The House of Favourite Newspapers

Kumekucha, Watanzania Wakwanza Kilimanjaro Marathon Kuzawadiwa Viwanja na SPC

0

WAANDAAJI wa Kilimanjaro Premium Lager Marathon wametangaza mdhamini mpya wa mbio hizo, Surveyed Plots Company (SPC) Ltd ya Jijini Dar es Salaam ambayo itatoa zawadi ya viwanja kwa mtanzania wa kwanza wa kiume na wa kike katika mbio za km 42 za mwaka huu.

“Gharama zote za kusajili viwanja hivyo kwa majina ya washindi  zitagharamiwa na kampuni ya SPC Ltd,”walisema waandaaji hao katika taarifa iliyotolewa Jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Executive Solutions Limited waandaaji wa mbio hizo, Aggrey Marealle.

 

Mkuu wa Uendeshaji wa kampuni ya SPC, Kenny Rodgers, alisema wanajivunia kuwa sehemu ya mashindano makubwa ya Kilimanjaro Marathon 2022. “Hili ni tukio kubwa na ni nafasi nzuri kwetu kujitangaza kwani haya ni mashindano makubwa ya riadha katika ukanda mzima wa Afrika Mashariki na hasa ikizingatiwa kuwa mashindanoi hayo yanaadhimisha miaka 20,” alisema.

“Tutafanya utaratibu wa kuwamilikisha viwanja hivyo kwa majina yao na kuwapa nyaraka zote,” alisema Bw. Rodgers.

Alitoa wito kwa watanzania wajifue na kujiandaa vizuri kwa mbio hizi za Km 42 ili wajishindie viwanja hivi. “Tunaamini ushindani utakuwa mkubwa kwa hivyo watakaojiandaa vizuri wana nafasi kubwa sana ya kushinda mwisho wa siku,” alisema.

Wadhamini wa mbio za Kilimanjaro Marathon 2022 ni Kilimanjaro Premium Lager (Mdhamini Mkuu) Tigo (21km) na Grand Malt (5km).

Wadhamini wa meza za maji ni pamoja na Absa Tanzania, Unilever Tanzania, TPC Sugar, Simba Cement na Kilimanjaro Water. Wasambazaji rasmi ni GardaWorld Security, Keys Hotel, Kibo Palace Hotel, CMC Automobiles na Surveyed Plots Company Ltd (SPC) na Bodi ya Utalii (TTB).

Katika hatua nyingine, Kwa mujibu wa waandaaji wa Kilimanjaro Marathon, kwa mara ya kwanza kutakuweko na maonesho yanayojulikana kama Kili Expo (The People’s Expo) ambapo wadhamini na wadau wengine wa mbio hizo watapata fursa ya siku tatu za kuonyesha bidhaa na huduma wanazotoa, maonyesho ambayo yanatarajiwa kufanyika kati ya Februari 24-26, 2022, katika viwanja vya MoCU.

“Maonyesho haya pia linakusudiwa kuwapa umma uzoefu wa muda mrefu wa mbio za Kili Marathon; pia kwa mwaka huu wanaotarajia kushiriki mbio hizo watapata fursa ya kuchukua namba zao za ushiriki eneo la chuo kikuu cha Ushirika badala ya eneo la hotel kama ilivyokuwa miaka ya nyuma”, ilisema taarifa hiyo ya wandaaji.

Mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon, zinatarajiwa kufanyika Jumapili ya Februari 27, 2022, katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), ambapo zimeandaliwa na taasisi ya Kilimanjaro Company Limited na kuratibiwa na wadau wa hapa nchini kampuni ya Executive Solutions Limited.

Leave A Reply