The House of Favourite Newspapers

Kwa Mwanangu Nitakayemzaa -50

0

Destiny na Mtima wako nchini Kenya hotelini katika mapumziko kabla ya Mtima kuelekea nchini Uholanzi. Wakiwa katika chumba hicho cha hoteli wawili hao wanajikuta wakidumbukia katika dimbwi zito la mahaba jambo lililosababisha wafanye mapenzi kabla hata ya kuingia kwenye ndoa. Pia baada ya tendo hilo wawili hao walibakia wamekumbatiana huku wakiambiana maneno matamu kwa zamu.
SONGA NAYO…

KULIPOPAMBAZUKA, majira ya saa mbili, Destiny na Mtima waliamka na kuelekea bafuni, baada ya kujimwagia maji na kujiweka sawa walikwenda kupata kifungua kinywa kwenye mgahawa uliokuwa ndani ya hoteli hiyo kisha baada ya hapo Destiny alimsaidia Mtima kufanya taratibu za safari yake ya kuelekea Uholanzi.
Ambapo walikwenda hadi kwenye ofisi za Shirika la Ndege la Emirates zilizopo katika Mtaa wa Kibaki Kona, pembeni ya Barabara ya Jaramongi  Oginga wakakata tiketi iliyomtaka Mtima kusafiri usiku wa siku hiyo hadi India ambako angepanda ndege iliyoelekea barani Ulaya.

“Kwa heri mpenzi,” Destiny alimnong’oneza Mtima wakiwa wamekumbatiana baada ya muda wa safari kuwadia.
“Ubaki salama D.”
“Asante, usafiri salama pia.”
“Usijali, tutaonana baada ya siku chache.”
“Sawa mpenzi.”
Destiny alimsindikiza Mtima kwa macho huku machozi yakiwa yanambubujika wakiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta mpaka alipoishilia sehemu zilikoegesha ndege, baada ya kufanyiwa ukaguzi akaingia ndani ya ndege ya Boeing 565AK, yenye uwezo wa kubeba abiria takriban 200.
Baada ya kuingia kwenye ndege hiyo na kukaa kwenye siti yake ndani ya dakika 15 baadaye ndege hiyo ilikuwa mawinguni na ilifika India saa 10 usiku, alfajiri ya siku hiyo Mtima alibadili ndege na kuchukua ya Shirika la Europe Safe iliyomfikisha katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Amsterdam baada ya saa 18 kupita akiwa safarini. Uwanjani hapo alikodi teksi iliyompeleka nyumbani kwao.

***
Hali ya hewa ilikuwa tulivu mno asubuhi hiyo, nyumbani kwa mzee Johannes shughuli za kawaida zilikuwa zinaendelea pia. Hayo yalikuwa ni majira ya saa mbili za asubuhi ambapo mzee Johannes, mkewe na familia yote wakiwa wanapata kifungua kinywa, mara walisikia kengele ya mlangoni ikigonga, akaenda kufungua msaidizi wa kazi za ndani wa nyumbani hapo.

“karibu,” alimkaribisha mgeni aliyekuwa amesimama mbele yake huku amebeba begi mgongoni na dogo mkononi.
Baada ya kukaribishwa Mtima aliingia ndani huku akiwa ameupamba uso wake kwa tabasamu pana hadi pale alipogonganisha macho yake na mzee Johannes, mkewe na wanafamilia wengine.
“Mtima,” mzee Johannes aliita akiwa mwenye wasiwasi sana. “Umekuja kutuua?” aliuliza kabla Mtima hajazungumza.
“Hapana, nimerudi nyumbani babu.” Mtima alijibu kwa upole.
“Si kweli!”
“Ni kweli, nimebadilika, sasa si Mtima yule muovu ni mwingine kabisa.”
Ukweli ni kwamba lilikuwa jambo gumu nyumbani pale kuamini kuwa Mtima aliamua kuachana na shughuli ya kufanya mauaji aliyokuwa anaifanya, lakini huo ndiyo ulikuwa ukweli, baada ya kukaa kitako na kijana huyo aliwaeleza nini hasa kilichosababisha  hadi akafikia uamuzi huo.
Familia nzima ilifurahi mno na kumpongeza Mtima baada ya kuyasikia maelezo yake, lakini pia walimfahamisha Alile mama yake mdogo juu ya ujio wa kijana huyo, naye ilikuwa vigumu kuamini hadi pale alipokwenda nyumbani kwa mzee Johannes na kumuona.

Siku hiyo ikapita kila mmoja katika familia  hiyo akiwa mwenye furaha kupindukia, siku iliyofuata walimpeleka Mtima kuzuru kwenye kaburi la mama yake mzazi Abikanile, Rotterdam.
Akiwa katika kaburi hilo, Mtima alilia sana huku akiomba msamaha kwa mabaya aliyoyatenda, aliapa kutokurudia badala yake alihamishia nguvu katika kuwasaidia watu wenye ulemavu wa ngozi Afrika baada ya kuwezeshwa na mzee Johannes na kujenga kituo kiitwacho African House of Albinism kilichoshirikiana kwa ukaribu sana na Kituo cha  DICOPE (Different Colour One People), kilichomilikiwa na mama yake mdogo Alile na mumewe Max Dean.
Siku zikazidi kusonga mbele baada ya mwaka mmoja kupita Mtima alifunga ndoa na Destiny katika Kanisa la Anglican huko Amsterdam baada ya kumfanyia mwanamke huyo upasuaji wa ngozi (Plastic surgery) na kuondoa makovu yote usoni kwake. Baadaye walipata watoto mapacha wa kike waliowaita Isabella na Gabriella.

MWISHO!
Asante sana kwa kuwa nami kuanzia mwanzo wa simulizi hii mpaka leo inafika tamati, wiki ijayo nitaianza safari nyingine ya simulizi iitwayo Sitalipa Kisasi, usikose.

Leave A Reply