The House of Favourite Newspapers

Kwa Mwanangu Nitakayemzaa-45

0

Destiny yuko mahututi katika Hospitali ya Agha Khan kutokana na ajali mbaya aliyoipata wakati anawafuatilia akina Mtima. Upande wa pili wa simulizi hii Mtima na rafiki yake kipenzi Abdulrahman wanajikuta wakiingia katika mgogoro mkubwa baada ya kuanza kukwaruzana kutokana na Mtima kuonesha mabadiliko ya kitabia.Je, nini kiliendelea? Teremka nayo…

“Unafanya nini?” Abdulrahman alimuuliza Mtima.
“Huoni?”
“Naona ila sikuelewi!”
“Nimechoka kufanya mauaji.”
“Kwa sababu zipi hasa?
“Basi tu, nimechoka.”

“Dah!” Abdulrahman aliguna huku akishindwa kuamini kile alichokuwa anakiona na kusikia, alijiuliza rafiki yake huyo aliingiwa na mdudu gani kichwani lakini hakuweza kupata jibu.
Ghafla kijana huyo mwenye asili ya Kiarabu alijikuta akijawa hasira moyoni mwake, bila kutegemea akainua bunduki yake na kumnyooshea Mtima.

“Unataka kuniua?” Mtima alimuuliza Abdulrahman huku akimtazama kwa macho makavu.
“Ndiyo.”
“Haya niue.”

Baada ya maneno hayo Mtima alisimama wima na kumtengea kifua Abdulrahman huku akimsisitiza ampige risasi na kumuua, lakini kijana huyo alibaki akimtazama tu huku mkono wake ukiwa umeshika kwenye kidude cha kufyatulia risasi, akipambana na roho iliyokuwa inamshawishi amtwange risasi rafiki yake huyo nyingine ikimtaka asifanye hivyo.

Mwishowe hasira zilishuka, Abdulrahman akaamua kuushusha mkono wake chini kisha akamsogelea Mtima wakakumbatiana huku wote wakilia kwa uchungu utadhani watoto wadogo.
“Nimechoka kuua Abdu!” Mtima aliongea baada ya kuachiana.
“Kwa nini?”
“Basi tu.”

“Lazima kuna sababu.”
“Tunatenda dhambi!”
“Kipindi cha nyuma hukulifahamu hilo?”
“Nililifahamu.”

“Sasa…?”
“Shetani alinipitia.”
Ukweli ni kwamba maneno ya Mtima yalimshangaza sana Abdulrahman. Hakupenda kabisa kuamini kuwa yale aliyokuwa anayasikia yalitoka kinywani kwa Mtima, aliyemshawishi kujiingiza katika masuala ya kijasusi kwa kuua watu ovyo huku akidai yalikuwa ni malipo waliyostahili wanadamu kutokana na kile walichomtendea mama yake mzazi Abikanile.

Taratibu Abdulrahman alijikuta akikosa neno la kuongea, nguvu zikamuishia akajikuta akikaa chini, kwa kasi ya upepo mawazo mengi yalianza kupishana ndani ya kichwa chake akiwaza jinsi alivyonusurika kifo mara kadhaa walipokuwa kwenye viwanja vya mapambano.

Abdulrahman akajutia mambo mengi, kama si Mtima alifahamu wakati huo angekuwa amepiga hatua kubwa kwenye maisha yake hasa kutimiza ndoto alizokuwanazo za kuwa mwanajeshi wa Jeshi la Somalia siku moja.

Kwa upande wa Mtima wakati huo hakuwa tayari kabisa kuendelea kuua kama walivyokuwa wanafanya kila mara.Ndoto za kulipiza kisasi kutokana na mabaya ambayo binadamu walimtendea mama yake mzazi zilikuwa zimeyeyuka kabisa akilini mwake, alichowaza wakati huo ni juu ya dhambi aliyokuwa anaifanya ya kuua watu wasiokuwa na hatia.

Siku hiyo ilikatika Mtima na Abdulrahman wakiwa kwenye maficho yao hapo katika maeneo ya Jiwe Kuu lakini hawakuwa wanaongea hata kidogo, muda wote walikuwa kimya kila mmoja akionekana mwenye mawazo sana.
***
Destiny alikuwa bado kwenye chumba cha uangalizi maalumu (ICU), akiwa ameunganishwa kwenye mipira iliyopitisha gesi ya oksijeni kutoka kwenye mitungi yenye gesi hiyo, pia madaktari wa hospitalini hapo waliendelea kumhudumia ili kuhakikisha anarudi kwenye hali yake ya kawaida.

Siku zilizidi kusonga mbele mwanamke huyo akiwa katika hali hiyo lakini baada ya kupewa huduma bora kwa muda wa miezi tisa na madaktari bingwa chini ya uangalizi wa mzee Boti, msichana huyo alirejewa na fahamu, miezi michache mbele akapona kabisa.

“Mungu mkubwa,” mzee Boti alimwambia siku moja Destiny.
“Ni kweli, ninakushukuru sana mzee, Mungu atanilipia kutokana na ukarimu ulionitendea.”
“Usijali, Mwenyezi Mungu alituagiza upendo.”
“Kweli kabisa.”

Siku hiyo Destiny na mzee Boti waliongea mambo mengi sana, mwanamke huyo akamsimulia kisa kizima kilichosababisa mpaka yeye kufikia hatua ya kupata ajali pia kuharibika sura yake baada ya kuunguzwa na moto wa mabomu yaliyolipuka kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Mzee huyo alisikitishwa sana na simulizi hiyo lakini zaidi alishangazwa na upendo aliokuwa nao Destiny kwa Mtima, kiasi cha kuhatarisha maisha yake bila kuogopa kuwa angeweza kufa.
“Bado unampango wa kumtafuta?” mzee Boti alimuuliza baada ya maongezi ya muda mrefu.
“Haswaa!!”
“Huogopi kufa?”

“Kwa ajili yake niko tayari kwa lolote lile.”
“Mh!”
“Nampenda sana, ninahitaji abadilike na kuwa binadamu mwenye moyo wa huruma.”

Mzee Boti alibaki mdomo wazi, upendo aliokuwanao msichana huyo ulikuwa wa nadra sana kuukuta kwa binadamu wengi katika karne hiyo, hakupenda kumvunja moyo zaidi alimuahidi kumuunga mkono katika kila hatua hadi pale ambapo angeitimiza azma yake.
Je, nini kitaendelea? Usikose wiki ijayo.

Leave A Reply