The House of Favourite Newspapers

Kwa Haya Yanayotokea, Nina Wasiwasi Mkubwa na Hatma ya Tanzania Kesho

0

 

IJUMAA iliyopita, nikiwa naendelea na majukumu yangu ya kikazi, nilikutana na habari iliyokuwa ikioneshwa kwenye runinga ya mtandaoni (online television) ya kampuni yetu iitwayo Global TV Online. Ilibidi niache kila nilichokuwa nakifanya, nikaikodolea macho simu yangu na kutazama kwa makini kilichokuwa kikitokea.

 

Ilikuwa ni habari ya mazishi ya kijana Salim Mohammed Almas aliyeuawa kwa kupigwa risasi na polisi, Mei 14, mwaka huu jirani na mashine ya kutolea fedha benki (ATM), Kurasini jijini Dar es Salaam.

Kwa wafuatiliaji wa mambo mtakumbuka kwamba kifo cha Almas kimesababisha msu­guano mkali baina ya pande mbili, ndugu wa marehemu na jeshi la polisi ambao mpaka leo ninapoandika makala haya bado haujapatiwa ufumbuzi.

 

Si lengo langu kukumbushia nini kilichotokea lakini kwa kifupi, sakata la Almas siyo jambo lina­lopaswa kupuuzwa kwa sababu ukifuatilia kwa makini msuguano uliokuwepo, kila upande unaen­delea kutetea unachokiamini na kinachoonekana sasa, sakata zima linahama na kuchukua sura ya udini.

Kwa kifupi, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam lililokuwa chini ya Kamanda Si­mon Sirro (kabla hajapandishwa cheo), lilieleza kwamba Almas alipigwa risasi kwenye jaribio la ujambazi. Likaendelea kueleza kwamba yeye na wenzake, wa­likuwa wakijaribu kupora fedha kutoka kwenye ATM hiyo.

 

Msimamo wa jeshi la polisi haujawahi kubadilika, wameen­delea kushikilia msimamo kwamba aliyeuawa ni jambazi. Wakati jeshi la polisi likiamini hivyo, upande wa ndugu, ma­rafiki, jamaa na waumini wa dini aliyokuwa akiiamini Almas, wanaeleza kitu kingine tofauti kabisa.

Wanaeleza kwamba ndugu yao, hakuwa jambazi na wala hana re­kodi ya matukio yoyote ya uhalifu. Almas anaelezwa kwamba enzi za uhai wake, alikuwa imamu msaidizi wa msikiti aliokuwa akisali na kama hiyo haitoshi, alikuwa mwanafunzi wa teknolo­jia ya mawasiliano (ICT) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ngazi ya stashahada.

 

Mvutano huo ulianza kama masihara, baadaye ndugu wak­agomea kuchukua maiti ya ndugu yao mpaka pale jeshi la polisi litakapokanusha taarifa kwamba aliyeuawa hakuwa jambazi bali walifanya makosa na kumuua raia asiye na hatia. Ikawa ni vuta nikuvute, mwili ukasota mochwari kwa siku 47 mpaka juzi Ijumaa ndugu walipoamua kwenda kuusitiri, huku kauli ‘tata’ zikitolewa na waumini waliohudhuria mazishi hayo, wengi wakiwa ni viongozi wa juu wa kidini.

 

Sitaki kusema nani alisema nini kwa sababu itakuwa ni kama nachochea na kamwe hilo si len­go langu, ninachotaka kukisema hapa, kauli zilizotolewa, kuanzia kwenye Msikiti wa Kichangani, Magomeni mpaka makaburini, zinaashiria jambo baya sana.

Tayari suala la udini lime­anza kuingizwa kwenye sakata hilo na hakujawahi kutokea vita mbaya duniani kama vita ya kidini. Najua lazima watatokea watu wa kuanza kuchochea kati ya pande mbili zinazovutana kwa sababu wahenga walisema siku zote kwamba kamba hukatikia pabovu.

