The House of Favourite Newspapers

Kuzimu Na Duniani-19

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

Nilikubali kwa kutingisha kichwa kwamba nimewaelewa vizuri sana. Mara, mlangoni tukasikia sauti ya mke wangu akiendelea kuimba zile nyimbo za Injili, wale wanawake majini wakafutika haraka sana mbele ya macho yangu na kuniacha mimi natetemeka kwa wasiwasi na woga.

SASA ENDELEA MWENYEWE…

 Mke Wangu aliingia ndani na ndoo yake ya maji huku akiwa hana wasiwasi wowote. Nilikaa kwa kuogopa. Mwili ulitetemeka wenyewe.

“Bado unachota maji?” aliniuliza mke wangu.

“Ndiyo, mpaka nifikishe ndoo kumi,” alinijibu kwa sauti iliyojaa ujasiri wa hali ya juu.

Nilijiuliza wale majini kabla ya kukimbia walitaka kuniambia nini zaidi maana walianza kwa kumlaumu mke wangu kwamba amepata bahati, amesaidiwa. Nikawa najiuliza sana.

Lakini pia nikajiuliza je, ni sahihi kwa mimi kuendelea kuwaamini majini huku viashiria vya wazi kwamba, hawana uwezo wa kumzidi Muumba vikiwa wazi?

“Mbona siku za mwanzo waliweza kujitokeza mbele ya mke wangu na kuongea na mimi? Kwa nini leo wasifanye vilevile ili nipate ujumbe kwa njia sahihi?” nilijiuliza mwenyewe.

Mke wangu alipotua ndoo ile, akachukua nyingine na kutoka. Kawaida yake akishajaza ndoo saba, baada ya hapo anajaza pipa kubwa. Nilimpa pole wakati akitoka.

Ile anatoka tu, wale majini wakarudi na kunifokea sana. Wakaniambia kwamba mawazo yangu kuwa wao hawana nguvu si sahihi.

“Sisi hatujashindwa kutokea huku mkeo akiwepo ila sema tu kwa sababu tunamuweka kwenye eneo ambalo asiwe na shaka tena kwamba kuna kitu tofauti.

“Tulipokuwa tunakutokea na yeye akiwepo aliweza kubaini mengi sana hasa kwa vile alikuwa akiona upepo unatikisa nyumba.

“Sasa kwa sababu umeamua kutokutuamini tunaondoka na wewe na utaishi tunapotaka sisi na utafanya kazi tunayotaka sisi,” alisema jini mmoja kwa sauti iliyojaa hasira.

Palepale mmoja wao akanifuata, akanishika kichwani, nikahisi kuchanganyikiwa na kupoteza uwezo wa kuona. Nilipokuja kufumbua macho, nilikuwa kwenye chumba chenye watu kibao, kama hamsini hivi na kila mmoja alikuwa bize na mambo yake.

“Kaa hapo,” sauti iliniamuru.

Nilikaa haraka sana. Nikasikia sauti nyingine ikisema:

“Utapewa kazi maalum muda si mrefu.”

“Sawa,” nilikubali huku nikitetemeka. Nilijua yote yale yalikuwa yakinipata kwa sababu ya kuwaza kwangu. “Kumbe majini wanaweza kujua tunawaza nini?” Nilijiuliza mwenyewe kisha nikayafuta haraka sana mawazo hayo ili nisije nikapewa adhabu nyingine.

“Simameni,” sauti moja yenye kishindo kikuu iliamuru.

Tulisimama wote ndipo nilipobaini kuwa, hatukuwa kiasi cha hamsini. Tulizidi hata watu mia mbili. Tulibanana sana japokuwa tulikuwa kwenye chumba kikubwa kupita kawaida.

“Mtatoka nje hapo, mtajua mnakwenda wapi na kufanya nini!” ilisema sauti.

Palepale tukaanza kutoka. Mzee mmoja akaniuliza:

“Hivi hapa ni wapi?”

“Mimi ni kama wewe. Nahitaji kujulishwa.”

“Hapa ni sehemu ambayo watu wa duniani waliochukuliwa na majini wanakutana na kufindishwa mbinu za kuumaliza ulimwengu kwa njia ya mauji, magonjwa mbalimbali au vifo vya kutatanisha,” alisema mtu mmoja, naamini ni jini kwani alitutokea mbele yetu ghafla huku akitembea kuelekea mlango mkuu wa kutokea.

Akaendeela kusema akinikazia macho mimi:

“Mfano wewe, kule Mlandege unakoishi ni salama lakini baadhi ya maeneo si salama. Iringa nayo imo kwenye orodha ya miji ambayo ina makao ya majini wakubwa. Ogopa sana pale njia panda ya kwenda Tosamaganga. Ogopa sana pale nje ya Uwanja wa Sabasaba. Ogopa sana pale Milima ya Gangilonga kwani ndipo penye lango kuu.

“Mji ambao kwa sasa tunapambana nao kwa sababu wakazi wake wanatusumbua ni Mkimbizi. Anga la mji ule ni zito kwetu na tunapambana kila siku.

“Ndiyo maana kuna makanisa yanaanzishwa halafu yanadumaa. Mkimbizi tunafanya kazi kubwa ya kuhamisha watu ikibidi hata nje ya mkoa ili wabaki wenye kuchangamana.”

Aliposema Gangilonga ndiko kwenye lango kuu, palepale nikakumbuka kwamba, nilipokwenda ujinini siku zile, niliporudi nilifika mjini nikitokea kwenye milima hiyo. Kumbe ni ya lango kuu la kuzimu!

Lakini ukiachana na hayo, lingine ni hayo maeneo ambayo yalitajwa kuwa ni hatari. Niliifikiria njia panda ya kwenda Tosamaganga, nikaufikiria mji wa Mkimbizi kwamba una wakazi wanaowasumbua majini. Lakini hapa sikuwa makini kujua hasa wanasumbua kivipi!

Ghafla mawazo yaliyonijia ni ya mke wangu. Kwamba, kule alipo, akirudi kutoka kwenye maji na kutonikuta, atajua nimekwenda wapi na kufanya nini.

“Kila mmoja atege sikio sasa ili tuelekezane,” ile sauti ilisema. Nikashangaa kwamba kumbe wote tulishatoka nje.

   Je, wewe msomaji unajua kilichotokea? Usikose kusoma wiki ijayo kwenye gazeti hili.

Leave A Reply