The House of Favourite Newspapers

Kwa Kasi ya Yanga… Simba Wajipange Ligi Kuu Bara, Wabanwa Kaitaba na Kagera

0

MPANGO wa kutofungwa mchezo wake wa 11 kwa kipa namba moja wa Simba, Aishi Manula, ulikwama mbele ya Kagera Sugar baada ya jana kuruhusu bao dakika ya 15 kutoka kwa beki, Deus Bukenya, wakati matokeo yakiwa; Kagera Sugar 1-1 Simba.

Katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Kaitaba uliopo mkoani Kagera, Simba ilikuwa na kazi ya ziada ya kufanya baada ya kutanguliwa kwa bao hilo.

Safu ya ulinzi ya Simba inayoongozwa na Henock Inonga, itajilaumu yenyewe kwa kushindwa kujipanga vizuri wakati wakiokoa kona iliyopigwa na Ally Kagawa, kabla ya kumkuta mfungaji ambaye alipiga kichwa cha kuparaza, mpira ukajaa wavuni.

Iliwabidi Simba wasubiri mpaka dakika ya 38 kupata bao la kusawazisha kupitia kwa beki wake, Henock Inonga ambaye aliunganisha kwa kichwa pigo la faulo lililopigwa na Mohamed Hussein.

Makosa yaleyale ya mabeki wa Simba, yalihamia kwa Kagera Sugar ambao walikuwa wakicheza kwa kujilinda baada ya kupata bao mapema, wakaruhusu washambuliwe na wageni wao kusawazisha.

Kipindi cha kwanza, pongezi kwa Manula ambaye aliokoa hatari dakika ya 42, kisha ikajibiwa na kipa wa Kagera Sugar Said Kipao dakika ya 43 kwa kuokoa pigo la kichwa cha mshambuliaji Moses Phiri.

Katika dakika 45 za mwanzo, nyota wa Kagera Sugar, David Luhende, alionyeshwa kadi ya njano dakika ya 23 kama ilivyokuwa kwa Yusuph Lwenge (dk 19) na Abdallah Mfuko (dk 45).

Kipindi cha pili, mashambulizi yalikuwa ya kushtukiza ambapo makocha wa pande zote mbili, Mecky Maxime wa Kagera Sugar na Juma Mgunda wa Simba, mabadiliko ya wachezaji waliyoyafanya, hayakubadili ubao wa matokeo, mwisho wa mchezo ikawa sare ya 1-1.

Sare hiyo imeifanya Simba kuendelea kusalia nafasi ya pili ikifikisha pointi 38 baada ya kucheza mechi 17, vinara ni Yanga wenye pointi 44 ambapo kasi yao, ni lazima Simba wajipange ili kupindua meza, la sivyo, ubingwa watausikia tu kama msimu uliopita.

Matokeo ya mechi zingine zilizochezwa jana ni; Tanzania Prisons 2-0 Dodoma Jiji na Geita Gold 1-1 Azam.

AHMED ALLY AKIRI – “TUMEKUWA na MATOKEO MABAYA, KUNA KAUGUMU kwa KAGERA”…

Leave A Reply