The House of Favourite Newspapers

Kisa Simba, Ngoma afungiwa… chumbani

0

DONALD-NGOMA

Straika wa Yanga, Donald Ngoma.

Sweetbert Lukonge, Dar es Salaam
YANGA ipo ‘on fire’, Simba nayo ipo on fire, yaani zote zipo moto kutokana na kupata ushindi mfululizo, hali hiyo imeongeza presha kuelekea mchezo ujao baina ya timu hizo ambao utafanyika Septemba 26, mwaka huu.

Baada ya kuona presha inazidi kuwa kubwa, straika wa Yanga, Donald Ngoma ambaye amejiunga na klabu hiyo hivi karibuni akitokea FC Platinum ya Zimbabwe, juzi jioni alifungiwa chumbani kwake na kupewa somo kali kubwa kuhusiana na wapinzani wao.

Timu hizo zinatarajiwa kukutana katika mchezo wa Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ambapo kutokana na timu zote kushinda mechi mbili za awali, kila upande umeanza kujinadi kuwa upo vizuri na lazima utaibuka na ushindi.

Baada ya kuona tambo zimeanza mapema, Ngoma ambaye mpaka sasa ameshapachika mabao mawili katika michezo miwili ya ligi hiyo, aliamua kuwaita baadhi ya wachezaji wenzake wa Yanga kisha kuwaomba wamsimulie juu ya upinzani wa Simba na Yanga.

Mmoja wa wachezaji hao aliliambia gazeti hili kuwa, walimueleza kila kitu alichohitaji kujua ikiwa ni pamoja na rekodi ya miaka ya hivi karibuni ya mabao 5-0 ambayo Yanga ilifungwa na Simba msimu wa 2011/12.

“Jana jioni (juzi), baada ya mechi yetu ya Prisons, tulikuwa na Ngoma chumbani, alituita mimi na (Amissi) Tambwe akitaka tumsimulie jinsi mechi yetu ya Simba inavyokuwa kwani huwa anasikia mambo mengi.

“Hata hivyo bila ya kumficha tulimwambia kila kitu ikiwa ni pamoja na lile deni la mabao 5-0 tunalodaiwa na timu hiyo,” alisema mchezaji huyo.

Championi Ijumaa lilipozungumza na Ngoma juu ya taarifa hizo, alikuwa na haya ya kusema: “Ni kweli niliwaita na kuwauliza, kwani nilitaka kuijua vizuri Simba kabla ya kukutana nayo, hata hivyo nipo vizuri kwa mechi hiyo na nina imani tutaendeleza rekodi yetu ya ushindi tuliyoanza nayo.”

Tangu kuanza kwa ligi kuu ya msimu huu, Yanga imeshinda mechi mbili dhidi ya Coastal Union (2-0) na dhidi ya Prisons (3-0) wakati Simba ilizifunga African Sports (1-0) kisha Mgambo (2-0).

Leave A Reply