The House of Favourite Newspapers

KISHINDO NDOA YA BEN POL

DAR ES SALAAM: Ni kishindo! Kama alivyoahidi mrembo bilionea wa Kenya, Anerlisa Joseph Karanja Muigai kuwa ndoa yake na staa wa Bongo Fleva, Benard Michael Paul Mnyang’anga ‘Ben Pol’ itakuwa ni funiko bovu, mambo yameanza, Risasi Mchanganyiko lina ishu. 

 

Katika mahojiano na vyombo mbalimbali vya habari nchini Kenya, Anerlisa aliweka wazi mipango ya ndoa yao ambapo alisema itakuwa ni ya kishindo kwa Afrika Mashariki. Alisema kuwa litakuwa ni tukio la aina yake kutokana na penzi lao kuwa na wafuatiliaji wengi ukanda huu wa Afrika Mashariki na hasa kwenye mitandao ya kijamii.

 

NDOA YA KIMILA

Tayari mambo yameanza ambapo Jumamosi iliyopita ya Juni 22, mwaka huu, wawili hao walianza kwa kufunga ndoa ya kimila ambayo sasa itafuatiwa na ndoa nyingine kubwa ya kukata na shoka. Ndoa hiyo ya kimila ilifungwa eneo maarufu linalotembelewa na watu wenye pesa zao la Runda Estate lililopo jijini Nairobi, Kenya.

RURACIO NI NINI?

Shughuli hiyo ya kimila maarufu kwa jina la “Ruracio” ilihudhuriwa na watu muhimu wachache kutoka kwenye familia na baadhi ya marafiki wa karibu.

 

Ruracio ni mila ya kabila la Wakikuyu (kabila la Anerlisa) ambapo mwanaume (muoaji) hukaribishwa kwenye familia ya mwanamke (muolewaji) na kufanyiwa matukio mbalimbali ya kimila ikiwemo kulipa mahari kisha kukabidhiwa mke kwa taratibu za kimila.

 

Kwa mujibu wa mitandao ya Kenya, baada ya tukio hilo, sasa kinachofuata ni shughuli kubwa ya harusi ambayo kwa mujibu wa Anerlisa itaacha historia kutokana na ukubwa na utofauti wake.

 

SHEMEJI WA TAIFA

Kufuatia tukio hilo la ndoa ya kimila, Anerlisa alipongezwa na wafuasi wake wa Kibongo kwenye mitandao ya kijamii huku wakimwita shemeji na wifi wa taifa kutokana na kuanza kutimiza ahadi yake ya ndoa na Ben Pol. Hata hivyo, waliishia kwa kuwatakia kila la heri kwenye maisha yao mapya ndoa.

ANERLISA NI NANI?

Anerlisa ni binti wa miaka 31, anayetokea familia ya kitajiri akiwa ni mtoto wa kwanza ambapo mama yake, Tabitha Karanja anamiliki kiwanda kikubwa cha kutengeneza bia kiitwacho Keroche Breweries kinachosambaza vinywaji vyake sehemu kubwa ya nchini Kenya.

 

Baada ya kufanya kazi na mama yake kwenye kiwanda hicho cha bia, mwaka 2013, Anerlisa aliamua kufanya biashara ya kujitegemea kwa kuanzisha kampuni yake mwenyewe aliyoiita NERO inayojihusisha na kutengeneza maji ya kunywa yanayosambazwa sehemu kubwa ya nchini Kenya.

 

Kampuni hiyo ya NERO imempatia Anerlisa utajiri mkubwa alionao sasa. Kwa mujibu wa Jarida la Forbes lililotoka mwaka jana, Anerlisa ni miongoni mwa vijana 30 wanaokuja kwa kasi katika ujasiriamali Afrika na wanaotegemewa kuwa matajiri wakubwa.

 

Pia Jarida la Business Elites Africa linamtaja Anerlisa kuwa miongoni mwa matajiri Afrika wenye umri chini ya miaka 40 wanaokuja juu kwa kasi ya ajabu.

 

Anerlisa anamiliki jumba la kifahari pande za Nairobi, magari kama yote yakiwemo Range Rover Evogue, Range Rover Velar na Jeep. Pia anamiliki vitu vya kifahari kama viatu aina ya Manolo Blahnik zaidi ya pea 100 vyenye thamani ya shilingi milioni mbili kwa pea moja.

WALIKUTANAJE?

Mwaka jana Anerlisa aliandaa shoo ya kuwapongeza watu wanaosapoti biashara yake ya maji ambapo mtumbuizaji alikuwa ni Ben Pol. Ilisemekana kuwa, baada ya shoo alimuomba Ben Pol wakatoe misaada kwenye kituo cha watoto yatima. Baada ya hapo ndipo mrembo huyo akatangaza kwa rafiki zake kuwa mchumba rasmi wa Ben Pol.

 

Katika Sherehe za Krismasi za mwaka uliopita, wawili hao walikwenda kujiachia kwenye mgahawa maarufu wa bei mbaya huko Dubai, Falme za Kiarabu. Mwezi Aprili, mwaka huu, Ben Pol alimvisha Anerlisa pete ya uchumba tayari kwa ndoa.

 

REKODI YA WABONGO KENYA

Ben Pol anakuwa miongoni mwa wasanii kadhaa kutoka kwenye Bongo Fleva ambao wamepata wanawake kutoka nchini Kenya.

Kwenye orodha hiyo yupo Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’ ambaye amemuoa Amina Khaleef kutoka Mombasa na Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ anayeminya na mtangazaji Tanasha Donna Oketch, naye kutoka Mombasa nchini Kenya.

Comments are closed.