The House of Favourite Newspapers

Kutumbuliwa kwa Kitwanga, Kicheko kwa Wauza Unga!

0

????????????????????????????????????

Na Mwandishi Wetu, UWAZI

KUFUATIA kutumbuliwa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga (pichani) wiki iliyopita, watu wanaojihusisha na biashara ya madawa ya kulevya maarufu kama unga, wameanza vicheko kutokana na ukali wa kiongozi huyo dhidi yao, Uwazi lina data kamili.

Mmoja wa watumiaji wa madawa hayo, aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake, alisema wauzaji hao wamepata faraja kubwa kutokana na kuondolewa kwa waziri huyo, kwani enzi zake walikuwa hawana amani, kutokana na kamatakamata iliyowaweka ndani wafanyabiashara wengi.

madawayakulevya“Jamaa alinipigia simu na kuniambia kuwa kitendo cha kuondolewa kwa waziri huyo watakisherehekea kwa kunywa mvinyo, kwani sasa watafanya kazi kwa amani tofauti na zamani,” alisema mtumiaji huyo, ambaye ni msanii maarufu nchini, akidai kupigiwa na muuzaji aliyefurahishwa kwa kutumbuliwa kwa Kitwanga.

Inadaiwa kuwa wauzaji hao, wakubwa na wadogo ambao hata hivyo wamebakia wachache baada ya wenzao kukamatwa na wengine kukimbia nchi, watafanya tafrija wakiomba mrithi wake awe mtu ‘anayezungumzika’ tofauti na Kitwanga anayedaiwa kutotaka mchezo kazini.

Tangu kuteuliwa kwake kuwa waziri wa wizara hiyo zaidi ya miezi mitano iliyopita, vita dhidi ya wauzaji wa madawa ya kulevya imefanyika kwa mafanikio makubwa, kwani wauzaji wengi wakubwa kwa wadogo wamekamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria, bila kujali nguvu yao kubwa ya kifedha.

Baadhi ya wauzaji hao wamefikishwa mahakamani na wengine wakiwa magerezani, ambapo ukamatwaji wao ulikuwa ukifanywa kimyakimya, kitu kinachowapa hofu kubwa na kulazimika kukimbia nchi.

Kufuatia madai hayo, gazeti hili juzi Jumapili lilimtafuta Kamanda wa Polisi wa Kitengo Maalum cha Kudhibiti Madawa ya Kulevya Tanzania, ACP Mihayo Msekhela (pichani) ili kutaka kujua kama juhudi za Kitwanga zitakuwa zimeondoka naye au la akasema:

“Wote wanaojihusisha na biashara hiyo waachane nayo na spidi yetu ya kuwakamata ipo vilevile hatujatetereka.

“Hivi ninavyoongea na wewe mtu mmoja Iddi Omari Kaunga mkazi wa Magomeni, nimemkamata na kete 66 za madawa ya kulevya aina ya cocaine na heroine, zinakadiriwa kufikia kilo moja na natarajia kumfikisha mahakamani kesho (Jumatatu),” alisema kamanda huyo.

Alisema mtu huyo wamemkamata kutokana na ushirikiano mzuri wa raia wema na jeshi la polisi na aliwataka wananchi kuzidi kushirikiana na idara yake ili kutokomeza kabisa biashara hiyo.

Leave A Reply