The House of Favourite Newspapers

Kuna Ulazima wa Ulinzi Huu au ni Show Off?

MIAKA ya nyuma wakati Bongo Fleva inaanza kushika kasi, wasanii hawakuwa na makuzi sana.  Mambo ya kulindwalindwa hayakuwepo kivile. Ilikuwa ni ngumu sana kukuta staa amezungukwa na hawa wanaojiita mabodigadi.

 

Sanasana katika maeneo ambayo ni hatarishi na msanii alitakiwa kwenda kufanya shoo ama kuhudhuria shughuli nyingine ya kijamii, polisi walichukuliwa na kumlinda. Ikibidi sana kwa sababu hizohizo za kiusalama, baadhi ya wasanii walikuwa wakitembea na washikaji zao ambao waliwatumia kama walinzi kiaina.

 

Kwamba kwa mfano anataka kwenda klabu usiku, anawashitua washikaji zake wawili watatu, anatimba nao ili endapo likitokea la kutokea, wao wamsaidie kwa kumpa kampani.

Hivyo ndivyo ilivyokuwa enzi zile ambazo akina Juma Nature, Prof. Jay, Ferouz, Inspector Haroun na wengineo walikuwa wanatamba.

 

Lakini siku za hivi karibuni kumekuwa na mabadiliko makubwa sana kwenye ulimwengu wa muziki huu wa Bongo Fleva, kubwa ni hili la ulinzi wa kushangaza wa baadhi ya mastaa wanapokuwa kwenye mjumuiko wa watu.

 

Yawezekana kuna wasanii wengine ambao wana utaratibu huu wa kusindikizwa na mabaunsa lakini kundi ambalo wasanii wake karibu wote wanalindwa na mabaunsa ni Wasafi Classic Baby ‘WCB’.

 

Hili lilianza kwa msanii anayefanya vizuri sana kwa sasa, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ambaye alianza kuonekana maeneo mbalimbali akiwa na ulinzi wa kutosha. Vijana wa sasa wanasema mabaunsa kama wote.

 

Kwa tunavyojua hali halisi ilivyo hasa kutokana na kuwepo kwa haya mabifu kwa wasanii, siyo jambo baya kuwa na walinzi lakini sasa ishu inakuja pale ambapo Diamond  anakuwa amezingirwa na mabaunsa kama 10 hivi.

 

Unajaribu kujiuliza; walinzi wote hao ni kweli wanahitajika au ni ‘show off’ tu na mbwembwe za mastaa wetu? Cha kustaajabisha zaidi ni kwamba, hili limehamia hata kwa wasanii wake wadogo. Harmonize alipokuwa WCB naye alikuwa kama braza wake Diamond, kila alikoenda alikuwa na mabodigadi, hata pale ambapo hakustahili kulindwa kivile.

Harmonize ameondoka WCB, ndiyo kwanza amezidisha. Kila anapokwenda anakuwa sambamba na wanaume wa shoka waliojazia ile mbaya. Ukiuliza kwa nini, utaambiwa ni kwa sababu ana maadui wanaoweza kumvamia na kumfanyia kitu kibaya, ndiyo maana kunakuwa na ukuta huo wa walinzi.

 

Hilo limekuwa hadi kwa wasanii wengine wadogo ambao wala hawahitaji kulindwa kivile kama Rayvanny, Mboso na wengineo waliopo WCB. Swali la kujiuliza ni kwamba, ni sahihi kwa msanii kama Mboso kulindwa na mabaunsa watano?

 

Na je, wanalipwaje? Halafu ni kweli kila sehemu anapokuwa Mboso anakuwa na walinzi hao au ni pale anapokuwa mbele ya kamera tu? Bado hili jambo lina maswali mengi sana ambayo majibu yake si rahisi kuyapata kwa haraka.

Hata hivyo, kilichonifanya nione hili la kuzungukwa na mabodigadi kibao ni kiki, ni tukio la juzikati la mwanadada ambaye aliwahi kuwa mpenzi wa Diamond, Irene Louis ‘Lynn’.

 

Huyu naye eti katika bethidei yake aliingia ukumbini akiwa amesindikizwa na mabodigadi kama sita hivi. Eti wote wanamlinda yeye! Unajiuliza wanamlinda kwa hatari gani ambayo mwanadada huyo iko nae? Jibu la haraka ni kwamba, hakuna hatari yoyote zaidi ya kutafuta kiki tu.

 

Na kama ni kutafuta kiki hakika ameipata kwani gumzo kubwa lilitawala kuanzia wakati anaingia ukumbini mpaka siku iliyofuata.

 

Kwa maana nyingine ni kwamba, hata mimi leo hii nikitaka niongelewe sana huko kwenye mitandao ya kijamii, nitafute vijana kama 10 hivi, niwashonee mavazi rasmi kisha kila ninapokwenda ambapo najua mapaparazi watakuwepo, naongozana nao. Sehemu ambazo hazina kamera, nakuwa na washikaji zangu tu. Si na mimi nitakiki?

Namshangaa tu Hamorapa kupitwa na kiki hii kirahisi, mshitueni, mwambieni anapitwa! Ingekuwa mimi ni Hamorapa mpenda kiki, nawazima wote hawa wanaojifanya kila sehemu wako na mabaunsa.

 

Kuwazima hao unajua unafanyaje? Unakodisha vijana kama 20 hivi ambao unaenda nao sehemu zenye watu wengi na mapaparazi. Ukifanya hivyo hii kiki itapungua nguvu maana kwa kweli tumeichoka.

Maana unajiuliza; kwani Alikiba na wasanii wengine wenye majina makubwa Bongo hawana maadui? Mbona wao hawayaendekezi sana mambo haya?

Acha niweke nukta kwa leo.

Comments are closed.