The House of Favourite Newspapers

Kwa Mwanangu Nitakayemzaa

0

ILIPOISHIA 

Kabla ya tukio la kuvamia makao makuu ya Amisom halijapoa Mtima na Abdulrahman wanasafiri hadi Nairobi, Kenya walikofanya mauaji ya kutisha kwenye supamaketi maarufu nchini humo iliyokuwa inamilikiwa na Destiny.

Wakati wakiendelea kutenda tukio hilo la simanzi kupitia kitundu kidogo toka chini ya meza alikokuwa amejificha Destiny, anaona alama fulani kwenye mkono wa haramia mmojawapo iliyomshtua sana!

SONGA NAYO…

“Mungu wangu!” Destiny aliongea taratibu.

Akazidi kuyakazia macho yake kwenye mkono huo akagundua kuwa hayakuwa yanamdanganganya, kovu aliloliona lilifanana kabisa na lile alilowahi kuliona miaka mingi iliyopita mkononi kwa rafiki yake Mtima aliyemwambia lilitokana na kuunguzwa na pasi ya umeme.

Akajiuliza haramia huyo aliyekuwa anaua watu bila huruma alikuwa Mtima na mwenziye ni Abdulrahman lakini hakuweza kupata jibu haraka hadi alipokuja kuhakikisha pale wauaji hao walipokuwa wanakimbia na kitambaa cha huyo aliyemshuku kuwa ni Mtima kudondoka chini akaiona sura yake.

Destiny alijikuta akipigwa na butwaa kuliko kawaida, katika maisha yake yote hakuwahi hata siku moja kuwaza kuwa Mtima angekuja kufikia hatua hiyo, akajikuta analia kwa uchungu, alimsikitikia zaidi kijana huyo na jinsi soko lake lilivyokuwa limeharibika pamoja na watu wote waliouawa na kujeruhiwa.

Wakati huo kwa mbali vingo’ra vya polisi vilikuwa vinasikika na walifika katika supamaketi hiyo baada ya muda mfupi tu tangu kutokea kwa tukio hilo, wakawachukua majeruhi na kuwakimbiza hadi katika Hospitali ya Jomo Kenyatta,marehemu wote walihifadhiwa huko kusubiri taratibu za kipolisi kufanyika ili watu wawatambue ndugu zao.

***

Uharibifu uliotokea kwenye kituo cha biashara cha Destiny ulikuwa ni mkubwa sana, ukiondoa binadamu waliofariki na kujeruhiwa hasara ya samani zilizoteketea ilikuwa ni zaidi ya shilingi za Tanzania, milioni 300.

Hiyo ilikuwa ni hasara kubwa mno kwa Destiny iliyomsababisha baadaye kukata tamaa ya kuendelea na biashara hiyo, akawaambia washirika wake alihitaji kulipiga mnada soko hilo na kufanya mambo mengine!

“Kwa nini umeamua hivyo?” Bi Lucy Okelo, mama yake mzazi alimuuliza baada ya kumpa taarifa hizo.

“Basi tu.”

“Lakini ni mapema mno kukata tamaa.”

“Nafahamu hilo lakini nimekwisha amua.”

“Unatakiwa kufikiri mara mbili juu ya uamuzi wako.”

“Siwezi kurudi nyuma nitatafuta jambo lingine la kufanya kuniwezesha kuishi.”

“Mh!”

Kila mmoja aliyezisikia taarifa za Destiny kuuza soko lake alionekana kushangazwa nazo sana, ukweli ni kwamba kwa wengi hayakuonekana kuwa maamuzi ya busara kutokana na kutoifahamu sababu iliyosababisha yeye kufanya hivyo lakini mwisho wa yote hakuna ambaye angemlazimisha kubadilisha alichokuwa ameamua.

Ambapo baada ya mwezi mmoja kupita Destiny alikuwa amekwisha liuza soko lake kwa wafanyabiashara wengine.

***

Kitu ambacho hawakukifahamu watu wengi, Destiny aliamua kukiuza kituo chake cha biashara ili tu kuianza kazi ya kumtafuta Mtima, ambapo baada ya kumaliza taratibu za kukiuza kituo hicho alihitaji kupata wasaa mzuri wa kulitafakari kwa kina jambo hilo.

Siku tatu zikapita akishinda amejifungia kwenye chumba chake akiwaza aianzie wapi kazi hiyo baada ya kutafakari kwa kina alipata mawazo mawili ambayo alihisi kumsaidia, kuwa mwanajeshi au mwandishi wa habari!

Akatafakari kwa kina kuhusu kuwa mwanajeshi, kazi ambayo hakuwahi kuvutiwa nayo kabisa katika maisha yake yote!

Alimfahamu mwanajeshi kuwa ni mtu aliyeishi chini ya sheria muda mwingi, kutegemea kupambana zaidi na mtu asiye na makazi ya kueleweka. Akatafakari kuwa mwandishi wa habari!

Hiyo nayo ilionekana kuwa kazi ngumu, kuwa mwandishi wa habari kwake kulimaanisha siku zote atatakiwa kuwa nyuma ya watu akitafuta matukio, kufahamu nini kinaendelea ulimwenguni na kuwafahamisha watu wengine.

Hayo aliyaona kuwa maisha ya kitumwa lakini kuliko kuwa mwanajeshi alichagua uandishi wa habari.

Je, nini kitaendelea? Usikose wiki ijayo.

Leave A Reply