The House of Favourite Newspapers

KWA MABADILIKO HAYA..LULU WA LEO KABADILIKA AU KABADILISHWA ?

HAPA duniani kila binadamu ameumbiwa matatizo, yaani kila mmoja yanaweza kumpata na yanapomtokea mtu inakuwa ni njia nzuri ya kujifunza kwani kama alikosea jambo fulani ni vigumu kuja kurudia kulikosea kwa mara nyingine tena. Katika watu ambao wamepitia kwenye changamoto za maisha wakiwa na umri mdogo ni staa wa filamu za Kibongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’ ambaye alipatwa na masaibu ya kumuua aliyekuwa msanii mwenzake, Steven Kanumba bila kukusudia na kuhukumiwa kwenda jela miaka miwili. Wakati akiendelea na kifungo Mungu siyo mwanadamu, akamfanyia muujiza ambapo alipata msamaha wa kifungo cha nje ambacho alimaliza Novemba mwaka jana.

Baada tu ya kumaliza kifungo, mambo yalianza kumnyookea kwani alivishwa pete ya uchumba na mchumba wake ambaye ni bosi wa redio EFM, Francis Ciza ‘Majizo’. Baada ya pete bata likaanza kwani Lulu na mchumba wake huyo walienda nchini China kwa mapumziko na habari kueleza kuwa, wamefunga ndoa ya kimyakimya huko.

LULU WA ZAMANI

Lulu wa sasa siyo yule wa zamani. Mabadiliko yake ni makubwa. Zamani mrembo huyu alikuwa ni mtu wa kujiachia mitandaoni lakini siku hizi ni nadra sana kumuona ameposti kitu, akiposti ni mara moja sana tena labda picha. Achana na hilo, pia Lulu alijulikana kama malkia wa mitindo iwe ya nguo au nywele. Lulu alikuwa akipamba kwenye mitandao hasa Instagram kwa kubadili nguo za kila aina pamoja na kubadili mitindo ya nywele kila kukicha ambapo mabinti na wanawake wengi walikuwa wanaiga mitindo ya kushona nguo na kusuka nywele kutoka kwake.

LULU WA SASA

Kwa sasa Lulu ana mabadiliko makubwa, kwani mambo yote aliyokuwa akiyafanya zamani hayafanyi tena. Amekuwa mpole, hasikiki na mambo yake amekuwa akiyafanya kimyakimya. Ile mitindo ya nguo aliyokuwa akibadili kila kukicha kwa sasa hakuna tena, mara nyingi anavaa nguo za heshima zile ndefu mpaka miguuni, wakati mwingine madera. Hivi karibuni aliachia picha mpya ambazo tena alienda kufanya ‘photoshoot’ akiwa amevaa dera, watu wengi walionekana kushangazwa na hilo kwani hapo awali haikuwa kawaida yake.

Isitoshe Lulu baada ya kumaliza kifungo ile mitindo mbalimbali ya nywele haionekani kwake tena, amekuwa akisuka nywele za kawaida za twende kilioni na maisha yanasonga. Kwa sasa pia siyo mtu wa kujichanganya hata na wasanii wenzake kwani muda mwingi anaonekana kuwa beneti tu na mchumba wake, Majizo.

KABADILIKA AU KABADILISHWA?

Ni ukweli usiopingika kwamba maisha yanabadilika. Na hayo mabadiliko ndiyo yamemkuta Lulu, huenda amebadilika kutokana na changamoto alizopitia, amebadilishwa au umri nao umechangia kwani mtu anapozidi kukua kiumri ndivyo hata kiakili anakua zaidi. Inawezekana ule ulikuwa ni utoto na sasa akili za utu uzima zimemjia ndiyo maana kaamua kutulia.

Kubwa kuliko yote inawezekana kabadilishwa na mchumba wake kwani kwa sasa ni mchumba rasmi wa mtu. Huenda mfumo wake wa kimaisha umebadilika kwa sababu anakwenda kuwa mke wa mtu au mama wa familia hivyo ili awe mke au mama bora lazima aachane na yale mambo ya ujana na awe mtulivu.

MASHABIKI WANAMMISS

Mashabiki wengi wameonekana kummiss Lulu hasa wanawake ambao walikuwa wakiiga mitindo ya nguo na nywele kutoka kwake kwani wamekuwa wakitoa maoni yao huku wengine wakidai kuwa huenda mwanadada huyo ni mjamzito au kakatazwa na mchumba wake Majizo kuendelea na staili yake ile ya maisha ya zamani.

KUTOKA RISASI JUMAMOSI

Pongezi kwako Lulu kwa kuonesha mabadiliko makubwa katika maisha yako, iwe umebadilika kwa sababu ya matatizo uliyopitia au kwa kuwa wewe ni mchumba wa mtu, kikubwa unachotakiwa kufanya ni kuyalinda mabadiliko hayo.

Unaelekea kwenye ndoa, usije ukajisahau ukaupeleka ustaa mpaka kwa mumeo kwani ukifanya hivyo ni rahisi maisha ya ndoa kukushinda kama mastaa wengine ambao hawadumu kwenye ndoa kwa kuwa wanaendekeza ustaa mpaka ndani kwa waume zao.

Comments are closed.