The House of Favourite Newspapers

KUELEKEA MKUTANO WA MAJAJI; JAJI MKUU AMGUSA LISSU -VIDEO

0
JAJI MKUU wa Tanzania
Jaji Mkuu akizungumza na waandishi wa habari leo.
JAJI MKUU wa Tanzania
Rais wa Chama cha Mahakimu na Majaji, Ignas Kitusi, akiongoza mkutano na waandishi wa habari.

 

JAJI MKUU wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, leo amesema shambulio la kupigwa risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, ni kitendo cha uhalifu mkubwa hivyo kitu cha kwanza kinachotakiwa kufanywa ni kukusanya ushahidi ili upelekwe mahakamani.

Jaji Mkuu huyo alifafanua hilo baada ya kutupiwa swali na mwandishi wa habari kuhusu waraka wa Chama cha Wanasheria cha Bar Human Rights Comitee cha Uingereza ambacho kimezungumzia tukio la kushambuliwa kwa kiongozi huyo kwenye barua yao waliyoiandika na kumpelekea Rais Dk. John Magufuli.

Katika waraka huo mzito chama hicho pia kimeelezea matukio ya kukamatwa mara kadhaa na baadaye kupigwa risasi na watu wasiojulikana kwa Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS).

Sehemu ya barua hiyo imelaani vikali matukio hayo na kutaka chombo huru kipewe nafasi ya kufanya uchunguzi.
Profesa Juma alisema tukio la Lissu linahitaji kukusanywa kwa ushahidi.

“Ushahidi huo utakusanywa hapa nchini, asikudanye mtu kuwa kuna mtu atatoka nje aje kukusanya ushahidi hapa nchini, ushahidi utakusanywa hapahapa Tanzania, sasa sisi mahakamani kanuni zetu haturuhusiwi kuongelea jambo ambalo tunaona litaletwa mahakamani.

“Ndiyo maana mnatuona kimya, kwenye mitandao watu wanajaribu kutuvuta lakini hatutaweza kusema chochote,” alisema.
Akaongeza :”Tutakapoona waliopewa jukumu la kukusanya ushahidi wameshindwa kufanya hivyo ndiyo tupige kelele kwani hata waraka unahimiza uchunguzi ufanywe na wahusika wapelekwe mahakamani.”

Aliongeza kuwa tukio hilo la Lissu ni funzo kwa nchi kuhusu kupambana na uhalifu kwani nchi nyingine kama Nairobi (Kenya) kuna CCTV barabarani.

Aidha katika mkutano huo alizungumzia mkutano unaotarajiwa kufanyika hapa nchini wa Chama cha Majaji na Mahakimu wa Jumuiya ya Madola unaotarajiwa kufanyika Septemba 24 hadi 28 mwaka huu utakaofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Benki Kuu Dar es Salaam.

Alisema kuwa mkutano huo hufanyika kila mwaka ukiwakutanisha wanachama wake kutoka nchi mbalimbali ambapo mkutano wa mwaka jana ulifanyika nchini Guyana.

Kaulimbiu ya mkutano huo ni Mahakama Madhubuti, Inayowajibika na Jumuishi’ na kwamba madhumuni hayo yanaendana na misingi ya utekelezaji wa mpango mkakati wa mahakama wenye nguzo kuu tatu ambazo ni utawala, uwajibikaji na usimamizi wa raslimali.

NA DENIS MTIMA/GPL

JAJI MKUU AKIZUNGUMZA

Leave A Reply