KUMEKUCHA TENA…NABII TITO AKIRI KUANGAMIZA WATU

KUMEKUCHA tena! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Nabii Tito Machibya kuibuka na kusema ameokoka kwa sasa yeye na mkewe ambapo amempokea Roho Mtakatifu kupitia Kanisa la BCIC lililopo Mbezi Jogoo jijini Dar es salaam chini ya Mchungaji Sylvester Gamanywa ambapo amekiri kuangamiza watu wengi kutokana na shetani aliyekuwa akimtumia afanye mahubiri ya kupotosha watu.

 

AFUNGUKIA WIKIENDA

Akiongea na Ijumaa Wikienda, Nabii Tito ambaye aliushangaza umma uliokuwa umehudhuria mkesha wa maombezi uliofanyika siku ya Ijumaa wiki iliyopita kwenye kanisa hilo alidai kuwa, kwa sasa ameamua kuokoka kwani njia aliyokuwepo ilikuwa ni ya shetani ambaye alikuwa akimtumia. “Unajua kwa sasa nimeamua kuokoka kwa sababu kule nilipokuwa, nilikuwa nikitumiwa na shetani na nimewaangamiza watu wengi kwa ushawishi wangu,” alisema Nabii Tito.

 

AZUNGUMZIA MATATIZO YAKE YA AKILI

Aidha, Tito aliongeza kwa kusema kuwa anasikitika kuelezwa kuwa yeye hana akili timamu; lakini ukweli ni kwamba yeye anazo akili nzuri ila aliyesababisha yote hayo ni shetani aliyekuwa akimtumia. “Mimi nina akili yangu timamu, shetani alinitumia vibaya ndiyo maana nikawaangamiza na watu wengine, kwa sasa nimempokea Yesu Kristo na nimeamini kuwa yupo kweli,” alisema.

 

APEWA USHAURI

Tito aliendelea kusema yupo hapo kanisani kwa ajili ya kupata ushauri na kujiweka sawa na endapo atakuwa sawa atakuwa nabii wa kweli na si wa uongo aliokuwa nao mwanzo. “Kwa sasa nimempokea Roho Mtakatifu na nipo kwenye ushauri nasaha naamini nikiiva kiroho naweza kuhudumu kama manabii wengine kwani nipo tayari kumtumikia Mungu,” alisema Tito.

 

MCHUNGAJI GAMANYWA AAHIDI KUMUONA

Baada ya kujieleza kwa mwandishi wetu aliyekuwa kanisani hapo alikwenda mbele ya kanisa ambako Mchungaji Gamanywa alikuwa akiongea na watu waliompokea Roho Mtakatifu na kutoa ushuhuda akajieleza kuwa; yeye ni Nabii Tito, amemuamini Kristo rasmi.

 

Kauli hiyo ilimshangaza mchungaji Gamanywa na kumhoji mara mbilimbili kisha akaahidi kuonana naye siku ya Jumanne wiki hii kwa maombezi zaidi.“Wewe ndiyo Tito yule, kweli? Basi nitakuona siku ya Jumanne,” alimwambia ambapo watu waliokuwa eneo hilo walikuwa wakimshangaa kwani hawakuwa na ufahamu kuwa yupo pale.

 

Waumini waonywa Waumini wa makanisa mbalimbali wameonywa kuacha kukimbilia makanisa mapya pasipo kuwajua baadhi ya wachungaji na huduma zao na ndiyo maana akawepo mchungaji Tito ambaye leo anakiri kuangamiza watu kwa mahubiri yake yaliyojaa upotoshaji mwingi wa neno la Mungu.

 

Tujikumbushe

Nabii Tito alikuwa maarufu siku za nyuma alipoanza kupita mitaa ya Posta, jijini Dar na kutangaza pombe kuwa inaruhusiwa na ni sehemu ya Maandiko Matakatifu. Aidha katika mafundisho yake hayo ambayo leo amekiri kuwa yalikuwa ya kupotosha watu kwa kusudi la kuwapeleka motoni. Ikumbukwe kuwa, alikuwa akiwahubiria watu kuwa mume kutembea na mfanyakazi wake wa kike wa ndani si dhambi.

 

“Eee mbona hata Nabii Ibrahimu alifanya mapenzi na mfanyakazi wake wa ndani na akazaa naye, kwa nini wanaume wa leo hawafanyi hivyo?” Nabii Tito aliwahi kuhubiri hivyo siku za nyuma. Kutokana na msimamo wake huo mkewe naye aliwahi kujitokeza na kutoonesha kujali pale mume wake Tito alipokuwa ‘akijisogeza’ karibu na mfanyakazi wao wa ndani.

 

Nabii huyo pia alikuwa akiruhusu waumini wake kucheza nyimbo za mapenzi na kukata nyonga kanisani, pia aliwaruhusu watu kutumia mkorogo na kuisifu pombe kuwa ni dawa ya magonjwa ya tumbo na kwamba watu wanapaswa kuinywa ili kujitibu.

 

Hata hivyo, nabii huyo alikuja kupoteza mvuto pale alipojaribu kujiua na hatimaye kukamatwa na polisi na kutakiwa kupelekwa Hospitali ya Magonjwa ya Akili, Merembe iliyopo mkoani Dodoma jambo ambalo mwenyewe alilipinga kwa kusema yeye ni mzima na hana tatizo lolote.

EXCLUSIVE: ‘BABA D’ ANAONGEA NA DIAMOND AFANYE NAE KOLABO |+255 GLOBAL RADIO


Loading...

Toa comment