Kumradhi Mawaziri Wa Afya

Jana, Machi 8, 2021 katika mtandao huu, kuliripotiwa taarifa iliyokuwa na kichwa cha habari: MAWAZIRI WA AFYA WAIKUBALI IMMUNO BOOSTER KUPAMBANA NA CHANGAMOTO ZA UPUMUAJI.
Msingi wa habari hiyo, ilikuwa ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Doroth Gwajima na Naibu wake, Dk. Godwin Mollel kutembelea banda la mtaalamu wa dawa za asili, Tabibu Riziki wa Kampuni ya Natural Therapy LTD na kujionea dawa mbalimbali alizokuwa anazizalisha, ikiwemo Immuno Booster yenye uwezo wa kupambana na changamoto za upumuaji na Corona.
Kwa bahati mbaya, baadhi ya maneno yaliyokuwemo katika habari hiyo, yamefanya habari nzima itafsiriwe tofauti kabisa na malengo ya awali ya mwandishi.
Lengo lilikuwa ni kuonesha jinsi mawaziri wanavyofurahishwa na wataalamu wa tiba asili wanaoendelea kujitokeza kuunga mkono maagizo ya serikali ya kuwataka wananchi watumie zaidi njia za asili za kupambana na maradhi mbalimbali yakiwemo ya changamoto za upumuaji.
Tunaomba radhi kwa Waziri Gwajima, Naibu Waziri, Dk. Mollel na watu wote ambao kwa namna moja au nyingine, wamepata usumbufu kutokana na kuchapishwa kwa habari hiyo! Tunaahidi kuendeleza umakini zaidi na kusimamia weledi wa taaluma ya uandishi wa habari!
Mhariri!

