The House of Favourite Newspapers

Kutoka mkimbizi, babantilie, BBC hadi Azam TVAkutana na mkewe

0

kassim kayiraNI Kassim Kayira. Hapa tunaangazia historia ya maisha yake, tangu kuzaliwa hadi kuwa staa katika nyanja ya utangazaji ambapo kwa sasa anatamba katika anga la kimataifa katika fani hiyo.

Hii ni sehemu ya tatu, ambapo wiki iliyopita katika sehemu ya pili, tuliishia pale alipoamua kusomea masomo ya ualimu baada ya kuona kazi pekee aliyokuwa anaipenda ni kufundisha, je aliingiaje kwenye utangazaji?

CHECHEMEA NAYO…

“Kwa hiyo nikaamua kusomea ualimu katika Chuo Kikuu cha Islamic, kilichopo Mbale, Mashariki mwa Jiji la Kampala, hii ni kuanzia mwaka 1993 hadi 1996,” anasema Kayira.

“Nikiwa hapo chuoni ndipo nilikutana na mke wangu kipenzi, lakini sitamtaja jina kwa sababu inawezekana asipende kwani sijaomba ridhaa yake,” anasema Kayira huku akinitazama usoni kuona kama nilikuwa nimeridhika na msimamo huo.

“Sawa, hanma shida, hapa muhimu siyo jina la mkeo, bali historia ya maisha yako,” nami namjibu kwa haraka tena nikifunua ukurasa unaofuata wa kitabu changu cha kumbukumbu (diary), tayari kabisa kwa kuendelea kumwaga wino.

“Ok, nashukuru kwa kuwa muelewa, basi tuendelee bwana,” anasema Kayira.

“Mmh, mlikutanaje na mkeo?,” namuuliza huku nikimtazama usoni.

“Unajua kwa wakati huo, tulikuwa viongozi wa timu za michezo, Volleyball na Baseball, kwa hiyo tulikuwa na muda mwingi sana wa kukutana kama viongozi, ingawa ilikuwa kwa tahadhari kwani chuo hicho, kama nilivyoeleza hapo awali ni cha Kiislamu, hivyo kulikuwa na sheria kali sana,” anasema Kayira.

“Nini kilikuvutia kwake?,” namuuliza tena.

“Aaah, mambo mengi, lakini kikubwa zaidi ni urefu wake, hapo ni kwa siku za mwanzo, lakini nilipomjua zaidi nikagundua ni mwanamke mwenye maadili sana, mwenye mtazamo chanya kuhusu maisha, nikazidi kumpenda, nadhani hata yeye alikuwa amevutiwa na mimi,” anabainisha na kuachia tabasamu kiaina.

“Kwa hiyo ni nani alianza kumueleza mwenzake hisia zake?,” hapohapo namtupia swali la kizushi.

“Aah, hayo ni mambo binafsi bwana, muhimu ni kujua tu kuwa kila mmoja wetu alikuwa akivutiwa na mwenzake, maisha yakasonga,” anasema Kayira.

Kufikia hapo, haraka sana naingiwa na wazo la kumuuliza Kayira endapo kama ni mara yake ya kwanza kufika Tanzania, naye bila kujiuliza mara mbilimbili, anafunguka.

“Yeah ni mara yangu ya kwanza kufika hapa nchini kwenu,” anasema Kayira na kuchungulia tena kwa nje ambapo safari hii ni kupitia kioo cha mbele kwa dereva, Banzi ambaye kwa wakati wote huo, alikuwa bize na usukani wa gari huku akisikilizia mazungumzo yetu.

“Basi tuendelee kaka, kwa hiyo mkaamua kuoana mwaka huohuo?” naamua kurudisha mawazo kwenye mazungumzo yetu ya msingi.

“Hapana, hapana, kwanza ujue alikuwa nyuma yangu kwa mwaka mmoja, hivyo nilimuacha chuoni huku mipango yetu ya kuoana ikiendelea,” anasema Kayira.

“Jamani tunaingilia geti lipi?” sauti ya Banzi inatushtua baada ya kufika nje ya jengo la Azam TV, Ilala jijini Dar.

“Nadhani pitia hapohapo, hilo ni geti la kuingilia limeandikwa pale,” haraka sana anadakia Kayira na dereva wetu kufanya kama alivyoelekezwa.

“Kabla hatujaingia ndani kabisa, hebu nieleze, kwa hiyo baada ya kumaliza masomo yako ya ualimu, ulianza kufundisha shule gani?” namuuliza.

“Hata sikufanya kazi ya ualimu, ni kama nilipoteza pesa bure, kwani nikajikuta nikishawishiwa kuchukua masomo ya utangazaji kwa muda mfupi,” anasema Kayira.

Kufikia hapo, tunalazimika kuteremka na kuingia moja kwa moja hadi mapokezi ambako Kayira anapokelewa na wenyeji wake, anapewa maelekezo ya kuonana na bosi mkuu wa kituo hicho.

“Aisee, samahani sana kaka, nisubiri hapo nimalizane na bosi kwanza,” anasema Kayira huku akinionesha eneo la kukaa ili nimsubiri.

Hata hivyo, dakika mbili baadaye, Kayira anatoka na kunipa maelezo ambayo kwa mbali yananivunja moyo, anasema analazimika kusitisha mazungumzo na mimi kwa wakati huo, kwani alitakiwa kwenda mjini Dodoma kwa kazi maalum ya kituo hicho kipya cha kwanza.

Bila hiyana nakubaliana na maelezo hayo.

Je, nini kitafuata? Alifikaje huko Azam? Usikose kufuatilia wiki ijayo kwa uhondo zaidi.

Leave A Reply