The House of Favourite Newspapers

KWA MISINGI HII, KAMWE PENZI LAKO HALITADUMU

TUANZE kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia siku hii njema. Kama kawaida hapa huwa tunazungumza mapenzi na maisha kwa jumla. Karibu!

Jamani tukubaliane kwamba ndoa ni taasisi nyeti mno kwa sababu inatengeneza familia ambayo baadaye inakuwa jamii na mwisho ni taifa na dunia kwa jumla.

Mtu yeyote mwenye akili timamu, hawezi kuingia au kuunda taasisi hii bila kufikiri kwa kina na kufanya uamuzi kwa umakini mkubwa. Epuka sana kukurupuka kuingia kwenye ndoa.

Ndoa ni mkataba wa maisha na siyo jambo la muda mfupi, siyo jambo lelemama ndiyo maana huwa tunasema ndoa si kwa ajili ya mvulana na msichana bali mwanaume na mwanamke.

Mkifanya makosa katika kuchaguana, kifuatacho ni majanga kwa wote wawili. Tunapaswa kufahamu kuwa ndoa ni kura ya turufu katika maisha. Kura hii hupigwa mara moja tu hivyo ukikosea inakuwa imekula kwako mazima.

Ndoa kwa wanaoamini ni agizo kutoka kwa Mungu hivyo ndiye huwa anatoa mwenza wa maisha.

Katika makala haya nimelenga kukuonesha misingi au kanuni ambazo zikifuatwa, kamwe maisha ya ndoa au mapenzi hayawezi kudumu;

NGONO

Mara nyingi vijana huwaza kuingia kwenye uhusiano au mapenzi ili kufaidi ngono. Sasa wanapofika huko na kukutana na mwenza ambaye hastahimili vishindo vya ngono, hapo ndipo tatizo huanza. Kama unataka kuingia kwenye ndoa, futa mawazo hayo.

HISIA

Tatizo kubwa linalojitokeza kwa baadhi ya watu ni kupenda ghafla. Anajikuta akimuona tu mtu na kutamani kuingia kwenye ndoa kutokana na hisia za mwili.

HOFU

Wapo wanaojikuta wamenasa au kushindwa kuendelea kuwa kwenye ndoa kwa sababu waliingia kwa hofu ya kukosa mwenza hivyo wakajikuta wamezoa yeyote aliyemkubalia bila kumfanyia tathmini.

SHINIKIZO

Wengine wamejikuta kwenye ndoa kutokana na shinikizo kutoka kwa wazazi, ndugu, marafiki au kuona umri umekwenda hivyo kudumu ni vigumu mno.

MAJUKUMU

Wengine huolewa au kuoa ili kukimbia kazi na majukumu ya nyumbani hivyo kufeli ni lazima.

PESA

Mbali na shinikizo, lakini pesa ni sumu nyingine bila kujali kuwa pesa hununua kitanda, lakini haiwezi kununua usingizi.

HURUMA

Wengine huolewa au kuoa kutokana na kumuonea mtu huruma. Yaani mwanamke anakutana na mwanaume mwenye shida fulani, anamwelezea hadi anatokwa machozi kisha anamhurumia na kumsaidia halafu wanajikuta kwenye uhusiano kisha ndoa. Hapa napo kufeli ni lazima!

KUJIDANGANYA

Mwanamke mwingine anaambiwa kabisa kwamba mwanaume fulani ni mvuta bangi, lakini anajidanganya kwamba atambadilisha! Anapofeli kumbadilisha ndipo mambo yanakwenda mrama.

UZURI

Kuna wale wanaozingatia uzuri na kusahau tabia. Hapa ndipo wanaume wengi huingia mkenge kirahisi. Kujipodoa kwa baadhi ya wanawake kumewaponza vijana walio wengi. Katika mazingira kama haya, ujue kabisa msingi ni mbovu hivyo huwezi kufika mbali kwenye ndoa.

UJAUZITO

Kuna wanaume wengine wamejikuta kwenye ndoa baada ya kumpa binti wa mtu ujauzito usiotarajiwa. Mwanaume hujikuta akimuonea huruma mwanamke aliyempa mimba na kuamini kuwa kumuoa ndiyo suluhisho na hakuna

namna nyingine. Hapa napo kufeli ni lazima kwa sababu anakuwa ameingia kwenye uhusiano akiwa na msukumo wa nje na siyo mapenzi ya dhati.

WAZAZI

Kuna wengine hujitahidi kuingia kwenye ndoa ili kuwafurahisha wazazi. Kwa kuwa tu mama au baba au wote wanampenda binti fulani, basi humshawishi kijana wao kumuoa, matokeo yake hawafiki mbali.

MUHIMU

Tukubaliane kwamba mambo haya ni ya muhimu mno na endapo yakitumika kama vigezo vya kuingia kwenye ndoa, kufeli ni lazima hivyo ni vyema kuwa makini mno.

Kwa maoni au ushauri, tumia namba hiyo hapo juu au tembelea ukurasa wetu wa Gazeti la Ijumaa Wikienda kwenye Facebook.

Comments are closed.