The House of Favourite Newspapers

Kombora la Israel Laangusha Jengo la Ofisi za Al Jazeera

0

MASHAMBULIZI  makombora katika eneo la Gaza yanaingia siku ya sita mfululizo, huku idadi ya vifo ikiongezeka kufikia watu 140, wakiwamo watoto 39.

 

Israel imeendelea kutumia makombora kushambulia majengo marefu katika eneo la Gaza, ikilenga jengo la ofisi za Shirika la Habari la Al Jazeera na Associated Press (AP) siku ya Jumamosi.

 

Al Jazeera ilirusha mubashara picha za wakati kombora la Israel lilipopiga ofisi zake, hii ni baada ya uongozi wa Shirika hilo kupokea simu kutoka Jeshi la Israel likiwaonya kuwa watashambulia jengo hilo, Wafanyakazi wa mashirika yote mawili waliondoka kabla ya tukio hilo.

 

Shirika hilo limeripoti kuwa wafanyakazi walipewa saa moja tu kuondoka ndani ya jengo hilo la Al Jalaa, lakini mmiliki wa jengo alijaribu kuwaomba wanajeshi wa Israel wamwongezee nusu saa nyingine ili watu waweze kutoa vifaa vyao kutoka ofisini. Jeshi la Israel lilikataa kuongeza muda na baada ya saa moja jengo hilo likashambuliwa kwa kombora.

 

“Ni uharibifu mkubwa. Mamia ya familia zimelazimika kuondoka katika jengo hilo na majengo mengine ya pembeni, hii inamaanisha kuwa sasa familia hizo zinaongezeka kwenye idadi ya maelfu wengine ambao hawana makazi.

Hakuna sehemu salama tena ndani ya Gaza,” anasema Youma al-Sayed, Mwandishi wa Habari wa Al Jazeera wa Gaza.

 

Mkurugenzi Mkuu wa AP, ambayo ilikuwa ikitumia jengo hilo la Al Jalaa pamoja na Al Jazeera, amesema ameshtushwa na shambulio la Israel kwenye ofisi zao.

 

Kitendo hicho cha Israel kimelaaniwa vikali na Rashida Tlaib, mjumbe wa Bunge la Congress nchini Marekani mwenye asili ya Palestina akisema kitendo cha kushambulia vyombo vya habari kinafanywa makusudi na Israel ili kuifumba macho dunia isione mauaji ya watoto na wazazi wa Kipalestina yanapofanyika.

 

Leave A Reply