 

Tayari kuna ufa umetokeza, waumini wa dini ya Kiislam wanaona kwamba mwenzao ameuawa si kwa sababu alikuwa jambazi, bali kwa sababu ya dini yake. Ukisikiliza pia kauli za jeshi la polisi, nako kuna utata mkubwa, hasa wanapohusisha tukio hilo na imani za watu.

Jamani, chondechonde, bado majeraha makubwa ya Kibiti, Mkuranga na Rufiji hayajapona, tusianzishe janga lingine ambalo hatutaweza kulituliza likichach­amaa. Chondechonde wanasiasa, msilichukulie tatizo hili kama mtaji wenu wa kisiasa, najua ni kwa namna gani familia ya Al­mas ilivyoumia kwa kumpoteza mpendwa wao.

 

Uchungu unazidi maradufu kwa sababu wanaamini ndugu yao amebandikwa sifa mbaya ya ujambazi wakati wanaamini hakuwahi kuiba chochote. Ni ra­hisi kupenyeza chuki kwa ndugu, jamaa, marafiki na waumini wenzake Almas na watu pekee wanaoweza kufanya hivi, ni wa­nasiasa uchwara.

Hebu sote tuunganishe ngu­vu kumomba Mungu aepushie mbali janga hili. Viongozi wangu wa nchi, ni hatari sana kuyan­yamazia matukio kama haya kwa sababu taratibu yanajenga matabaka, Muislam ataamini anaonewa kwa sababu ya dini yake, Mkristo naye ataamini hivyohivyo, mwisho mpasuko utakuwa mkubwa na kama nilivy­osema, hakuna anayeweza ku­uzima moto wa ubaguzi wa kidini, Mungu aepushilie mbali.

 

Waulize watu wa Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati (CAR) jinsi ubaguzi wa kidini ulivyoichakaza nchi yao na kuiacha ikiwa na magofu, makaburi, viwete na yatima. Mifano ipo mingi sehemu mbalimbali duniani, ambapo mambo kama haya yaliachwa na mwisho yakajenga sumu mbaya mno ya ubaguzi.

Wote tunaoitakia mema nchi hii, tupinge vikali siasa zozote za chuki zinazoweza kupandikizwa katikati, tuungane kuwaombea wafiwa waliompoteza ndugu yao, kijana wao, kaka, imamu, rafiki na mwanafunzi wenzao, hakuna namna pengo lililoachwa na mpendwa wao linaweza kuzi­bika lakini naamini kila mmoja kwa imani yake, bila kujali imani yake, akishiriki kuwaombea kwa Mungu awape wepesi wafiwa, tunaweza kuvuka katika wakati huu mgumu tunaopitia.

 

Yote tisa, kumi ni haya ya­nayoendelea Kibiti, Mkuranga na Rufiji. Mambo hayapo sawa Kibiti, Mkuranga na Rufiji! Mambo hayapo sawa Pwani! Ndugu zetu wanaendelea kupoteza maisha bila kuwa na hatia, idadi ya vijana wetu, wazee wetu, viongozi wetu na askari wetu inazidi kuongeze­ka, kila kukicha unasikia tukio jipya limetokea kama siyo Kibiti, basi ni Mkuranga au Rufiji.

Yalianza kama masihara, akauawa wa kwanza, wa pili, wa tatu… mpaka ninapoandika makala haya, zaidi ya roho 38 zimekwenda! Narudia tena, laz­ima mtu yeyote mwenye uchungu na nchi hii afumbue mdomo na kuzungumza! Hatuwezi kukaa kimya!

Hebu mamlaka zinazohusika zitueleze, nini kinaendelea Kibiti, Mkuranga na Rufiji? Alhamisi ya Aprili 13, 2017, nilisafiri kwenda Mtwara kwa ndege ya Shirika la Ndege la Precision Air na baada ya kumaliza kilichonipeleka Mt­wara, niliianza safari ya kurejea Dar es Salaam lakini safari hii, ni­likuja kwa barabara kwa sababu siku hiyo hakukuwa na ndege ya kurudi Dar es Salaam.

