The House of Favourite Newspapers

Benki ya Exim Yamuunga Mkono Pinda Upandaji wa Miti 10,000

0
Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda (kushoto) akijadili jambo na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambae kwa sasa ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Binilith Mahenge (Kulia), Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Bw Stanley Kafu (Katikati) na wafanyakazi wengine benki hiyo wakati wa zoezi hilo la upandaji miti.

Benki ya Exim Tanzania imeungana na Waziri Mkuu Mstaafu Mh Mizengo Pinda katika kufanikisha kampeni maalum ya kupanda miti 10,000 katika kata ya Zuzu jijini Dodoma ili kuunga mkono juhudi za serikali katika kuhifadhi mazingira.

Jitihada za benki hiyo ni muendelezo wa mpango mkakati wake wa kutunza mazingira ujulikanao kama ‘Exim Go Green Initiative’.

Katika kufanikisha kampeni hiyo iliyoratibiwa na taasisi ya Habari Development, benki hiyo pia ilichangia fedha ili kufanikisha ununuzi wa miti katika zoezi hilo muhimu lililohudhuriwa pia na viongozi waandamizi wa serikali waliojitokeza kuunga mkono jitihada za Waziri Mkuu huyo mstaafu.

Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda akikamilisha zoezi la upandaji wa mti kwa kumwagilia maji wakati wa uzinduzi wa kampeni maalum ya upandaji wa miti 10,000 jijini Dodoma inayoratibiwa na na taasisi ya Habari Development kwa kushirikiana na Benki ya Exim Tanzania kupitia mpango mkakati wa benki hiyo ujulikanao kama ‘Exim Go Green Initiative’. Wanaoshuhuda ni pamoja na Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Bw Stanley Kafu (Katikati) . Zoezi hilo lilifanyika katika kata ya Zuzu jijini Dodoma.

Baadhi ya viongozi hao ni pamoja na  aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambae kwa sasa ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Binilith Mahenge, wafanyakazi wa benki hiyo, walimu na wananchi wa kata hiyo.

Akizungumza wakati watukio hilo, Mh Pinda pamoja na kuipongeza benki ya Exim kwa kufadhili zoezi hilo muhimu, alielezea umuhimu wa kutunza mazingira huku akibainisha baadhi ya changamoto zitokanazo na uharibu wa mazingira kuwa ni pamoja na ukame na mabadiliko ya tabia nchi.

“Ndio maana binafsi nimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba  nashirikiana kikamilifu na wadau mbalimbali zikiwemo taasisi kama benki ya Exim ili kwa pamoja tuhakikishe tunaitengeza Tanzania ya kijani’’ alisema Mh Pinda ambae alitumia pia wasaa huo kuwatembeza wageni hao kwenye miradi yake mbalimbali ikiwemo ya kilimo na utunzaji wa mazingira.

Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wafanyakazi wa benki ya Exim wakiongozwa na Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Bw Stanley Kafu (watatu kulia) kwenye makazi ya Waziri Mkuu huyo mstaafu mara baada ya kukamilika kwa zoezi hilo la upandaji miti.

Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha Masoko na Mawasiliano, Bw. Stanley Kafu alisema utunzaji mazingira ni sehemu ya vipaumbele vya benki hiyo na ndio sababu imekuwa mstari wa mbele kubuni na kuunga mkono jitihada mbalimbali za utunzaji mazingira nchini ikiwemo upandaji wa miti na utunzaji wa bustani mbalimbali zilizopo katikati ya miji na majiji mbalimbali hapa nchini.

“Mabadiliko ya tabia nchi yanayosababishwa uharibifu wa mazingira yamekuwa na athari kubwa kiuchumi kwakuwa yamekuwa yakizorotesha pia shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo, ufugaji na ustawi wajamii kwa ujumla. Ni wazi kwamba hatuwezi kutenganisha athari hizi na ufanisi wa biashara za kibenki,na hiyo ndio sababu tunashiriki kikamilifu katika kutatua changamoto hii,’’ alifafanua.

Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda akiwaelekeza wafanyakazi wa benki ya Exim kuhusu ufugaji wa samaki wakati wafanyakazi hao walipotembelea miradi mbalimbali ya kilimo, uvuvi na ufugaji kwenye makazi ya Waziri huyo mstaafu jijini Dodoma.

Alisema kibiashara pia benki hiyo imekuwa ikitoa kipaumbele kwenye utoaji wa mikopo inayohusisha miradi inayozingatia utunzaji wa mazingira sambamba na kutumia mifumo ya kisasa ya teknolojia ya mawasiliano na utunzaji wa kumbukumbu ili kupunguza matumzi ya karatasi.

Baadhi ya wafanyakazi wa Benki ya Exim tawi la Dodoma wakiendelea na zoezi hilo la upandaji miti.

Zaidi, aliwasihi wananchi hususani wakazi wa kata ya Zuzu kuzingatia na kuheshimu sheria zinazosimamia na kulinda misitu ili waweze kunufaika na rasilimali hiyo muhimu huku akiahidi kuchimba kisima kwa ajili ya kuwezesha umwagiliaji wa miti hiyo.

Leave A Reply