboka alifika tena eneo la soko analofanyia ujasiriamali mchumba wake Stella na kufanya fujo ikiwa ni pamoja kumwaga mihogo na viazi alivyokuwa anakaanga na kufanikiwa kudhibitiwa na wafanyabiashara waliokuwepo eneo hilo. Shaweji alisema akiwa kwenye majukumu yake ya kujitafutia riziki, wasamaria wema walimpigia simu kumueleza kilichokuwa kikiendelea kwa mchumba wake, na kuamua kufuatilia ili akaelewe kile kilichokuwa kinafanyika.

 

Alidai wakati akiwa njiani kuelekea eneo hilo la sokoni, alimshuhudia Mwalimu Mboka akimkimbiza mtu mmoja aliyekuwa akimdhibiti huku mkono wake wa kulia akiwa ameshikilia kisu na alipomuona yeye (Shaweji) alimuacha mtu huyo na kutaka kumvamia yeye, hivyo alijitetea kwa kuokota kipande cha mti.

 

Shaweji alidai baada ya mgomvi wake kuona ameokota kipande cha mti alimrushia kile kisu na kutua kiganja cha mkono wake wa kulia, baada ya kukidaka na wakati akiugulia maumivu ya kile kisu, Mboka aliitumia nafasi hiyo kumvamia na kumvunja mkono na vidole vyake viwili. Naye Stella alisema yeye na mzazi mwenzake mwalimu Mboka walikuwa wapenzi walioishi pamoja na kufanikiwa kupata mtoto wa kike aitwaye Enjo lakini walitengana baada ya kuelezwa na mwalimu huyo kuwa anaoa mke wa kabila lake kutoka mkoani Mbeya.

 

“Mzazi mwenzangu akiwa chuoni alinipigia simu akinieleza amepata mke mwingine tena kabila lake hivyo, atakaporejea atanirudisha nyumbani kwa wazazi wangu, sikuwa na ubishi,” alidai Stella. Aliendelea kudai kwamba baada ya Mboka kurejea kituo chake cha kazi shuleni Chiwelele, iliyopo Kata ya Nyangao, kweli alimrejesha kwa wazazi wake, na akatoa onyo kwake kwamba hatapenda kuona (Stella) akienda nyumbani kwake kumfanyia fujo pale mke wake atakapofika.

 

Stella alisema anashangaa kuona mzazi mwenzake huyo sasa amekuwa mstari wa mbele kumfanyia fujo baada ya kuona amepata mchumba anayeishi naye kwa raha. Mwalimu Mboka hakupatikana ili kuelezea tukio hilo kwa kuwa alikuwa rumande.

 

Kamanda wa Polisi mkoani Lindi, ACP Pudensiana Protas alipoulizwa na gazeti hili, amekiri ofisi yake kupata taarifa ya tukio hilo, akafafanua: “Tayari mtuhumiwa Mwalimu Mboka Mwakyelwike tumemkamata na tunamhoji kuhusiana na ugomvi huo na atafikishwa mahakamani mara taratibu za ofisi zitakapokamilika.”

Stori: Said Hauni, Amani

Comments are closed.