The House of Favourite Newspapers

Kocha Simba Awafungia Mziki Mzima Al Merrikh

0

KIKOSI cha Simba leo kinatarajiwa kujitupa uwanjani kuvaana na Al Merrikh ya nchini Sudan katika mchezo wa tatu wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Simba inayoongoza kwenye msimamo wa Kundi A, ikiwa na pointi sita, ikishinda michezo yote miwili kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Al Ahly uliochezwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar na ule dhidi ya AS Vita uliopigwa Kinshasa, DR Congo.

 

Mchezo huo wa leo unatarajiwa kuanza kupigwa saa kumi kamili jioni kwenye Uwanja wa Al Hilal uliopo kwenye Jiji la Khartoum, Sudan wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 43,000.

Akizungumza na Championi Jumamosi, Kocha Mkuu wa Simba, Mfaransa Didier Gomes, alisema kuwa maandalizi ya kikosi chake yamekamilika kwa asilimia mia moja huku akifurahia morali ya wachezaji wake waliyonayo.

 

Gomes alisema kuwa anawafahamu vizuri wapinzani wake wakiwemo wachezaji hatari, hivyo atahakikisha anatumia upungufu walionao Merrikh kuhakikisha wanapata ushindi.

 

Aliongeza kuwa katika mchezo huo wataingia uwanjani kwa tahadhari kubwa ya kulinda na kushambulia lango la wapinzani wao ambao watakuwa nyumbani, hivyo ni lazima watumie kila mbinu kupata ushindi.

 

“Hakuna jinsi ni lazima tupate matokeo ya ushindi ugenini, ninafahamu siyo kazi rahisi lakini tutapambana ndani na nje ya uwanja kuhakikisha tunafanikisha malengo yetu.

 

“Kama tuliweza kupata matokeo ugenini Kinshasa, Congo, tulipocheza dhidi ya AS Vita, ninaamini hatutashindwa kupata matokeo mazuri Sudan, tukiwa tupo katika maandalizi itoshe kusema kuwa tunawaheshimu wapinzani wetu Merrikh.“

Ninawajua vizuri Merrikh na mimi nafahamu wanazijua vizuri mbinu zangu kutokana na kuwahi kuifundisha timu hiyo, lakini ubora wa wachezaji niliowakuta hapa Simba unanipa matumaini ya kushinda mchezo huu kutokana na mwendelezo mzuri wa matokeo mazuri ya michezo ya ligi na michuano hii mikubwa Afrika,” alisema Gomes.

 

Naye Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez alisema: “Mazoezi ya vijana wetu waliyoyafanya juzi Jumatano na Alhamisi yalikwenda vizuri hapa Khartoum.

 

Mafundi wetu watakaotuwakilisha kwenye mechi dhidi ya Al-Merrikh wako tayari kupambana kwa asilimia mia moja, hivyo tunaamini tutapata matokeo mazuri.“Kwa upande wa uongozi tumekamilisha maandalizi yote kuelekea mchezo huo tukiwa huku Khartoum na wenzangu akina Hans Pope (Zakaria) na Magori (Crescentius Magori) katika kuhakikisha tunapata matokeo mazuri.

 

“Kipa wetu Manula (Aishi) yupo fiti anaendelea na matibabu akiwa chini ya uangalizi ya madaktari, upo uwezekano mkubwa wa kucheza mchezo huu.”

STORI: WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

Leave A Reply