The House of Favourite Newspapers

Kocha Mpya Simba Kama Mourinho, Okwi, Mavugo na Boko Kicheko

0
Ko­cha wa Rayon Sport, Irambona Masoud Djuma aliyetua Simba akiongea.

MUDA mfupi tangu Jack­son Mayanja, raia wa Uganda aliyekuwa Kocha Msaidizi wa Simba kutan­gaza kujiuzulu nafasi hiyo kutokana na kile kilichoe­lezwa matatizo ya kifa­milia, hatimaye mrithi wa nafasi hiyo ametangazwa.

 

Mrithi huyo ni aliyekuwa Ko­cha wa Rayon Sport, Irambona Masoud Djuma, kocha ambaye anaweza kufananishwa na Ko­cha wa Manchester United, Jose Mourinho kutokana na kuwa na mbwembwe nyingi na maneno mengi.

 

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari katika Makao Makuu ya klabu hiyo ya Simba, Djuma aliweka hadha­rani kuwa amekuja ndani ya kikosi hicho kwa ajili ya kufanya kazi na kukisaidia kufanya vizuri kwenye kila kombe wana­loshiriki.

 

“Nimekuja hapa Simba kwa ajili ya kufanya kazi tu, na na­taka tushirikiane ili timu iweze kusonga mbele itoke hapa ilipo, na pia nipo hapa ili kukuza jina langu maana kiukweli unapo­zungumzia Simba unazun­gumzia juu ya klabu kubwa hapa nchini.

 

“Lakini pia nafahamu juu ya upinzani uliopo kati ya Simba na Yanga na siwezi kutabiri kwamba eti kwenye mechi yao Oktoba 28, nini kitatokea kwa sababu mimi siyo Mungu ila nataka watu wafahamu kwamba kwenye mechi kuna kufunga, kufungwa na sare, hivyo matokeo yoyote wakubaliane nayo.

 

“Unajua kwamba hizi mechi za watani duniani kote presha yake inakuwa ileile siyo Simba na Yanga pekee, hata nilipotoka mimi huko Rwanda kulikuwa na ushindani wa namna hiyo na hata Ulaya kwenyewe inapofika mechi hii basi presha huwa kubwa sana.

 

“Na watu wanajiuliza kwamba kwa nini nimekubali kuwa msaidizi hapa, niwaam­bie kwamba Simba ni sehemu kubwa na naamini uwepo wangu hapa utasaidia kwenye suala zima la kukuza jina langu.

 

“Niwaambie mashabiki kwamba nipo hapa na nina­hitaji tu sapoti yao kwa ajili ya kuifanya Simba isogee zaidi ya ilipo hapa kwa sasa, na mimi nitashirikiana nao kulifanikisha suala hilo,” alisema Djuma am­baye amewahi kufundisha soka kwenye Klabu ya Inter Club na Inter FC.

 

Katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofan­yika kwenye Makao Makuu ya Simba, Msimbazi jijini Dar, kocha huyo alionekana kuchangamka huku akitoa maneno mengi ya utani na hata majibu yake yalikuwa yamechangamka kitendo kilichofanya waandishi wawe wanacheka mara kadhaa.

 

Kocha huyo hadi anaondoka ndani ya klabu yake ya Rayon Sport, tayari alikuwa ameshai­saidia kutwaa ubingwa wa ligi sambamba na Kombe la FA la kwao, ambapo kocha huyo pia ni mtu wa misimamo na asiyependa kuyumbishwa.

Kocha huyo anatarajiwa kusaini mkataba leo Ijumaa.

 

Lakini pia uongozi wa Sim­ba chini ya kaimu rais wake, Salim Abdallah ‘Try Again’, umemteua Richard Robert kuwa meneja wa kikosi hicho akichukua mikoba ya Cosmas Kapinga ambaye aliamua kubwaga manyanga hivi karibuni.

 

Jana jioni kocha huyo aliun­gana na wenzake mazoezini ambapo pia alitambulishwa kwa wachezaji na benchi la ufundi, akapata muda kidogo wa kuzungumza na Omog na kiungo wa timu hiyo, Haruna Niyonzima.

 

Moja ya sifa za kocha huyo ni kuwa alikuwa msham­buliaji, hivyo anaweza kuwa na nafasi nzuri ya kuwapa mbinu washambuliaji Em­manuel Okwi, John Bocco, Shiza Kichuya, Laudit Mavugo na wengineo.

 

Mbali na hapo kuna taarifa kuwa kocha huyo atasaini mkataba wa kuwa msaidizi wakati ambapo anasubiri mkataba wa Omog umalizike baadaye mwaka huu ili apewe nafasi ya kuwa kocha mkuu.

Waandishi: Ibrahim Mussa, Musa Mateja na Said Ally.

Full Video: Lulu (Elizabeth Michael) Akiondoka kwa Masikitiko Mahakama Kuu Leo

Leave A Reply