 

Ni siku hiyo ndiyo ambapo kulitokea tukio baya ukanda huo, kwa askari nane kusham­buliwa na hatimaye kuuawa kwa kupigwa risasi na hawa wauaji. Ninaposema mambo hayapo sawa, namaanisha kwa sababu nilipita eneo la tukio saa chache tu baada ya mauaji.

Harufu ya damu ilitawala eneo hilo, damu ya vijana wetu, tena wengine wakiwa wadogo kabisa, ambao walijitolea kutulinda sisi raia na mali zetu. Walikuwa wameuawa kinyama utafikiri wao ndiyo majambazi. Iliniuma sana na nakumbuka niliporudi Dar es Salaam, kwa kutumia ukurasa huuhuu niliandika hisia zangu hapa.

 

Ni miezi mitatu tu imepita lakini bado hali inazidi kuwa mbaya, mauaji yanazidi kushika kasi. Kinachoumiza vichwa vya wengi, ni namna mauaji hayo yanayovyofanyika.

Naomba nirudie kuweka sawa jambo moja! Mimi kama Mtan­zania, mzalendo, nachukizwa sana na haya yanayoendelea kwa sababu siyo siri, yanaharibu mno taswira ya taifa letu. Nata­mani kufanya jambo kukomesha mauaji haya lakini hata sijui nifanye nini.

Kwa kuwa mbali na kuwa Mtanzania wa kawaida, mimi pia ni mmiliki wa vyombo vya habari, Gazeti la Uwazi, lililo chini ya Kampuni ya Global Publishers, ni miongoni mwa vyombo vya habari vilivyokuwa vya kwanza kabisa kuripoti kuhusu kikundi cha watu, waliokuwa wakiua viongozi wa vijiji huko Mkuranga.

 

Sisemi haya kwa kutaka kujisi­fia, hapana. Wajibu wa vyombo vya habari ni kuibua matatizo ili wahusika wayaone na kuyapatia ufumbuzi haraka, kazi ambayo Gazeti la Uwazi na mengine ya kampuni yetu, yaliifanya kika­milifu.

Hata hivyo, juhudi zetu za kuibua ukatili huo dhidi ya bin­adamu wenzetu uliokuwa uk­iendeshwa katika ukanda huo, mamlaka husika zilituona kama wachochezi, nakumbuka mara kadhaa tuliitwa Idara ya Habari (Maelezo), ugomvi wetu mkubwa na mamlaka husika ukiwa ni ku­waita wauaji hao ‘magaidi’.

 

Ilionekana kama kwa kuwaita jina hilo, tunapandikiza hofu kwenye mioyo ya Watanzania, tunaichafua taswira ya nchi yetu nje ya mipaka na kwa sababu kama nilivyosema hapo awali, mimi ni mzalendo ninayeipenda nchi yangu, tulisitisha kutumia neno ‘magaidi’ kwenye habari zetu, tukaamua tu tuendelee ku­waita wauaji au majambazi kama ambavyo jeshi la polisi limekuwa likisisitiza mara kwa mara.

Naliheshimu sana Jeshi la Polisi, namheshimu sana ali­yekuwa IGP, Ernest Mangu na namheshimu sana mkuu wa jeshi hilo kwa sasa, kaka yangu, IGP Simon Sirro. Heshima yangu si ya maneno matupu, la hasha! Namaanisha kile ninachokisema.

Nani ambaye anabisha kwamba jeshi letu, vijana wetu chini ya uongozi wa hawa ma- IGP, wa­nafanya kazi kubwa sana ka­tika kupambana na uhalifu? Ule ujambazi wa kutumia silaha mi­taani, umepungua sana, mambo ya kukabwa na vibaka, yamepun­gua sana, tunaishi kwa amani na familia zetu. Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni.

 

Lakini wengi wasichokijua, wewe unapokuwa umelala na familia yako, mnakoroma, kuna vijana wako mitaani usiku kucha, wakiwa na bunduki zao, wakizun­guka huku na kule kuhakikisha hakuna mhalifu anayesumbua raia na mali zao mitaani.

