The House of Favourite Newspapers

Kuzimu Na Duniani-8

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

Nilibaini pia kwamba, nilikuwa nimetokea kwenye nyumba za eneo hilo ambazo zipo jirani na milima. Hivyo nilitembea kwa mwendo wa kuchoka mpaka nikafika eneo la Shule ya Msingi Gangilonga.

SASA ENDELEA MWENYEWE…

Nikatoka hapo tena nikatembea hadi kwenda kutokea kituo cha daladala cha kwenda mjini lakini mimi nilipitiliza hadi Mlandege.

Nilifika nyumbani, nikakaribishwa na mke wangu huku akinipa pole na kazi za siku hiyo. Nilishangaa sana kugundua kuwa, hakuwa akijua lolote kuhusu mimi. Hakujua yaliyonipata.

“Mke wangu unaniona nipo kawaida?” nilimuuliza, akacheka na kujibu:

“Kwani umebadilika nini mume wangu?”

“Je, nikisema natoka mbali sana?”

“Mbali ahera au?”

“Mbali ni ahera tu?” nilimuuliza.

“Na kuzimu labda.”

Nilishtuka kumsikia akijibu hivyo, nikanyamaza na kuanza mazungumzo mengine mbali na hayo. Lakini ghafla upepo mkali sana ukavuma mle ndani kwangu, nikawa na wasiwasi mkubwa kwani iliashiria kwamba, upepo ule ungeweza kuanua hata paa la nyumba kwa jinsi ulivyokuwa mkali.

“Ni nini hii hali?” aliniuliza mke wangu, sikumjibu kitu. Sikumjibu kwa sababu mimi mwenyewe nilihisi ni upepo uliotokana na jamaa zangu wale, yaani majini.

Kufumba na kufumbua, sura ya jitu la kutisha ilionekana juu ya dali ikiniangalia kwa hasira na kusema:

“Si ruhusa hata kumwanishia mke wako mazungumzo ambayo yatampa wasiwasi. Wakati unatoka, mimi nilikwambia ya kule yawe ya kule. Usalama wa maisha yako upo kwa kutunza kila tulichosema. Sawa?”

“Sawa,” nilijibu kwa kutetemeka, palepale upepo ukatulia na ile sura mbaya ikapotea.

Ilikuwa sura yenye umbile la binadamu mwenye masikio marefu kupita ya sungura. Macho yake yalikuwa ya duara tena mekundu sana. Alipokuwa akizungumza na mimi, midomo yake ilikuwa ikitoa miale ya moto. Lakini alinukia manukato mazuri.

“Mume wangu yaani mimi nakulalamikia kuhusu upepo wewe unaimba nyimbo za dansi. Ina maana ndiyo ulikuwa unaufukuza upepo au?”

“Nilikuwa naimba wimbo gani wa dansi?” nilimuuliza mke wangu.

“Si ulikuwa ukiimba wimbo sijui wa bendi gani ya zamanai sana.”

Palepale nilinyamaza kimya. Nilibaini kwamba, kumbe kule kusema kwangu na ile sura, mke wangu alisikia kama naimba. Moyoni nilisema safi sana, kumbe sijabainika na ndiyo uhai wangu unavyotakiwa kulindwa kwa mujibu wa ile sauti.

Usiku uliingia sana, nikaenda kuoga, nikarudi kula, ukafika muda wa kwenda kulala. Mke wangu akasema anatangulia, ana usingizi. Mimi niliendelea kubaki sebuleni kwa muda nikiwa naanza kuhisi kama kusinzia vile.

Ghafla nikawa kwenye barabara kuu ya kutoka Iringa mjini kwenda eneo la Kihesa. Nilisimama katikati ya barabara eneo la Miyomboni ambapo gari moja lilikuwa linakuja kwa mwendo wa kasi kutoka eneo ambalo zamani kulikuwa na Jengo la Sinema la Highland, nikalinyooshea mkono, likanikwepa mimi na kwenda kutumbukia kwenye mtaro pembeni.

Kishindo cha hilo gari wakati wa kufika kwenye mtaro kilifuatia na ukimya wa hali ya juu. Nikajua waliokuwemo ndani ya gari hilo, mawili. Wamefariki dunia au wamejeruhiwa vibaya sana, kiasi kwamba hawawezi hata kuzungumza.

Nilitembea kwa mwendo wa kawaida mpaka pale. Bado vumbi jingi liliifunika gari kiasi kwamba ilikuwa si rahisi kujua kuna nani na nani ndani yake.

Ghafla nilizungukwa na watu watatu, wa aina ya kule ujinini. Ni wanawake wote. Kila mmoja, mkononi alishika bakuli la bati.

Walinifuata, mmoja akanishika mkono wangu wa kushoto na kuutingisha kwamba ananipongeza kwa kazi nzuri.

Kisha wao wakatembea hatua kwa hatua mpaka kwenye gari kabisa, wakafungua mlango mmoja ambapo mlango wa pili, gari liliulalia wakati wa kupinduka. Mimi niliendelea kusimama kuwaangalia.

Baada ya dakika kama moja tu, wakatoka wakiwa na mabakuli yao. Nilibaini ndani ya mabakuli hayo mlikuwa na damu kwa sababu ya wekundu!

Wakaja mpaka niliposimama mimi, wakasimama sanjari. Kufumba na kufumbua wakapotea usoni mwangu. Kufumba na kufumbua, mimi nikaamka kitandani, nyumbani huku nikikohoa kwa nguvu.

Nilishangaa kumwona mke wangu akiwa macho, hana hata lepe la usingizi.

“Mbona hulali? Huna usingizi?” nilimuuliza mke wangu.

“Nashangaa, sina usingizi wala sitaki kulala. Sijui kuna nini? Chumba nakiona kizito sana lakini jioni nilikwenda kanisani, mchungaji akaniambia nina majaribu mazito sana mbele yangu, nijitahidi kumwomba Mungu.”

Nilishtuka kwa maneno hayo ya mke wangu. Kwangu yaliashiria kwamba, kiroho mchungaji wake alijua kuna jambo ndani ya familia yangu.

Itaendelea wiki ijayo.

“Ungelala ili ijulikane moja, kesho tutaendelea na mambo mengine,” nilimwambia.

Lakini kabla ya kulala, akaniangalia na kusema: “Lakini na wewe mbona kama ulikuwa unaweweseka ukiwa usingizini halafu unaota ndoto za ajabuajabu?”

“Ni hali tu. Kwani wewe hujawahi kuweweseka?” nilimjibu.

“Nimewahi lakini wewe zaidi. Halafu nikawa nasikia kama sauti za wanawake zikikupongeza. Ilikuwa nini?”

Nilishtuka sana kusikia hivyo kwani kama unakumbuka ndugu mwandishi ni kweli wale wanawake walinipongeza kwa kazi nzuri ya kupindua gari. Lakini nilijiuliza, inawezekana kweli kwamba, mtu akusikie upo kwenye ndoto unazungumza halafu akawasikia na unaoongea nao?!

Nilikataa moyoni lakini nikasema kama ni kweli, basi mke wangu atakuwa anapewa ujumbe kupitia nguvu kubwa ya Mungu.

Comments are closed.