The House of Favourite Newspapers

Kwa Mwanangu Nitakayemzaa-47

0

ILIPOISHIA:

 

Abdulrahman alikuwa amedhamiria kumuua Destiny. Bila huruma yoyote akiwa kwenye maficho yake katika mapango ya Kuchungu anamchukua msichana huyo kisha kwenda kumuweka sehemu maalum kwa ajili ya kulikamilisha zoezi hilo kisha anachomoa kisu kikubwa kilichonolewa vyema.

Kabla ya kuuawa Destiny aliomba angalau sekunde kadhaa kutubu dhambi zake ili afikie mahali pema peponi pale mwili wake utakapotengana na roho. Abdulrahman alikubaliana na hilo, msichana huyo akapiga magoti taratibu kisha kuanza kusali, ile anamaliza tu bila kutegemea risasi zilianza kurindima katika eneo hilo!

 

TAMBAA NAYO…

ABDULRAHMAN alishtuka na kutupa kisu pembeni kisha akaichomoa bastola yake kiunoni. Bila kupoteza muda aliruka mfano wa nyani kwa sarakasi hadi upande mwingine kulikokuwa na silaha zake za mapambano kisha akaanza kujibu mashambulizi bila kufahamu ni nani aliyekuwa anapambana naye na kwa sababu zipi!

Kwa upande wa Destiny naye alijikuta akichanganyikiwa, huku akitetemeka kwa woga alikimbilia upande mwingine wa pango hilo na kujificha nyuma ya jiwe kubwa.

Mapambano yalizidi kuwa makali, sehemu hiyo ikageuka kuwa uwanja wa kivita, jambo lililomshangaza Abdulrahman ni pale alipochunguza kwa makini na kugundua kuwa watu aliokuwa anapambana nao walikuwa wamevaa mavazi yaliyowatambulisha kuwa ni wanajeshi wa Kikosi cha Majeshi ya Umoja wa Mataifa (Amisom).

Alijiuliza wanajeshi hao walifahamu vipi alikuwa mahali hapo lakini hakuweza kupata jibu, kwa ujasiri mkubwa alipiga moyo konde na kuendelea kupambana lakini ilifikia hatua alianza kuhisi kuzidiwa nguvu baada ya kuishiwa risasi!

Abdulrahman akaamua kuitupa bunduki aliyokuwa nayo mkononi kisha akakimbilia mpaka chini kabisa ya pango hilo, akatafuta sehemu iliyomfaa na kujificha akisubiri muujiza wa Mungu kumuokoa.

Kwa upande wa wanajeshi wa Amisom walizidi kulizunguka pango hilo kwa tahadhari kubwa maana walifahamu mtu waliyekuwa wanapambana naye alikuwa ni hatari kwenye uwanja wa kivita, wengine walipita upande wa kushoto, wengine kulia na juu, mwisho wakazama ndani ya pango.

Akiwa amebana nyuma ya jiwe kubwa Abdulrahman alianza kuvisikia vishindo vya hatua za wanajeshi, moyo ukamlipuka, hofu ya kukamatwa ikatanda.

Kwa haraka kijana huyo wa Kiarabu aliwaza afanye kitu gani lakini hakuweza kupata jibu. Moyo ulikuwa unamdunda na kutokana na hali halisi, alifahamu ni lazima angekamatwa.

Kweli kama alivyokuwa anawaza, baada ya saa zima kupita akikwepana na kundi hilo la wanajeshi, Abdulrahman alijikuta akiwa amezungukwa kila kona na kutiwa mbaroni.

Hasira walizokuwa nazo wanajeshi wa Amisom dhidi ya kijana huyo kutokana na maafa aliyokuwa ameyasababisha akiwa na Mtima zilikuwa hazielezeki, ukweli ni kwamba walipomtia tu mikononi walimtesa sana huku wakimshinikiza aseme alipo Mtima jambo ambalo Abdulrahman alikuwa halifahamu.

Barabarani kote kuelekea Kenya, wanajeshi hao walimfunga Abdulrahman miguu kwenye gari na kuiacha sehemu yake ya kichwa ikigusa chini kwenye lami. Aliburuzika kichwa chote kikabondeka, hadi gari hilo linafika kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya, Namanga, Abdulrahman alikuwa amekwishapoteza maisha muda mrefu.

Baada ya kufika nchini Kenya, kupitia vyombo vya habari msemaji wa Jeshi la Amisom alitangaza juu ya kuuawa kwa kijana huyo, watu wengi walifurahishwa nayo isipokuwa familia yake. Walimlilia sana lakini hawakuwa na uwezo wa kuibadilisha hali halisi, walichokifanya ilikuwa ni kumuombea kwa Mungu asamehewe dhambi zake na kufikia mahala pema peponi.

***

Hadi wakati huo Mtima hakuwa anafahamu jambo lolote lililomtokea Abdulrahman, baada ya kukosana naye na kutengana alikuwa anaendelea na maisha yake kama kawaida na alionekana kuyafurahia sana.

Kila mara alikuwa anaongozana na Manyama kwenye shughuli za uvuvi na wakati mwingine shambani kulima, pia wakati huo alikuwa amekwishajenga nyumba ya kuishi kwenye kiwanja alichopewa na Manyama zaidi alianzisha uhusiano wa kimapenzi na msichana wa Kisukuma aitwaye Keja.

Maisha yakasonga huku uhusiano ukizidi kukomaa na ilifikia hatua wakawa wamepanga waoane, Mtima alimshirikisha Manyama aliyepanga kumsaidia katika kila hatua hadi atakapoifanikisha azma yake hiyo.

“Kile kule ni nini?” Mtima alimuuliza Keja akimuonyesha kwa kidole.

“Sielewi?”

“Siyo mtu kweli?”

“Inawezekana, lakini atakuwa amefikaje huku?”

“Hatuwezi kujua, hebu ngoja…”

Mtima alianza kupiga hatua kuelekea sehemu hiyo kulipoonekana kuna mtu alikuwa amelala katika shamba lao hilo. Walipofika walijikuta wakipigwa butwaa baada ya kumuona mtu akiwa katika hali mbaya mno huku akionekana kuwa na makovu mengi ya moto usoni na tumbo lake lilikuwa limeingia ndani jambo lililomaanisha alikuwa na njaa kali.

Mtima na Keja waliamua kumsaidia wakamkokota na kuelekea naye hadi mahali walipokuwa wanaishi. Walimfanyia pia huduma ya kwanza, wakampa chakula baadaye alilejea katika hali yake ya kawaida kabisa.

Je, nini kitaendelea? Ni nani huyo aliyeokotwa na Mtima? Usikose Jumamosi ijayo.

Je, nini kitaendelea? Usikose Jumamosi ijayo.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

Leave A Reply