The House of Favourite Newspapers

KUHUSU MFEREJI WA MAJI HAYA…. MBAGALA WAIANGUKIA SERIKALI

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Juhudi uliko Mbagala Kizuiani, Athuman Namna akionesha uharibifu wa makazi ya watu ambao umetokana na maji kutuama eneo hilo kutokana na kukosekana kwa mitaro ya kupitisha maji ya mvua katika mtaa huo.
WANANCHI wa Mbagala Kiuzuiani Mtaa wa Juhudi wameiomba Halmashauri ya Wilaya  Temeke katika Mkoa wa Dar es Salaam kuwawekea mifereji ya kupitisha maji ya mvua ili kunusuru makazi yao na watu wa maeneo hayo.
Wamesema katika eneo la Juhudi changamoto kubwa ni maji kujaa katika makazi ya watu ambayo msingi wake mkubwa ni kukosekana kwa mifereji ya kupitisha maji ya mvua,hivyo yanalazimika kupata katika barabara  na matokeo yake yanakwenda kutuama katika makazi ya watu.
Wakizungumza leo wakazi wa mtaa huo wakiongozwa na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Juhudi Athuman Namna, wamesema ombi lao kubwa ni eneo hilo kuwekwa mifereji kwani wanaamini ndio ufumbuzi wa kero ya maji kutuama ambayo ni ya muda mrefu huku wakieleza matumaini yao kwa Serikali ya Awamu ya Tano ambayo imejikita kuwasiliza wanyonge na kutatua kero zao.
Wakati mvua za masika zikianza kushika kasi katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo  mkoa wa Dar es Salaam wakazi wa mtaa wa Juhudi kata ya Kiburugwa wameeleza hofu yao kufuatia mvua hizo.
Wamesema kukosekana kwa mitaro ya kupitisha maji makazi yao  yamekuwa njia ya maji taka na inapofika msimu wa mvua maisha yao wanakuwa hatarini pamoja na uwepo wa magonjwa ya mlipuko yakiwamo ya kipindupindu.
Wakati huo huo mkazi  wa eneo hilo Rashid Mgaza amesema kuwa hali ya kufurika maji wakati mwingine inasababisha watoto kushindwa kwenda shuleni kwani kuna wakati maji yanakuwa mengi kiasi cha kufika usawa wa madirisha ya nyumba.
“Mvua zikinyesha wakazi wa Juhudi hatuna amani kwanza hata mtoto akienda shule unakuwa roho juu hayo maji yanayotiririka hata mtu mzima ni hatari kupita sasa ndio apite mtoto.Ombi letu kwa Serikali itusikie huku nako tunaoishi ni watu na kwa kuwa serikali yetu ni ya wanyonge basi itusikie na kutupatia ufumbuzi wa changamoto hii,” amesema Mgaza.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Juhudi, Athuman Namna amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kueleza kuwa imesababishwa na maji yanayotoka maeneo ya juu kukosa mwelekeo na matokeo yake yanashuka chini kwenye makazi ya watu.
Ameongeza kwa nafasi yake na kwa kushirikiana na wananchi wamechukua hatua mbalimbali za kuwasilina na viongozi wa Manispaa ya Temeke lakini bado hawajapata ufumbuzi wa tatizo hilo.
“Tukisikia mvua amani inatoweka huku kwetu na kama hii iliyotangazwa watu wanalazimika kuacha nyumba zao lakini ikitengenezwa mifereji hili tatizo litakuwa historia,”
“Niwaombe viongozi wangu wasikae ofisini waje kuona hali ilivyo maana kwa kuambiwa unaweza usielewe ila ukweli ni kwamba tuna wakati mgumu sana kuelekea hiki kipindi cha mvua,”amesema Namna.
Wakazi wengine wamesema hawana tatizo na Serikali kwani wanaimani na ndio maana haja ya kutoa kilio cha hasa kipindi hiki ambacho mvua hazijashika kasi kwani kuna hatari zaidi kama hakutafanyika jitihada za kuwekwa mitaro hivi sasa.”

Comments are closed.