The House of Favourite Newspapers

Kuelekea Kariakoo Dabi.. Nabi Asuka Mikakati Mipya Yanga, Aanza Na Gym

0
Wachezaji wa timu ya Yanga.

JESHI lote la Yanga juzi Jumatatu jioni liliingia kambini tayari kwa ajili ya mchezo wa Kariakoo Dabi huku Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mtunisia, Nasreddine Nabi akisuka mikakati mipya ya ushindi katika mchezo huo.

 

Dabi hiyo inatarajiwa kuzikutanisha timu kongwe za Yanga dhidi ya Simba utakaopigwa Jumapili hii saa 11:00 jioni kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

 

Katika mchezo huo, Yanga wataingia uwanjani wakiwa na hasira ya kutoka kutolewa dhidi ya Al Hilal ya nchini Sudan katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Akizungumza na Championi Jumatano, Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi alisema kuwa maandalizi ya mchezo wa dabi yameanza jana Jumanne kwa kuanza program moja ya gym pekee asubuhi kabla ya leo Jumatano kufanya ya kimbinu zaidi.

 

Nabi alisema kuwa mara baada ya timu hiyo, kuingia kambini juzi Jumatatu usiku, alifanya kikao na wachezaji wote na kikubwa kuwatengeneza kisaikolojia kwa kuwataka kusahau matokeo yaliyopita dhidi ya Al Hilal na badala yake kuelekeza nguvu katika dabi hiyo.

Aliongeza kuwa kutolewa kwao Ligi ya Mabingwa Afrika sio sababu ya wao kufungwa katika dabi, hivyo amepanga kukiboresha kikosi chake vema katika baadhi ya sehemu ili kuhakikisha anapata matokeo mazuri kwenye mchezo huo.

 

“Nimeona makosa tuliyoyafanya katika michezo miwili dhidi ya Al Hilal na kusababisha tutolewe katika Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo nimepanga kufanyia maboresho ili kuhakikisha tunapata matokeo mazuri katika dabi.

 

“Hivyo timu imeingia kambini jana (Jumatatu) jioni na Jumanne asubuhi tumeanza mazoezi ya gym kwa ajili ya kuongeza fitinesi kabla ya jioni yake kuanza yale ya kimbinu zaidi.

 

“Kikubwa nimewataka wachezaji wangu wasahau matokeo yaliyotokea Sudan tulivyocheza dhidi ya Al Hilal na kutolewa nao katika Ligi ya Mabingwa Afrika na badala yake kuhamisha akili na nguvu katika mchezo huu wa dabi ili tupate matokeo mazuri ili turudi katika mstari,” alisema Nabi.

STORI: WILBERT MOLANDI NA MUSA MATEJA

Leave A Reply