Wanahatarisha maisha yao, baridi ya usiku, mbu, wakati mwingine mvua, vinawaishia wakiwa wanatekeleza majukumu yao.

Vijana hao, ni askari wetu wa jeshi la polisi, ambao baadhi ya watu wasio na utu, wana­posikia wameuawa huko Kibiti, wanashangilia, wanasahau kazi kubwa wanayoifanya.

 

Matendo ya askari wachache wasio waaminifu, yanawafanya baadhi yetu wawahukumu wote kwamba hakuna wanachokifanya zaidi ya kuonea raia.

Narudia tena, mnyonge mnyon­geni lakini haki yake mpeni! Pamoja na heshima yangu kwenu walinzi wetu wa usalama, na­taka kuzungumza nanyi kidogo, yawezekana hoja yangu ikawa ndogo lakini ina maana kubwa.

 

Kwa nini wananchi wa Ukanda wa Rufiji, Mkuranga na Kibiti wanawaona nyie kama adui zao? Kwa nini wapo tayari kushiriki­ana na wahalifu kwa kuficha siri kuliko kushirikiana nanyi katika kutoa taarifa zinazoweza kusaidia kuzuia matukio hayo?

Sina uzoefu na mambo ya kijeshi lakini kwa uelewa wan­gu mdogo, siamini kama kuna oparesheni yoyote ya kijeshi inayoweza kufanikiwa kwa ku­tumia ‘maguvu’ pekee. Huwezi kupambana na majambazi au wauaji kwa kutumia ubavu tu kwa sababu tofauti na nyie ambao huwa mnavaa sare na kubeba silaha, mhalifu hana alama.

Mtu pekee anayeweza kumjua mhalifu, ni yule anayeishi naye jirani. Kwa lugha nyepesi, jamii ndiyo inayowajua wauaji wa Mkuranga, Kibiti na Rufiji. Kwa hiyo, jambo la kwanza ambalo vyombo vyetu vya ulinzi na usala­ma vinapaswa kulitilia nguvu, ni kurejesha imani kwa wananchi, wasiwaone polisi kama adui zao ambao kazi yao ni kuwatesa, kuwanyanyasa, kuwapiga na ku­waumiza bila hata hatia.

 

Ulinzi shirikishi ndiyo dawa pekee itakayomaliza mauaji haya, kila mwanajamii ajione kuwa se­hemu ya ulinzi, kila mmoja aone jukumu la kuzuia mauaji haya ni lake. Hili likifanyika, jinamizi hili litaisha mara moja na zitabaki stori tu.

Ni ushirikiano mzuri na jamii ndiyo unaoweza pia kulisaidia jeshi la polisi pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, kwamba wanachokitaka wauaji ni nini hasa (kama kipo)! Machafuko mengi duniani, humalizwa kwa diplomasia tu.

 

Tanzania ni kubwa kuliko Kibiti, Mkuranga na Rufiji! Watanza­nia ni wengi kuliko wa Kibiti, Mkuranga na Rufiji lakini pia Watanzania wanaoishi Katavi, Mbeya na Songwe hawana to­fauti na wale wanaoishi Mkoa wa Pwani. Hebu tuunganishe mikono pamoja, tushikamane na kwa pamoja tuseme ‘NO’ kwa mauaji yanayoendelea Mkoa wa Pwani.

Nazipongeza juhudi za jeshi la polisi za kuanzishwa kwa kanda maalum ya kipolisi ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji (Mkiru) itakayoon­gozwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Onesmo Lyanga, wananchi tumuunge mkono, hakika tutashinda.

Tukiyazingatia yote niliyo­yasema, kesho yetu itajawa na nuru lakini tukienda tofauti, sijui hatma ya taifa letu siku za usoni. Mungu ibariki Tanzania.

ITAENDELEA WIKI IJAYO

Kumbukumbu za Kweli za Maisha Yangu-200 | ERIC SHIGONGO

====

Hatimaye Denti UDSM Aliyeuawa na Polisi kwa Tuhuma za Ujambazi Azikwa Kisutu

Leave A Reply