The House of Favourite Newspapers

Kocha Simba Awazidi Ujanja AS Vita

0

ACHANA na ile ya kila pasi tano bao, sasa hivi Kocha Mkuu wa Simba, Mfaransa Didier Gomes amekuja na kila krosi bao huku akiwatumia mabeki wa pembeni na mawinga katika kutengeneza mabao.

 

Hiyo ni katika kuelekea mchezo wao wa tano wa hatua ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa leo saa kumi kamili kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

 

Katika mchezo uliopita wa awali wa michuano hiyo, Simba ilifanikiwa kupata ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Mkongomani Chris Mugalu kwa njia ya penalti.

Kocha huyo juzi alionekana akiwapa mbinu mbalimbali za uchezaji zitakazompa ushindi katika mchezo huo ambao mashabiki 10,000 wameruhusiwa na Caf kutazama pambano hilo baada ya awali kuwazuia.

 

Katika mazoezi hayo yaliyokuwa yakifanyika kwenye Uwanja wa Simba Mo Arena, Bunju nje ya Jiji la Dar es Salaam alionekana kuwapa program maalum mabeki wa pembeni na mawinga jinsi ya kupiga krosi kwa washambuliaji wake Mugalu na John Bocco kabla ya kufunga.

 

Katika kuelekea pambano hilo, kocha huyo ameonekana kutaka kuingia kwa mbinu nyingine tofauti za kutafuta mabao kwa kutokea pembeni akiwatumia mabeki wa pembeni na mawinga wakati awali alikuwa akitumia katikati kulazimisha kupenya kwenye ng’ome ya safu ya ulinzi ya wapinzani.

Hiyo inamaana kuwa mabeki wa pembeni Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Shomari Kapombe watakuwa wana kazi mbili katika kuelekea mchezo huo wa AS Vita ambazo kulinda goli na kupeleka mashambulizi kwenye goli la timu pinzani.

 

Pia, viungo washambuliaji wanaotokea pembeni Luis Miquissone na Clatous Chama watakuwa wana kibarua cha kutengeneza mabao kwa krosi zitakazowafikia washambuliaji wa timu hiyo.

 

Katika mazoezi ya juzi, kocha alionekana kuwatumia mabeki wa pembeni Gadier Michael na David Kameta kupiga krosi kwa washambuliaji Bocco na Mugalu huku Kapombe na Tshabalala waliopewa mapumziko maalum na kocha wakifuatilia kwa ukaribu mbinu hizo.

STORI: WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

Leave A Reply