The House of Favourite Newspapers

KUNA MAISHA BAADA YA KUUMIZWA, YATAFUTE HIVI !

Related image

DUNIA ya wapendanao kila siku ina mambo mapya. Huyu anaingia huyu anatoka. Kuna ambaye analia na kuna ambaye anacheka. Anayecheka si rahisi sana kumfikiria anayelia, anaamini kama vile mambo yanavyomuendea vizuri basi wote mambo yao yako vizuri.  

Ndugu zangu, mapenzi yana siri nzito. Unaweza kuingia kwenye uhusiano ukajiona umefika kumbe wapi, bado hujafika. Mwanamke au mwanaume uliyenaye ni wa mpito tu. Mtu utakayeingia naye kwenye ndoa ni mpenzi wa pili au wa tatu atakayefuata baadaye. Historia ya kuumizwa mara kwa mara kwenye mahusiano huwa inasababisha kutoweka kwa imani.

 

Kumbukumbu mbaya huwa inajirudia kwenye akili yake na kumfanya asitamani tena kupenda. Anahisi akipenda atakutana tena na maumivu. Kama ni mwanaume, anawaona wanawake wote wapo kama yuleyule aliyemuumiza. Kama ni mwanamke basi anawaona wanaume wote duniani mwalimu wao ni mmoja na wana mbinu zilezile za kuwatesa wanawake.

 

Marafiki mnapokutana na changamoto hiyo katika mapenzi, hampaswi kukata tamaa. Haijalishi umri umekutupa kiasi gani au kwamba umeumizwa na watu wangapi lakini hilo lisikuvunje moyo. Unapaswa kujiamini, kusimama na kusema wakati wako bado haujafika. Amini kwamba kila kitu kinakuja kwa wakati na wakati wako unakuja. Utaumizwa na huyo uliyekuwa naye, atakuumiza mwingine na hata mwingine tena lakini yupo mtu mahali fulani ambaye ndio chaguo lako. Anakusubiri bila kujua kama anakusubiri wewe.

 

Jinsi mtakavyokutana, si wewe wala yeye anayejua. Kuna mazingira fulani yatawakutanisha na moyo wako utasema sasa nimefika. Nimefika si kwa sababu unajua kutathimini sana lakini mambo yenyewe yanajipa kila uchwao. Unakutana na mtu ambaye hana longolongo, hapindishipindishi maneno kama wanavyofanya vijana wasiokuwa waaminifu. Yeye anakuja kwako yupo ‘serious’ na mahusiano, hana mzaha. Akiingia kwenye uhusiano ana malengo, mkiyaunganisha safari inakwenda haraka.

Image result for couples

Kwa jinsi ambavyo mambo yatakuwa yanajipa yenyewe hapo ndipo utakapoona kweli kila jambo linakuja kwa wakati maana hulazimishi, mwenzako anakueleza kuhusu kujipanga kwa ajili ya ndoa. Anakupa mikakati yake, mnaunganisha nguvu kwa pamoja na ndani ya muda mfupi mnaoana. Kikubwa unachotakiwa kufanya pale unapoumizwa ni kutokukurupuka kuanzisha uhusiano mwingine. Tuliza sana akili yako. Usiwe na papara kwamba kila umuonaye mbele basi tu uamini ndiye atakayekwenda kuziba kovu lako.

 

Tafakari kwa muda fulani, usijutie mapito yako bali wewe furahia maisha mapya uliyonayo. Shukuru kwa yule uliyekuwa naye kuondoka kwenye maisha yako. Yawezekana ungeendelea kuwa naye angekuja kukutesa siku za mbeleni. Yawezekana angekuja kukuumiza wakati tayari, mmeshaingia kwenye ndoa jambo ambalo lingekuumiza zaidi. Amekuumiza na kukuacha katika hatua za awali, shukuru na umtakie kila la kheri huko aendako kwani hakuwa wako.

 

Yule ambaye ni maalum kwa ajili yako yupo, amini hivyo siku zote. Tembea kifua mbele, usiwe mtu wa mawazo kwani yanaweza kukusababishia matatizo ya kiafya na hata kudorora kwa ufanisi katika kazi zako za kila siku. Usikubali kuharibikiwa sababu tu ya mtu ambaye amekutenda. Achana naye, unamfikiria wa nini wakati yeye hathamini hata chembe ya maumivu yako? Kataa kuteseka, isake furaha yako kwa gharama yoyote na uhakikishe moyo wako una amani.

 

Ni matumani yangu mtakuwa mmenielewa. Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri. Mnaweza kunifuata kwenye mitandao yangu ya kijamii. Instagram na Facebook natumia Erick Evarist, Twitter natumia ENangale.

Comments are closed.