UNAWEZA kusema upepo umebadilika na huenda ndio kilikuwa kitu kilichowashangaza watu wengi baada ya mashabiki wa Morocco kuamua kuishangilia Al Ahly katika mechi yake ya kwanza ya Kombe la Dunia la Klabu.
Mechi hiyo kwenye Uwanja wa Tengue ilihudhuriwa na watu wengi sana. Kwanza ilionekana kama ni kitu cha kushangaza kwa kuwa ni haikuwa ikicheza timu ya hapa Morocco.
Timu sita kutoka mabara yote zinashiriki michuano hiyo na Afrika ina bahati ya kuwakilishwa na timu mbili, Ahly ya Misri iliyoshika nafasi ya tatu msimu uliopita katika michuano hiyo na wenyeji Wydad Casablanca.
Lakini kuna Flamengo kutoka Amerika Kusini, Seatlle Sounders ya Amerika Kaskazini, Al Hilal ya Saudi Arabia kwa Bara la Asia na kutoka Ulaya ni Real Madrid na Auckland City ya New Zealand.
Mechi hiyo ilichezwa kwenye mji ambao uko Kaskazini kabisa mwa bara la Afrika, mji ambao ni maili 12 tu kwenda Hispania kupitia Gilbrata na maarufu sana kutokana na kuwa na moja ya bandari kubwa zaidi barani Afrika.
Mashabiki wengi hawakuweza kumaliza mchezo huo kutokana na baridi kali iliyotawala na kuongezeka ghafla. Baadhi ya mashabiki walitoka mapema kurejea makwao na hasa wale waliokuwa na watoto kwa kuwa walihofia afya zao.
Ndio maana kwa wale waliokuwa wakiangalia kwenye runinga, waliona sehemu kubwa za uwanja huo zilikuwa wazi katika kipindi cha pili.
Kimchezo ilionekana Auckland wamejiandaa lakini taratibu walianza kutoa nafasi za Ahly kutengeneza nafasi nyingi ambazo walishindwa kuzitumia.
Mwishoni mwa kipindi cha kwanza, Ahly walifanikiwa kupata bao na unaona. Muda mwingi mashabiki waliokuwa uwanjani walikuwa wakiwazomea Ahly.
Mashabiki wa Ahly hawakuwa wengi sana uwanjani lakini kama ilivyo ada ya Ultras walijitahidi kuonyesha juhudi kubwa za kushangilia.
Kadiri inavyokwenda, mashabiki waliokuwa wanaizomea Ahly walianza kupungua taratibu na kuanza kuishangilia. Jambo ambalo wazi lilionekana kuwaongezea nguvu wababe hao wa Misri na Afrika.
Kulikuwa na mjadala miongoni mwa mashabiki na wengi hawakukubaliana na suala la kuzomewa lakini wengi waliamini si timu ya Morocco na mpinzani mkubwa wa Wydad.
Hata hivyo, damu ni nzito kuliko maji na baada ya Ahly kupata bao la pili na wachezaji wake kuendelea kuonyesha kuwakubali mashabiki wa Morocco licha ya awali kuwazomea, mashabiki nao wakaanza kuwaunga mkono.
Ilikuwa ni sherehe hasa na hii ikawa nguvu zaidi Ahly ambao walipata bao la tatu kutoka kwa Msauz, Perci Tau aliyeingia dakika za jioni.
Utamu umeanza kuwa juu katika Kombe la Dunia ambalo limeandaliwa vizuri sana na wenyeji Morocco ambao waliwahi kuandaa mashindano haya makubwa kwa klabu mara mbili na wakayatendea haki.
Maandalizi yako vizuri kwenye kila kitu, kuanzia sehemu za kuishi timu, usafiri wao, sehemu sahihi za mazoezi, sehemu sahihi za waandishi na vyombo vya Habari lakini mashabiki wana uhakika wa kwenda kuingia na kutoka uwanjani kwa usahihi bila ya bugudha.
Uwanjani ni sehemu salama na sahihi kwa burudani, ulinzi wa uhakika na huduma zinatolewa na watu wenye mafunzo. Kwa usahihi, viwanja ni rafiki.
Ahly sasa wanakwenda kuwavaa Seattle Sounders huku wenyeji Wydad wakisubiri kuwavaa Al Hilal ya Saudia. Hakuna mechi ya kitoto hapo.
Vigogo Flamengo na Madrid watakuwa wanasubiri kuanzia hatua ya nusu fainali. Baada ya mechi moja wakishinda ni fainali. Maana yake hapo mshindi kati ya Ahly na Sounders na Wydad na Hilal ndio watakwenda kukutana na wababe hao.
Kwa Morocco kama utakuwa unaisikia ukiwa mbali basi unaweza kuona mambo kama hayatawezekana hivi lakini ukiwa hapa utagundua kuwa wamejiandaa vyema na wana uzoefu mkubwa na mashindano ya kariba hii ndio maana inaweza isiwe kazi ngumu sana kwao hata kuandaa Kombe la Dunia kwa kuwa wana vifaa na uzoefu wa kutosha.
Mashindano ndio yameanza, Afrika ina vigogo wawili kutoka Kaskazini, ligi mbili bora za Afrika kwa zimetoa timu.
Swali kuna nafasi ya Afrika wakiwa katika ardhi yao na timu mbili kufika angalau fainali? Acha tuendelee kufuatilia, jibu litapatikana siku chache zijazo.
Imeandikwa na Saleh Ally, Morocco