The House of Favourite Newspapers

Kuingia Kwa Chillah WCB Asipojizatiti, Kaburi lingine!

Q Chillah na Richard Mavoko

Na ERICK EVARIST| CHAMPIONI JUMAMOSI| MAKALA

MUZIKI ni biashara hilo halina ubishi. Kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele, upinzani katika muziki hususan wa Bongo Fleva unazidi kuongezeka. Japo si kwa wote, lakini wasanii wengi wanaufanya muziki huu ‘serious’. Wanatengeneza fursa! Ndiyo maana unaona vijana wanajikusanya pamoja, wanatengeneza uongozi wao na kusimamia kazi zao.

Tunaona kama Weusi wanafanya vizuri na Weusi Kampuni. Uongozi wao umesimama, wanafanya biashara ya muziki na ukweli inawalipa. Mkubwa Fella anafanya vizuri na Yamoto Band, ametanuka na kuanzisha Kundi la Muziki wa Taarab, Yah TMK Modern na fursa zinaonekana. Ali Kiba naye yupo ndani ya mikono salama ya uongozi wa Rockstar4000 ambayo inawasimamia wasanii wengine kama Baraka The Prince na mkongwe Lady Jaydee.

Ukirudi upande wa pili kuna Wasafi  Classic Baby (WCB), unakutana na rais, Nasibu Abdul ‘Diamond’ anafanya kazi na vijana wengi wazuri kama Rayvanny, Harmonize na Rich Mavoko.

Ray Vanny

Wote hao wana uwezo mkubwa ndiyo maana unaona kuna ushindani wa hali ya juu. Wakati Rich Mavoko anasaini WCB mwaka jana, aliwakuta vijana waliokuwa wanachipukia, Rayvanny na Harmonize, wanachuana kweli. Wengi wakabashiri kwamba huenda Rich Mavoko aliyekuwa levo moja na Diamond, alikwenda kujichimbia kaburi.

Kweli akajitutumua akaanza kutoa Ngoma ya Imebaki Stori ambapo video yake aliifanyia nchini Afrika Kusini, watu wakaupokea vizuri. Baada ya muda, bwa’mdogo Rayvanny akaomba namba kwa rais, Diamond akapewa na wakafanya naye Salome. Salome ukawa wimbo mkubwa sana, si kwa maana tu Diamond ameshiriki lakini uwezo wa Rayvanny ulichagiza kwa kiasi kikubwa kwenye mafanikio ya wimbo huo. Huku na huku, Rich Mavoko akaja tena na Kokoro akimshirikisha rais wake, Diamond. Hapa utaona ni jinsi gani Diamond mwenyewe hataki kupitwa.

Q Chillah

Hataki kufi chwa, anautamani ufalme wake uendelee. Huku akiwapa nafasi f’lan hafi fu wanaomfuata wasiweze kuvimba kichwa na kuwa rais. Kuna uwezekano mkubwa sasa mkongwe mwingine, Aboubakar Shaban Katwila ‘Q Chillah’ akasaini mkataba na WCB. Anaingia kwenye ulimwengu wa vijana wakali, Rayvanny na Harmonize. Huku pia na Rich Mavoko anayetamani kutusua maana analingana umri na rais. Ushindani utakuwa mkubwa.

Asipoangalia Q Chillah anaweza kuanguka. Kuweza kutoboa kwenye miamba kama ile, inahitaji nguvu ya ziada. Bado kuna taratibu na kanuni za uongozi. Naamini uongozi nao hauwezi kumruhusu saana Q Chillah afanye anavyotaka. Atabanwa tu! Anahitaji nguvu ya ziada. Pili, Q Chillah anapaswa kuwa makini pia kwenye suala zima la mikataba.

Meneja wa WCB Salam Sk wa kwanza (kushoto), Rayvanny na Richard Mavoko

Isimbane sana katika kutoa ngoma. Awe huru kuachia na kusapotiwa ngoma zake. Alikotoka kule kwa Q-S Mhonda, Chillah alikuwa na fursa ya kurekodi kadiri anavyotaka lakini sayansi ya muziki au mfumo ukawa umekataa. Ukisikiliza mazungumzo ya uongozi wake wa awali, unamtuhumu kwa mambo ambayo yanaweza kuwa na hoja au yasiwe na hoja.

Kama binadamu, kama ni kweli tuhuma zile zinazoonesha Q Chillah amepoteza nidhamu ya kazi, basi ajirekebishe maana sehemu anayotarajia kuingia inaongozwa na nidhamu ya hali ya juu ya muziki. Asije kuanza kuzuiwa vitu fulani, mfano labda kama ni mlevi sana akaona ni adhabu, anapaswa kuheshimu muziki.

Q Chillah kila mtu anajua uwezo wako. Anajua wapi umetoka, wewe ni fundi, fundi hasa. Ni bidhaa adimu sana katika Muziki wa Bongo Fleva hivyo jukumu lako ni kuamua.

Waswahili wanasema kupanga ni kuchagua, kama ulivyoamua kuacha madawa ya kulevya unaweza pia kuamua aina ya maisha unayotaka kuishi na Watanzania wakainjoi muziki mzuri kutoka kwako urudi kule tulipokuwa tukikusikia haushikiki na ngoma zako kali kama Si Ulinikataa,Ninachokipata, Zaidi ya Jana na Mariam. Uukubali mfumo wa kisasa. Muziki umebadilika, kuna namna ambayo Wasafi  wanafanya ili kuendana na soko hivyo unapaswa kuendana nao. Ukiukataa ni sawa na kujitengenezea kaburi lingine katika muziki wako.

Comments are closed.