The House of Favourite Newspapers

Waziri Alipokiri Kuwa Mchawi-25

ILIPOISHIA WIKIENDA

“Kama mmelipata hilo gari ninashukuru sana. Gari langu liliibiwa usiku na kunisababishia usumbufu mkubwa.” 

“Liliibiwa usiku?” 

“Ndiyo. Kama saa tano usiku nilikuwa katika hoteli moja pamoja na mke wangu. Tulipotoka gari likawa halipo.”

 “Uliripoti kituo gani?”

 “Sikuwahi kuripoti kituo chochote. Nilikuwa nije niripoti asubuhi hii.”

 “Sasa fika hapa kituoni, kuna maswali.”

 “Kuhusu hilo gari au…?” 

“Ndiyo kuhusu hili gari na kuhusu wewe mwenyewe. Ikiwezekana fika na mke wako.”

 SASA  ENDELEA…

Suala la kufika kituo cha polisi pamoja na mke wangu lilikuwa haliwezekani. Kama nimeweza kuwadanganya polisi kuwa gari langu liliibiwa usiku, nisingeweza kumdanganya mke wangu ambaye alikuwa anajua nilikuwa ofisini usiku na kwamba sikuwa naye katika hoteli yoyote.

Ingekuwa vyema kama ningetangulia kumwambia kuwa nilipokuwa narudi kutoka ofisini kwangu nilipitia hotelini kukutana na mtu mmoja na nilipotoka nikakuta gari limeibiwa.

 Lakini kwa vile sikumwambia mke wangu uongo huo pale usiku niliporudi, ingekuwa vigumu kumwambia wakati ule wa asubuhi.

 Na kama nitaamua kwenda naye kituo cha polisi kama wito wa polisi ulivyonitaka, nilizidi kujiambia, mke wangu angeshtuka kusikia madai ya kuibiwa gari hilo nje ya hoteli wakati anachojua yeye ni kuwa nilikuwa ofisini kwangu.

“Natumaini umenisikiliza vizuri?” Sauti ya msemaji wa polisi ikasikika kwenye simu baada ya ukimya mfupi ambao niliusababisha mimi.

“Ndiyo, nimekusikia. Nitafika na mke wangu,” nikamwambia.

Simu ya upande wa pili ikakatwa.

Wakati nakirudisha chombo cha kusemea niliyapitisha macho yangu kumtazama mke wangu aliyekuwa amelala nyuma yangu, nikashtuka kuona ananitazama kwa makini.

“Kumbe umeamka?” nikamuuliza.

“Ulikuwa unazungumza na nani?” akaniuliza.

Sikuwa na jibu la haraka. Sikujua ningemjibu nini kwani sikuwa na uhakika kuwa alinisikia au hakunisikia. Sikuwa nikijua aliamka saa ngapi na kunisikiliza.

“Ulikuwa unazungumza na nani?” mke wangu akaniuliza tena alipoona nipo kimya.

“Unaniuliza mimi?”

“Jamani! Kwani tuko wangapi hapa, baba kijacho unaumwa?”

Nikajiuliza; “Sijui nimwambie? Lakini nitaanzia wapi? Na nisipomwambia ukweli pengine ameshanisikia…!”

“Ulikuwa unazungumza na mwanamke wako ndiyo sababu hutaki kusema?”

“Hapana. Ni simu imetoka ofisini.”

“Asubuhi hii kuna ofisi ya nani?”

 Nikajidai kucheka baada ya kuona uongo wangu ulikuwa umedunda.

Kimoyomoyo nilijiambia nikibadili maneno, mke wangu ataniona muongo.

 “Kuna baadhi ya maafisa walibaki ofisini. Wameniambia kuwa wamekamilisha kazi na wameondoka.”

“Mume wangu nakuona hivi hivi unanidanganya.”

Ili kuyakatiza yale mazungumzo nikashuka kitandani.

“Nikudanganyie nini mke wangu. Nimekueleza ukweli,” nilimwambia na kuelekea maliwatoni.

Dakika chache baadaye nikawa nimeshavaa suti yangu tayari kwa kutoka. Nilifahamishwa kuwa dereva wangu wa gari la serikali alikuwa akinisubiri nje ya geti. Nikamuaga mke wangu na kutoka.

Kabla ya kujipakia kwenye gari nilimpigia simu dereva wa mke wangu ambaye alikuwa akiendesha lile gari lililokamatwa.

“Martin bado uko nyumbani?” nikamuuliza.

“Ndiyo nataka kutoka hivi.”

“Unajua lile gari liliibiwa usiku lakini sikumwambia mke wangu.”

“Liliibiwa wapi?”

“Nilikuwa kwenye hoteli moja pale Kinondoni. Nilipotoka gari halipo. Lakini polisi wameshalikamata. Nimepigiwa simu asubuhi hii.”

“Limekamatwa wapi?”

“Sijui. Lakini ninachotaka kukwambia tukutane pale kituo kikuu cha polisi. Mimi nakuja hapo, nataka nikukute hapo.”

“Sawa mheshimiwa nitafika.”

“Panda hata bodaboda uwahi kufika. Nitakurudishia pesa yako.”

“Sawa.”

“Tafadhali usimfahamishe mke wangu chochote.”

“Sitamwambia kitu.”

Nikakata simu na kujipakia kwenye gari. Badala ya kuelekea ofisini kwangu nilimwambia dereva anipeleke kituo kikuu cha polisi.

Wakati dereva analiwasha gari hilo na kuliondoa, mawazo yakaanza kunijia. Nilijiuliza hao polisi walitaka kunihoji kuhusu nini na mke wangu walitaka kumhoji nini?

Wasiwasi wangu ulikuwa ni endapo gari langu lilionekana nilipoliegesha wakati nilipokwenda kumuwangia waziri mkuu.

Je, nini kiliendelea?

Usikose kufuatilia kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda siku ya Jumatatu.

Comments are closed.