The House of Favourite Newspapers

Kumbe dharau za Zahera ziliiponza Yanga

KOCHA Msaidizi wa Lipuli FC, Selemani Matola, amesema dharau za Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, ndiyo sababu kubwa ya kupoteza mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), juzi Jumatatu.

 

Matola aliliambia Championi Jumatano kuwa, alimsikia Zahera akisema wameenda Iringa kuwaaibisha wenyeji wao kitu ambacho ilionekana ni dharau.

 

Aliongeza kuwa, baada ya kusikia kauli hiyo, alipania kuwafunga Yanga ili kukwepa aibu na dharau za Zahera ambaye alisema kwenye mchezo wa ligi walipocheza uwanjani hapo, walifungwa kwa kwa bahati.

“Mbali na vijana wangu kuahidiwa shilingi laki 5 kwa kila bao, bado tulijipanga kushinda ili kukwepa fedheha ya kuambiwa tumenunuliwa na Yanga.

“Lakini pia hakuna jambo ambalo lilitukwaza kama kusikia kocha mwenzangu akisema mchezo wa kwanza tulibahatisha na akisahau ubora wa vijana wangu ambao ndiyo chachu ya ushindi wetu huku akisema amekuja kutuaibisha,” alisema Matola.

 

Aliongeza kuwa; “Tulikuwa na nafasi ya kuwapiga mabao matano kutokana na kasi ambayo tulianza nayo kipindi cha kwanza na kipindi cha pili ila ndio hivyo tumeambulia mabao mawili.”

 

“Kwa Yanga ukiwabana mabeki na ukicheza kwa nidhamu ni rahisi kushinda hivyo hawakunipa kazi kuwamaliza, sasa kazi inayofuata ni dhidi ya Azam FC hakieleweki mpaka tubebe ubingwa,” alisema Matola.

 

Hii inakuwa mara ya kwanza kwa Lipuli kutinga hatua ya fainali ya shirikisho ambapo bingwa wa michuano hii anaiwakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa.

Stori Musa Mateja na Lunyamadzo Mlyuka

Alivyotangazwa MWENYEKITI Mpya wa YANGA, Toborowa Atoa Neno!

Comments are closed.