The House of Favourite Newspapers

Kocha wa Yanga: Mashabiki Tulieni, Kazi Haijaisha, Tunaenda Kuwashangaza Kwao

0
Kocha mkuu wa Yanga, Nasredine Nabi

NASREDDINE Nabi, Kocha Mkuu wa Yanga, ana kibarua cha kwenda ugenini kusaka ushindi dhidi ya Al Hilal baada ya mchezo wa kwanza kutoshana nguvu kwa kufungana bao 1-1, lakini amewaambia Wanayanga watulie, kwani kazi haijaisha.

 

Jana Jumamosi kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar, kulikuwa na mchezo wa nguvu nyingi na akili kati ya wenyeji Yanga dhidi ya Al Hilal ya Sudan wa Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo dakika 45 za mwanzo zilikamilika kwa timu hizo kushindwa kufungana, huku kipindi cha pili ndipo mabao yakipatikana.

 

Fiston Mayele alianza kuifungia Yanga bao dakika ya 50 akiwa nje ya 18 akitumia pasi ya Khalid Aucho.

 

Bao hilo lilidumu hadi dakika ya 67 baada ya Al Hilal inayonolewa na Kocha Mkuu, Florent Ibenge kusawazisha kupitia Mohamed Youseif.

Mashabiki wa Yanga wakifanya yao Uwanja wa Mkapa.

Yanga ina kibarua kingine cha kwenda kusaka ushindi ugenini ili kutinga hatua ya makundi kwenye mchezo wa marudio unaotarajiwa kuchezwa nchini Sudan Oktoba 16.

 

Kuelekea mchezo wa marudiano, Kocha Nabi amewaambia Wanayanga watulie kwani wanaenda Sudan kuwashangaza wenyeji wao na kufuzu hatua ya makundi.

Katika mchezo wa jana, kiungo wa Yanga, Stephane Aziz Ki ambaye alianza kikosi cha kwanza, alipata nafasi tatu ambazo mashuti yalilenga lango dakika ya 8, 38 na 41.

 

Mayele shuti lake moja ambalo lililenga lango, ndilo lilikuwa bao, huku mengine matatu yakishindwa kulenga lango.

 

Wakati Yanga ikilazimishwa sare ya 1-1, Kipanga nayo ilishindwa kufungana na Club Africain, ukiwa ni mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya kwanza uliochezwa Uwanja wa Amaan, Zanzibar. Timu hizo zitarudiana wikiendi ijayo nchini Tunisia.

STOLI NA ISSA LIPONDA NA KAZIJA THABIT

Leave A Reply