Kwa nini hawara ale cha mkeo?

couplehavingwineinbedonvalentinesdaysexbummers.jpgAsalam alaikum, bwana Yesu asifiwe. Poleni kwa majukumu ya wikiendi na ni matumani yangu wazima na wale wagonjwa nawaombea dua mtapona ishallah.

Nashukuru kwa kunisoma kwani napata ujumbe wenu na naona jinsi mnavyofaidika kwa mada ninazowaletea.

Ukiandika kitu ukaona watu wanakutafuta na kukupa hongera unajivunia kwani unaamini wanakipenda kile unachowaandikia.

Leo nimekuja na mada hii ili kuwasema akina baba wenye tabia ya kuchukua pesa za wake zao na kwenda kuwapa mahawara wakati mke anajinyima na kutafuta kwa ajili ya watoto ambao mmezaa.

Hebu sikia kisa cha huyu mama ambaye amenisababisha mimi kuandika mada hii.

MSIKIENI WOTE

“Mimi ni mama wa watoto watatu, nimekuwa najishughulisha na biashara ya genge baada ya kuona hali ni ngumu. Mume wangu anafanya kazi lakini hata akipata fedha ni vigumu mimi kuiona.

“Kinachoniuma zaidi, mume wangu amekuwa ni muumini wa pombe na wanawake na ndiyo maana amekuwa hatoi fedha. Akipata mshahara unaishia huko kwa mahawara na pombe.

“Siku moja alikuja na kuniomba nimkopeshe fedha zangu ambazo nilizikusanya kupitia genge. Kwa sababu ni mume wangu nilimpatia akaniahidi kunirudishia. Kiukweli ilikuwa ni nyingi. Aliniambia ana biashara anataka kuanzisha kitu ambacho nilikiona ni kizuri.

“Cha kushangaza, siku zilikatika, sisikii biashara yoyote kuwepo ndiyo nikaamua kumhoji kitendo ambacho hakukipenda.

“Tulilumbana mpaka akanipiga. Hata hivyo, nilichunguza nikabaini kampangishia nyumba dada mmoja ambaye niliwahi kuambiwa anatembea naye,” alisema msomaji huyo ambaye alikuwa ana uchungu.

Hebu jipe nafasi hiyo wewe ambaye unamfanyia mwenzako hivyo akifanya yeye, utajisikiaje?

Baadhi ya wanaume wamekuwa wakiwatenda wake zao na kuchukua pesa zao na kuzipeleka kwa mahawara. Hivi ni kwa nini hawara ale cha mkeo?

Fanya kwa siri basi

Kama ni tabia yako hakuna wa kukubadilisha kabisa, lakini basi kama umeamua kuwa na ‘nyumba ndogo’  basi fanya kwa siri mkeo asijue na ujitahidi kutomuudhi.

Mshahara wako uhusike kwa hawara

Mkeo keshakubaliana na hali ya wewe kutomueleza pesa  unapeleka wapi? Kaamua kujifungulia kigenge kwa ajili ya kulea familia,  kwa nini fedha za mshahara zisitoshe kwa hawara wako mpaka ufikie hatua ya kuchukua na akiba ya mkeo?

Kumbuka ni chanzo cha umaskini

Kuhamisha akiba ya nyumbani kupeleka kwa hawara ni chanzo cha umaskini kwani mama atachoka kutafuta watoto watashindwa kusoma. Je, huoni kutosoma kwa watoto wako mwisho wa siku ni umaskini?

Mwanaume unayefanya hivyo tafakari kwa kina kwani hawara atabaki kuwa hawara na mke na familia ndiyo wako wa kuzikana kwa sababu hawara akipata wa kumuoa wewe utajilaumu, kwani atakuwa amekugeuza buzi ‘meeeee’.

Tuonane wiki ijayo kwa mada nyingine.


Loading...

Toa comment