The House of Favourite Newspapers

Kocha Mkuu wa Simba Awatega Musonda, Mayele Atoa Maagizo

0

KOCHA Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ametoa angalizo kubwa kwa mabeki wa timu hiyo kwa kuhakikisha wanaongeza umakini mkubwa katika safu ya ulinzi kuhakikisha washambuliaji wa Yanga, Kennedy Musonda na Fiston Mayele hawaleti madhara katika mchezo wao wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa Aprili 16, mwaka huu kutokana ubora walionao kwa sasa.

Fiston Mayele

Robertinho ametoa kauli wakati Simba ikiwa inatarajia kucheza mchezo wa robo fainali ya Kombe la FA dhidi ya Ihefu mchezo uliopangwa kupigwa Aprili 7, mwaka huu kabla ya kuwavaa Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Bara ambao unatarajia kupigwa April 16, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar.

Akizungumza na Championi Jumamosi, Robertinho amefunguka kuwa kwa sasa Yanga wana safu bora ya ushambuliaji inayoongozwa na washambuliaji wake Musonda na Mayele hali inayompelekea kuwataka mabeki wake kuongeza umakini kuelekea katika mchezo wao wa dabi.

“Katika kipindi hiki ambacho tunasubiria ratiba ya robo fainali baada ya kukamilisha hatua ya makundi, malengo na mipango yetu imerejea kwenye ligi kwa sababu ndiyo sehemu ambayo tunahitaji kuweka nguvu kubwa ya kuweza kushinda vikombe, tuna mechi mbili ngumu mbele yetu ambazo ushindi kwetu utakuwa jambo muhimu.

“Tunaenda kucheza na Ihefu katika robo fainali ya FA ambao kwa sasa siyo timu kuibeza kutokana na maboresho makubwa waliofanya lakini katika ligi tuna mchezo mwingine mgumu dhidi ya Yanga ambayo kwa sasa imekuwa bora sana kutokana na safu yake ya ushambuliaji kufanya vizuri hasa Mayele na Musonda kitu ambacho mabeki wangu wanatakiwa kuongeza umakini mkubwa ili kupunguza kasi yao katika mchezo muhimu wenye ushindani, ” alisema Robertinho.

Leave A Reply